HATI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA ZANZIBAR KUWASILISHWA BUNGENI!!

Mwenyekiti wa Kamati namba sita wa Bunge Maalum la Katiba Stephen Wassira akiwasilisha maoni ya Kamati yake leo mjini Dodoma kwenye kikao cha ishirini na mbili cha Bunge hilo.
Mwenyekiti wa Kamati namba sita wa Bunge Maalum la Katiba Stephen Wassira akiwasilisha maoni ya Kamati yake leo mjini Dodoma kwenye kikao cha ishirini na mbili cha Bunge hilo.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Utaribu, Stephen Wassira amesema Serikali itawasilisha Hati ya Makubaliano ya Muungano katika Bunge Maalumu la Katiba baada ya siku mbili zijazo.

Wassira ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Namba Sita ya Bunge hilo ambazo zilikuwa zikijadili Sura ya Kwanza na ya Sita za Rasimu ya Katiba, alitoa kauli hiyo leo baada ya kuzuka mjadala juu ya uwepo wa hati hiyo na kama ipo kwa nini haijawasilishwa kwa wajumbe wa Bunge hilo.
Mwenyekiti huyo alitoa kauli hiyo, kabla ya kuanza kutoa taarifa za wajumbe walio wengi na wachache juu ya majadiliano ya sura hizo.
“Nataka kuwahakikishia Hati ya Muungano ipo tena ipo katika hali nzuri. Nataka kuhaidi kwamba hati hiyo itafikishwa katika Dola ya Jamhuri ya Muungano siku mbili zijazo,” 
alisema Wassira.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta amesema mjadala wa sura ya Kwanza na ya Sita za Rasimu ya Katiba,utaendelea hata kama bado hati hiyo haijawasilishwa.

Sitta alitoa kauli hiyo baada ya mjumbe mmoja wa Bunge hilo, John Mnyika kuomba mwongozo wa kutaka Bunge hilo, lisiendelee na mjadala wa sura hizo hadi hati hiyo iwasilishwe Bungeni hapo.
“Mwenye mamlaka ya kutaka mjadala uendelee ni Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalum la Katiba, hilo, analolisema Mnyika haliwezekani. Tunaliendesha Bunge hili kwa gharama. Ombi hili litazuiliwa. Hati ya Makubaliano itawasilishwa kwa wakati wake,” 
alisema Sitta huku akisisitiza kuwa hati hiyo haiwazii kuendelea na kazi ya mjadala huo, hata Kanuni za Bunge hilo hazisemi hivyo.

Akiwasilisha maoni ya walio wengi katika kamati yake, Wassira alisema wanapendekeza neno Shirikisho liondolewe kwa sababu Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
”Hati ya Muungano ni sheria ambayo haikuanzisha shirikisho kama wajumbe walio wachache wanavyodai na badala yake ilikusudia kuanzisha Muungano. Hivyo, kutumia neno Shirikisho ni kwenda kinyume na Makubaliano yaliyopo katika Hati ya Muungano,” 
alisema Wassira.

Wassira aliongeza kuwa mapendekezo ya kuanzisha serikali ya shirikisho yanakinzana na masharti yaliyowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katika Sura 83 kifungu cha 9(2) kinachokazia uwepo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
”Ingawa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inadai yalikuwa mawazo ya wananchi; swali ni kwamba kama wananchi walitoa maoni wangetaka kuvunja Muungano. Je Tume ingesemaje?. Shirikisho la serikali tatu litasababisha uendeshaji wa shughuli za umma kuwa na gharama kubwa na hivyo kuwa mzigo wa kiuchumi kwa wananchi,” 
alisema.

Alisema, kwa mfano gharama za sasa za kuendesha taasisi za muungano ni takriban sh. Trilioni 10.7 kwa mujinbu wa makusanyo ya mapato yote ya ndani ni sh. Trilioni 12.6 kwa mujibu wa takwimu za bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012.
“Kuundwa kwa serikali ya muungano kutaongeza gharama na kupanua nakisi ya bajeti,” 
alisema.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa wajumbe walio wengi wa kamati hiyo, wameshangazwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kudai kwamba muundo wa serikali tatu ni maoni ya wananchi walio wengi, wakati hakuna ushahidi wa takwimu.
“Mfumo wa serikali tatu pamoja na kupigiwa debe na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na UKAWA, lakini hakuna ushahidi wa takwimu kuonyesha kuwa unakubalika kwa wananchi walio wengi. Aidha, kwamba unakubalika na pande zote za Muungano,” 
alisema.

Wassira alisema kwa mujibu wa takwimu za Tume, Zanzibar asilimia 61 inasemekana walitaka Muungano wa Mkataba; asilimia 31 walitaka muundo wa serikali mbili.
“Katika hali hiyo kusema serikali tatu ni mawazo ya wananchi walio wengi wa wapi? Kwa Tanzania Bara kati ya watu 16,000 waliochangia Muungano, 8,682 ni kutoka Mkoa wa Kigoma pekee na waliosalia ni kutoka mikoa mikoa mingine iliyobaki.”
“Sasa kwa takwimu hizi unawezaje kusema watu wengi wanataka serikali tatu? Suala la msingi hapa ni kwamba mfumo wa kukusanya maoni uliotumiwa na Tume bila ya kujali ukubwa au udogo wa sampuli, hauna mamlaka ya kubadili mfumo kutoka Muungano kuwa Shirikisho,” 
alisema Wassira. Aliongeza: 
“Hii ni kweli, kwa vile mwaka 1964 Rais Julius Nyerere aliwawakilisha Watanganyika na Rais Abeid Amani Karume aliwawakilisha Wazanzibar wote katika makubaliano ya kuunganisha nchi zetu mbili.”

Wassira alisema kubadilisha hati ya muungano unahitaji kwanza kurudisha Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, kisha kupitia kura ya maoni, uamuzi wa mfumo gani wa Muungano na kama ni shirikisho, basi viongozi wa Tanganyika na Zanzibar wajadiliane aina ya ushirikiano.

Katika Kamati hiyo, Wassira aliwasilisha maoni ya wajumbe wachache ambao walipendekeza Muungano wa Tanganyik na Zanzibar uwe wa Shirikisho.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Kamati Namba Saba ya Bunge hilo, kuhusu Sura ya Kwanza nay a Sita, ya Rasimu ya Katiba, Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngiwilizi aliwasisha maoni ya kamati yake, ambayo pia wajumbe wengi walipendekeza muundo wa Serikali Mbili na maoni ya wajumbe wachache walipendekeza Muundo wa Shirikisho lenye Serikali Tatu.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment