Kamanda Boaz akiwa ameshikilia sehemu ya malighafi zinazotumika kutengezea Konyagi Feki.Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro Robert Boaz akionesha Pombe feki ya Konyagi iliyokamatwa hivi karibuni wilayani Hai
Sehemu ya bidhaa zilizokamatwa katika kiwanda hicho zikiwa kituo cha polisi Bomang'ombe.
Kamanda Boaz akionesha mihuri ambayo imekuwa ikitumika kuonesha tarehe ya kuanza na kumalizika kwa tarehe ya matumizi ya kinywaji hicho.
Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa baada ya kukutwa wakifanya shughuli ya utengenezaji wa bidhaa hiyo feki.
JESHI la polisi mkoani Kilimanjaro limefanikiwa kunasa kiwanda cha kutengeneza Pombe "Feki" aina ya Konyagi huku likiwashikilia watu wanane waliokutwa ndani ya kiwanda hicho wakifanya shughuli za utengenezaji wa pombe hiyo.
Mbali na kiwanda na watuhumiwa hao pia Polisi imefanikiwa kunasa mitambo mbalimbali iliyokuwa ikitumika kiwandani hapo zikiwemo malighafi zilizokuwa zikitumika kufunga bidhaa hizo kabla ya kuuzwa katika maduka ya jumla ya kuuzia Pombe
Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro,kamishna mwandamizi msaidizi wa polisi,Robert Boaz alithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao Machi 14 mwaka huu majira ya saa 7:00 Mchana katika eneo la Kambi ya raha nje kidogo ya mji wa Bomang'ombe.
"Askari polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hawa baada ya wananchi kutoa taarifa za kuwepo kwa utengezaji wa Pombe ambayo haijaruhusiwa kisheria ikiwa na nembo ya Konyagi ndipo askari walianza uchunguzi na kufanikiwa kuwakamata watu hao katika nyumba inayomilikiwa na Elias Samson mwenye umri wa miaka 31"alisema Boaz.
Kamanda Boaz alisema watuhumiwa hao pia walikutwa na lita 400 za pombe ikiwa imehifadhiwa katika mapipa tayari kwa ajili ya kujazwa katika vifungashio pamoja na Katoni 46 za pombe hiyo zote zikiwa na nembo ya Konyagi.
Mbali na vitu hivyo Boaz pia alisema watu hao walikutwa na Makasha tupu 178 ya kuhifadhi Konyagi yakiwa na nembo,Pipa tupu 10 zinazoaminika kuhifadhia pombe hiyo wakati wa utengenezaji na Mihuri miwili inayoonesha tarehe ya kutengezea na tarehe ya mwisho wa matumizi ya bidhaa.
"Katika vitu vingine tulivyo wakuta navyo ni pamoja na majiko ya mafuta "Ya Mchina"zaidi ya matano,vifaa vingine ambavyo ni kama Pasi vilivyokuwa vikitumika kwa ajili ya kuchomea karatasi za nailoni baada ya kujaza hiyo Pombe"alisema Boaz.
Kamanda Boaz aliyetembelea eneo kilipo kiwanda hicho aliwataja waliokamatwa kuwa ni pamoja na George Kisivani (28), Yusuf George(33), Preygod Urassa (27) na Richard Leonard (35) Hagai Nelson (38),Jackson Shayo (29), Greyson Jonathan (27) wote wakazi wa Arusha pamoja na Mohamed Rashidi (44) mkazi wa Dar es Salaam.
Makasha na vifungashio vyakutwa na alama ya TBS na TRA.
Katika hali isiyo ya kawaida Makasha ya bidhaa hiyo Feki yamekutwa yakiwa na alama ya Ubora itolewayo na shirika la viwango Tanzania,(TBS) huku karatasi zenye Pombe zikiwa zimebandikwa karatasi inayotumiwa na mamlaka ya mapato nchini (TRA).
Kamanda Boaz alisema uwepo wa alama hizo mbili ni kutaka kumuaminisha mnunuzi pamoja na mtumiaji wa bidhaa hiyo kuwa ni halali na imethibitishwa na taasisi hizo mbili muhimu zinazosimamia Ubora wa bidhaa pamoja na mapato.
Alisema uchunguzi wa kina unafanyika ili kubaini watengezaji wa Makasha hayo,pamoja upatikanaji wa alama hizo za TRA huku akiongeza kuwa mbali na kosa hilo la kutengeneza bidhaa bandia pia watu hao wanashiriki katika kuhujumu Uchumi wa nchi.
"Huu ni uhujumu Uchumi kwa sababu wametengeneza bidhaa feki ,halafu wanaziuza madukani bila ya kulipia kodi,wakiwadanganya wauzaji na watumiaji kuwa bidhaa yao imethibitishwa na TBS na wanalipa kodi kwa kuweka alama ya TRA"alisema Boaz.
Kutokana na hali hiyo kamanda Boaz alisema tayari amefanya mawasliano na Uongozi wa shirika la viwango Tanzania (TBS) pamoja na mamlaka ya mapato nchini (TRA) ili kuondoa utata uliopo huku akiongeza umuhimu wa kutolewa kwa elimu ili kuzuia athari za matumizi ya bidhaa zisizokuwa na ubora
0 comments:
Post a Comment