Wajumbe wa Bunge la Katiba. |
Bunge Maalumu la Katiba linaendelea na
kikao chake na miongoni mwa shughuli zinazotarajiwa kufanywa kuanzia
leo, ni kurekebisha baadhi ya kanuni za uendeshaji wake na kuanza
kujadiliwa kwa ibara zilizopo ndani ya rasimu ya Katiba.
Pamoja na kazi hiyo ya kufanyia
marekebisho kanuni za Bunge, Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo Maalumu la
Katiba, Samia Suluhu Hassan akiahirisha kikao cha Bunge juzi, alisema
leo Bunge litaanza kazi ya kupitia rasimu ya Katiba kwa kuanza na Sura
ya Kwanza na Sura ya Sita.
Sura ya Kwanza inazungumzia muundo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Sita inazungumzia masuala ya Muungano.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, mjadala
kuhusu Kamati ya Bunge utafanyika kwa muda usiozidi siku mbili na baada
ya mjadala, kila Kamati itaandaa taarifa kuhusu mambo yaliyoafikiwa na
wajumbe walio wengi kwa ajili ya kuwasilishwa kwenye Bunge Maalumu.
Kanuni hizo zinasema endapo kutakuwa na
wajumbe ambao hawakuunga mkono maoni ya wajumbe walio wengi katika
Kamati, wajumbe hao wanaweza kuandaa maoni yanayohusu maeneo ambayo
hawakukubaliana nayo na yatajumuishwa kwenye taarifa ya Kamati.
Baada ya Kamati kuandaa taarifa yake,
Mwenyekiti wa Kamati inayohusika atamjulisha Mwenyekiti kwa maandishi
kuwa Kamati imekamilisha kazi yake.
Kwa mujibu wa kanuni, keshokutwa wenyeviti
wa Kamati 12 za Bunge hilo Maalumu la Katiba sasa wanatarajia
kuwasilisha taarifa za kile walichojadiliana katika sura namba moja na
sita za rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu.
Baada ya jaribio la awali kutaka baadhi ya
kanuni kurekebishwa kugonga mwamba wiki iliyopita, sasa azimio lenye
lengo hilo litawasilishwa leo.
Jaribio la awali lilishindikana baada ya
wabunge wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupinga mpango
wa kutaka kanuni hizo kurekebishwa wakati hazijaanza kutumika, wakisema
ni mbinu za kutaka kuwadhoofisha.
Walitaka kanuni za 37 na 38 pekee ambazo ziliwekwa kiporo ndizo zijadiliwe.
Ukawa kupitia kwa Mwanasheria wao, Tundu
Lissu, ulipinga jaribio hilo hata kabla ya Mwenyekiti wa Kamati ya
Kanuni na Haki za Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho kusoma azimio hilo
ndani ya bunge wiki iliyopita, huku Lissu akiita karatasi iliyokuwa na
mapendekezo hayo kuwa ni 'takataka'.
Kutokana na mzozo huo, Mwenyekiti wa Bunge
hilo Samuel Sitta alilazimika kuagiza Kamati ya Kanuni kuahirisha
uwasilishaji wa Azimio la Marekebisho hayo ya kanuni wamalize kwanza
utata ulioibuliwa na Ukawa; ambao ulisababisha kikao cha Bunge
kuahirishwa kutokana na vurugu.
Taarifa zilizomfikia mwandishi, zilisema
baada ya kutafakari kwa kina na kupitia kwa Kamati ya Maridhiano, Ukawa
wamekubali kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya kanuni baada ya kuonekana
kuwa baadhi zinawabana wabunge katika ushiriki wao kwenye vikao vya
Bunge na hata kwenye vikao vya Kamati.
Alhamisi iliyopita Mwenyekiti Sitta
alitangazia wajumbe kwamba kwa vile marekebisho ya kanuni yalikwama,
sasa Kamati zitaendesha mijadala kwa kutumia kanuni zile zile za Bunge
Maalumu.
Agizo hilo la Sitta lilionekana kuwa mwiba
kwa wabunge wengi, ambapo kanuni ya 32 inawabana kuvaa mavazi rasmi,
mjumbe kusimama anapotaka kutoa hoja hata kama wako wachache na vikao
vya kamati vitalazimika kuanza saa tatu asubuhi hadi saba mchana na
baadaye saa 10 jioni hadi saa mbili usiku, kama ilivyo kwa vikao vya
Bunge, jambo ambalo limeonekana kuwa ni mwiba mkali.
Hata hivyo inadaiwa baadhi ya kanuni
zilizotakiwa awali kuwasilishwa kwa marekebisho, hazitakuwepo kutokana
na makubaliano yaliyofikiwa ikiwemo kanuni inayohusu uamuzi kupitishwa
kwa theluthi mbili za pande zote mbili za Muungano ili utaratibu wa
kutumika uwe wa wingi wa kura.
Kanuni nyingine ambayo pia ilikuwa ifanyiwe
marekebisho na baada ya mashauriano hayo itabaki kama ilivyo, ni ya
32(1) ambayo inasema kila Kamati itajadili rasimu ya Katiba kwa wakati
mmoja kwa kuzingatia mgawanyo wa sura mbili za rasimu kwa mujibu wa
ratiba itakayopangwa na Kamati ya Uongozi.
Hatua hiyo inaondoa mpango aliotangaza
Mwenyekiti Sitta wiki iliyopita kwamba Kamati zitabadili kanuni hiyo
ziweze kujadili kanuni tatu tatu au nne nne, suala ambalo lilipingwa na
Ukawa ukidai msingi wake unalenga katika kujadili sura nyingi kwa pamoja
jambo litakaloondoa umakini.
0 comments:
Post a Comment