SHEHENA YA MWISHO YA MABOMBA KWA AJILI YA UJENZI WA BOMBA LA GESI YAWASILI DAR ES SALAAM!!


 Katibu mkuu wizaraya Nishati na Madini, Eliakim Maswi (Watatu kushoto), akizungumza jambo na Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa (Wanne kushoto), wakati kamati hiyo ilipotembelea bandari ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kujionea kazi ya upakuaji vifaa vya ujenzi na kupokea shehena ya mwisho ya mabomba ya kupitishia gesi. Wengine ni wajumbe wa kamati hiyo, Raha Mohammed (Kulia), Richard Ndasa (Wapili kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), Yonah Kilagane.
 Katibu Mkuu wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi (Wapili kushoto), akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, ikiongozwa na mwenyekiti wake, Victor Mwambalaswa (Wakanza kushoto) kuhusu kazi ya upakuaji vifaa vya ujenzi na kupokea shehena ya mwisho ya mabomba ya kupitishia gesi bandarini jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Watatu kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), Yonah Kilagane.


 Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Victor Mwambalaswa (Wapili kulia) na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Mhe Richard Ndasa, wakiangalia kazi ya upakuaji saruji kutoka kwenye meli bandarini jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kamati hiyo ilitembelea ili kujionea kazi hiyo na ile ya kupokea shehena ya mwisho ya mabomba ya kupitishia gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, akiwaeleza wajumbe wa kamati ya bunge ya Nishati na Madini (Hawapo pichani), kuhusu kazi ya upakuaji saruji kutoka kwenye meli, bandarini jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Saruji hiyo itakayotumika kujengea mabomba ya kupitishia gesi, iliwasili sambamba na shehena ya mwisho ya mabomba hayo.
 TANZANIA  inatarajia kufaidika na matumizi ya gesi asilia ambayo yataokoa zaidi ya shilingi  Trilioni 1.6trn/- kila mwaka, mara baada ya gesi ya Mtwara kuanza kutumika katika sekta mbalimbali, mara kazi ya ujenzi wa bomba la gesi  toka Mtwara kuja jijini Dar es Salaam itapokamilika. 
 Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Victor Mwambalaswa (mb) wakati wa hafla ya kupokea shehena ya mwisho ya mabomba kwa ajili ya ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara na Songo Songo hadi Dar es S.alaam.
Mhe. Mwambalaswa amesema, kiasi hicho cha fedha ndicho kinachotumika na taifa kuagiza mafuta ya kuendesha mitambo mbalimbali ambapo baada ya gesi kufika Dar es Salaam, fedha hizo sasa zitaelekezwa kwenye maeneo mengine kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.
Mhe. Mwambalaswa amesema utekelezaji wa mradi utaleta manufaa makubwa kwa wananchi hasa maeneo gesi asilia inapopatikana. Huduma mbali mbali za jamii kama vile maji, umeme, afya, elimu na miundombinu zitatolewa au kuboreshwa. Mapato ya kodi za Halmashauri yataongezeka na ajira kwa wazawa zitaongezeka.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakimu Maswi, alizitaja baadhi  ya faida ambazo wananchi wa Mtwara na Lindi watafaidika nazo ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa mitambo ya kusafishia gesi itakayojengwa Madimba na Songo Songo: Kila mtambo utahitaji kiasi cha wafanyakazi wa moja kwa moja wapatao sitini (60) watakaoendesha mitambo hiyo. Vile vile, kutahitajika watu watakaotoa huduma ya chakula, afya, usafiri pamoja na huduma nyingine za kijamii.
Bw. Maswi ameelezea kuhusu ujenzi wa kiwanda cha saruji cha kampuni ya Dangote ambacho kitatoa ajira rasmi kwa wananchi takribani 500 na zile zisizo rasmi takribani watu 800 na ujenzi wa kiwanda kingine cha Saruji cha kampuni ya Meis kitakatoa ajira kwa wananchi takribani 1000.
Bw, Maswi amesema, wizara yake ya Nishati na Madini imetenga fungu maalam ambalo litatumika kuwapatia umeme wananchi wa vijiji vyote vinavyopitiwa na bomba gesi.
Sambamba na faida hizo za jumla, pia sehemu ya gesi itakayozalishwa katika maeneo ya Mnazi Bay, Ntorya na kina kirefu cha maji itaendelea kutumika kuzalisha umeme kwa matumizi ya mikoa ya Mtwara na Lindi pamoja na mikoa mingine inayopakana nayo, wakati kwenye matoleo ya bomba la kusafirisha gesi limeweka matoleo ya kuchukulia gesi asilia (off take) katika miji ya Mtwara, Lindi, Kilwa na Mkuranga ili kuhakikisha kuwa maeneo haya yanapata gesi asilia ya uhakika kwa ajili ya viwanda na matumizi mengine.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini, Bw. Yona Kilaghane, amesema mazungumzo ya ujenzi wa mitambo ya (LNG) yameanza kati ya TPDC, kupitia Wizara ya Nishati na Madini na Makampuni ya Statoil, British Gas (BG), Ophir pamoja na Exxon Mobil ili kuzalisha LNG kwa kutumia mtambo mkubwa utakaojengwa karibu na maeneo ya ugunduzi.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment