Mjadala wa Mabadiliko ya Katiba jana ulihamia nje ya Bunge
wakati Jaji Joseph Warioba alipomchambua mhadhiri maarufu nchini,
Profesa Issa Shivji akimueleza kuwa si mkweli bali mpotoshaji wa Rasimu
ya Katiba.
Jaji Warioba, ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, pia amemtuhumu Profesa Shivji kuwa ndiye
mwanzilishi wa chokochoko za Zanzibar za kudai serikali tatu, jambo
ambalo sasa analigeuka kutokana na kuona hali imekuwa mbaya.
Kauli ya Warioba imekuja baada ya Profesa Shivji
kuichambua Rasimu ya Katiba jana asubuhi kwenye Kongamano la Vijana
lililoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
lililokuwa na dhima ya Vijana Katika Kuimarisha na Kuendeleza Muungano
Baada ya Miaka 50. Tamasha hilo lilifanyika kwenye hoteli ya Blue Pearl,
Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.
Akiwasilisha mada kwenye kongamano hilo, Profesa
Shivji alisema katika kujadili Muungano, wananchi hawana budi kuzingatia
mambo mawili ambayo ni nchi zinazozungumziwa kwenye Rasimu kuwa ni
Zanzibar, Tanganyika au Tanzania, ambayo alisema haina mamlaka katika
pande hizo mbili za Muungano.
Pia alisema suala la maadili kwa viongozi halina
budi kuangalia kuwa linazungumzia maadili ya viongozi wa Zanzibar,
Tanganyika au Tanzania na kwamba rasimu inazungumzia viongozi wa
Tanzania ambao hawana mamlaka kwa Tanganyika na Zanzibar.
Katika majumuisho yake, Profesa Shivji, ambaye
aliikosoa Rasimu kuwa haiwakilishi matakwa ya Watanzania kwa kuangalia
sampuli zilizotumika, alisema kwamba wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba
walikuwa na nia njema.
Lakini Shivji akaenda mbali zaidi kwa kusema “the
road to hell is paved in good intention,” akimaanisha kuwa njia ya
kuzimu imetengenezwa kwa nia njema.
Akijibu hoja hizo, Jaji Warioba alisema Profesa
Shivji amegeuka maandishi yake yaliyokuwa yanachochea utaifa wa Zanzibar
na sasa anaona Tanganyika ndiyo hatari kwa Muungano.
“Shivji ni msomi na mimi najua anaelewa matumizi
ya takwimu,” alisema Jaji Warioba, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakati alipozungumza na gazeti hili
nyumbani kwake jana jioni.
“Nasema hapa, Shivji akiwa msomi, amekuwa intellectually dishonest (si mkweli kiusomi). Anapotosha kwa makusudi.”
Jaji warioba alisema Shivji ndiye amekuwa chanzo
cha uchochezi wa kitaifa Zanzibar kupitia maandishi yake. Alisema
waliokuwa wanadai serikali tatu kwa muda mrefu walikuwa wananchi wa
Zanzibar.
“Shivji alikuwa anasema Tanganyika imejificha
kwenye Muungano ili inufaike. Kwa hiyo anasema Tanganyika iwe wazi
isijifiche,” alisema Jaji Warioba.
“Na Shivji amechochea hilo… wote wale waliokuwa wanamnukuu
walikuwa wanatoa hayo kwenye maandishi yake na kwamba mpaka leo hii kuna
watu wa Zanzibar wanaamini Muungano huu si halali kisheria kutokana na
Shivji ambaye alisema Baraza la Mapinduzi halikuridhia articles (ibara)
za Muungano.”
Alipoulizwa jana usiku kuhusu tuhuma hizo za
uchochezi na chanzo cha hisia za utaifa wa Uzanzibari na Utanganyika,
Profesa Shivji alisema hawezi kujibu tuhuma hizo kwa kuwa hajamsikia
Jaji Warioba akizungumzia hilo.
“Hey, amezungumza lini?” alihoji. “Siwezi kujibu kwa kuwa sijamsikiliza mwenyewe.”
Lakini Jaji Warioba alisema watu walitumia msingi
huo kudai utaifa wa Zanzibar na kusisitiza kuwa Shivji amesababisha
hisia za utaifa na kwamba haya yanayoendelea sasa yanatokana uchochezi
huo.
“Hata kabla ya sisi kuanza mchakato huu, Shivji
alikwenda Zanzibar akazungumza na Baraza la Wawakilishi na akawaambia
issue kwa Zanzibar ni self determination (kujitambua), Sasa leo anaona
kama hatari ni Tanganyika, lakini yeye ndio amechochea nationalism
(utaifa),” alisema Jaji Warioba.
Kuhusu takwimu, Jaji Warioba alisema mara ya
kwanza Profesa Shivji alizungumzia takwimu za Zanzibar kuhusu muundo wa
Muungano akisema kuwa waliozungumzia suala hilo walikuwa 47,000, huku
watu 27,000 wakitoka Tanzania Bara na 19,000 kutoka Zanzibar.
“Safari hii ametaja zile za Tanzania Bara na
kusema hiyo ni figure (namba) ndogo sana ukilinganisha na watu 300,000
waliotoa maoni,” alisema Warioba.
Alisema Tume ilitumia takwimu zinatokana na watu
waliozungumzia suala ambalo wameliwekea asilimia na si kwa ujumla na
ndio maana anaona Profesa Shivji anataka kupotosha kwa makusudi.
Warioba alimuelezea Profesa Shivji kuwa sasa
ameamua kueneza propaganda za serikali mbili kwa kuponda Rasimu ya
Katiba ambayo inaonyesha kuwa muundo wa serikali tatu ndio unaoifaa
Tanzani kwa sasa.
Aidha, Warioba alisema msimamo wa Profesa Shivji ni kwamba Zanzibar haikukosea kubadilisha Katiba mwaka 2010.
“ Nimeshangazwa na Shivji kusema kwamba kitendo
cha Zanzibar kubadili Katiba yao kuwa ‘Zanzibar ni Nchi’ halikuwa jambo
la ajabu,” alisema Warioba.
Alisema Shivji ni msomi ambaye anafahamu kitendo cha kubadilisha Katiba kilikuwa na madhara makubwa katika muundo wa Muungano.
“Nadhani mnakumbuka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
alipoulizwa Bungeni kama Zanzibar ni nchi au siyo nchi, alijibu kuwa
Zanzibar siyo nchi, vurugu zake mnakumbuka,” alisema.
Alisema lakini msomi kama Shivji haoni kama suala
hilo la ‘Zanzibar ni nchi’ lina madhara makubwa katika mstakabali wa
taifa letu.
Jaji Warioba alisema kama serikali tatu
hazitakiwi, basi kinachotakiwa kufanywa ni kwa Zanzibar kubadili Katiba
yake ili iseme kwamba Zanzibar ni sehemu ya Muungano, vinginevyo
haiwezekani.
“Maana kama ni kusahihisha, ni lazima kwanza
Katiba ya Zanzibar itumie maneno yale yale yaliyo kwenye Katiba ya
Muungano. Yaani Zanzibar iwe sehemu ya nchi. Zanzibar wakubali hilo,”
alisema.
“Zanzibar wakubali Rais wa Muungano ana madaraka
nchi nzima maana mabadiliko ya 2010 yamemuondolea Rais wa Jamhuri ya
Muungano madaraka yake.”
Akitoa mfano wa mbunge wa Simanjiro, Christopher
Ole Sendeka, Jaji Warioba alisema amekuwa akidai takwimu hazionyeshi
uhalisia wa maoni ya wananchi.
“Kwa mfano, Jimbo la Simanjiro linakuwa na watu
100,000 lakini waliojiandikisha kupiga kura ni watu 20,000 na waliopiga
kura ni watu 15,000. Hii ina maana ushindi wake utakuwa katika watu
waliopiga kura na siyo idadi ya watu wa Simanjiro,” alisema Warioba
Chanzo;mwananchi
Chanzo;mwananchi
0 comments:
Post a Comment