KASHFA NZITO ILALA: MAJALADA YA WAALIMU SHULE 107 YATOWEKA KWAUTATANISHI!!


Chama cha Walimu (CWT)

Hali ya sintofahamu imeikumba Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, baada ya majalada yenye nyaraka na kumbukumbu muhimu za walimu wa shule 107 za halmashauri hiyo kudaiwa kuwa yamepotea.

Upotevu huo unadaiwa kuwa umemlazimisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Raymond Mushi kuahidi kuitisha mkutano wa wadau wiki ijayo ili kujadili suala hilo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) Manispaa ya Ilala, Emanuel Kihako, nyaraka hizo zilipotea wakati wa kuhamisha majalada kwenye ofisi za Idara ya Utumishi wa Walimu zilizokuwa zinahamishwa kutoka maeneo tofauti.

Aliiambia NIPASHE Jumamosi jijini Dar es Salaam katika mahojiano kuwa, awali kumbukumbu hizo pamoja na vitu vingine vilihamishwa kutoka manispaa hiyo kwenda Ubungo Plaza na kisha kurudishwa katika jengo la Anoutoglou la Manispaa hiyo.
"Tuliambiwa taarifa za walimu zimepotea baada ya kuhamahama kwa ofisi za utumishi wa walimu lakini tunashangaa kwani si jambo la kawaida kupotea kwa majalada yote," alisema Kihako.

Alieleza kuwa habari hizo wamezifikisha kwa Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye aliahidi kuitisha mkutano Alhamisi wiki ijayo ukihusisha pande zote zinazovutana ili kupata suluhisho.

Alisema sheria za kazi zimeweka wazi juu ya uondoaji wa kumbukumbu za watumishi na inaelekeza jalada litafungwa baada ya miaka mitatu ya kumaliza ajira na kupelekwa katika idara ya utunzaji wa kumbukumbu kwa ajili ya kuhifadhiwa.

"Walimu hawa hawajamaliza ajira, wanaendelea na kazi sasa pale wanapoambiwa eti majalada yao yamepotea na wapeleke kumbukumbu upya ni kinyume na sheria," aliongeza na kusema mwenyekiti huyo.

Aliliambia gazeti hili kuwa baadhi ya walimu wameitikia wito na kupeleka kumbukumbu zao, kitendo alichokielezea kuwa hakimaanishi kuwa wamekubaliana na serikali bali wamelazimika kufanya hivyo kuhofia ajira zao.

Katibu wa Utumishi wa Walimu Wilaya ya Ilala, Subira Mwakibete, alipoulizwa kuhusu taarifa hizo za CWT alikanusha na kueleza kuwa majalada yote yapo na hatua ya kuchukua kumbukumbu kutoka kwa walimu ni jambo la kawaida kiutumishi.
"Majalada yote tunayo hapa ofisini unaweza kuja kuyaangalia, jambo linalotokea hapa ni kwamba watu wachache kwa sababu binafsi hawataki kupitiwa kumbukumbu zao," alisema.

"Kiutaratibu utumishi wa walimu kila mwaka unapitia upya kumbukumbu za walimu kwa ajili ya kuhakikisha wanapatiwa haki zao ikiwamo kupandishwa madaraja na muda wa kustaafu," alisema.

Mwakibete alieleza kuwa kati ya shule 107 zilizopo Ilala, walimu kutoka shule 103 tayari wametimiza utaratibu wa kuwasilisha kumbukumbu zao na zilizobaki zinaendelea na zoezi hilo.

Alisema kutokana na kuhama kwa ofisi mwaka jana hawakuweza kuendesha zoezi hilo. "Kwa sababu mwaka jana hawakuambiwa, tumewaambia mwaka huu wameona ni kitu cha ajabu, hili ni jambo muhimu sana kwa sababu mtumishi asipopandishwa daraja ni rahisi kumhoji mkurugenzi," alisema Mwakibete.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment