WAJUMBE WA BUNGE MAALUM LA KATIBA WAUMBUANA!!

http://victorndanshau.blogspot.com
Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum, Pandu Ameir Kificho

Bunge Maalum la Katiba jana liligeuka sehemu ya kuumbuana na kupeana mipasho, kufuatia wajumbe wake kutoa siri za yale yanayoendelea ndani ya vikao vya kamati vya majadiliano ya kupitia Rasimu ya Katiba Mpya, ambavyo wanahabari hawaruhusiwi kuhudhuria.

Hali hiyo ilijitokeza jana asubuhi mara baada ya kuwasilishwa kwa jedwali la marekebisho ya Kanuni za Bunge Maaluum za mwaka 2014, na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalum, Pandu Ameir Kificho na baadaye wajumbe kupata muda wa kujadili.

Hata hivyo, wakati wajumbe wakichangia, walitoa siri zilizokuwa zikifanyika kwenye vikao hivyo, hatua iliyosababisha mjadala huo kuingiliwa kati kwa kuomba miongozo na taarifa na kusababisha wajumbe wengine kususa na kutoka ndani ya ukumbi wa bunge.

Siri zilianza kuvuja baada ya mjumbe Moses Machali, kusema azimio hilo linapaswa kupitiwa vizuri na mjumbe apewe haki ya kufanya mabadiliko badala ya kuletwa bila wajumbe kujiandaa.

Kuhusu Kanuni 32d, inayozungumzia amani na utulivu ndani ya bunge, alitaka kiondolewe kifungu hicho na kwamba tayari mapendekezo yaliyoletwa yameanza kuathiri kifungu 56 fasili ya tisa.

“Sipati picha na sioni kwanini Mwenyekiti wa Kamati asishauriane na Mwenyekiti wa Bunge Maalum. Waliopendekeza kifungu hichi waliona kuna sababu. Inawezekana Mwenyekiti asiweze kutenda haki kutokana na mtizamo wake, atakapokwenda kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu ni lazima wataitana na kushauriana kuhakikisha haki inatetendeka.”

Alisema kumpa Mwenyekiti wa Kamati mamlaka, kwa uzoefu wa siku mbili walizokaa kwenye kamati kunaweza kukaleta vurugu na kukosekana kwa amani ndani ya vikao hivyo.

“Tayari wenyeviti wa vikao wameanza kutoa lugha za matusi…Mwenyekiti hawezi kumtukana mjumbe, pamoja kuwa Mwenyekiti huwezi kumtukana mjumbe wa bunge hili, kama anamuona amekosea ana wajibu wa kutumia lugha ya staha, siyo kumtumia Mpambe wa Bunge aje atutoe,” alisema.

Baada ya kauli hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Na.10, Anna Abdallah, alisimama na kumtaka Mjumbe huyo aseme ni kamati gani iliyofanya hivyo, kwa kuwa yeye ni Mwenyekiti wa kamati hiyo ambayo Machali yumo. “Nataka aseme ni kamati gani na siyo kusema kamati nyingine kama ni yangu aseme ili tujirekebishe”.

Machali alisimama kujibu hoja hiyo kwa kusema Anna Abdallah, alipokasimu madaraka kwa Makamu Mwenyekiti, alitoa matusi kwa kuwaita baadhi ya wajumbe kuwa wanatenda matendo ya kihuni na kwamba, kama mwenyekiti alikuwa na haki ya kusikiliza. “Hakuna mamlaka ya mwenyekiti kuzivunja kanuni.”

Dk. Avemaria Semakafu, naye alimama na kusema kuna baadhi ya wajumbe wanatumia kanuni kwa ajili ya kujilinda na uhalifu wanaoufanya, alisema mjumbe aliyetoka kulalamika, wakati wajumbe wengine wakichangia kwenye kamati hiyo, alikuwa akisimama na kuonyesha kwa ishara kuwa wajumbe wengine hawana akili.

“Ninaomba mjumbe awe na nidhamu…Wakati wajumbe wengine wanachangia alikuwa akifanya hivi (akionyesha kwa vitendo) kuwa hatuna akili, ajirekebishe..yeye ndiye alikuwa mhuni,” alisema.

Naye Faida Mohamed Bakar, alisimama na kumuunga mkono Mwenyekiti wake na Dk. Semakafu kwa kusema kuwa Machali ana tabia mbaya anapenda kuropoka kwenye kamati na kuwafokea wenyeviti na wajumbe wanapoongea anawatolea maneno.
Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan, aliingilia kati na kuwataka wajumbe kutumia lugha za staha wanapokuwa ndani ya vikao vya Kamati.

Mjumbe Ezekia Olouch, alipendekeza shughuli za kazi ziishe Ijumaa kwa kuwa watu wazima wanahitaji kupumzika waende kwa saa 40 kama ilivyopendekezwa.

Alisema baadhi ya wajumbe kwenye kamati hawana hoja, hawachangii, hawazungumzi, hawana data badala yake wana vitabu vya Mwalimu Nyerere. Alisema wakipewa nafasi watakwenda kwenye mitandao na kufanya utafiti.

Alisema watu wanatumia mipasho, hawana takwimu, watu wanapashana habari za ugomvi katika nyumba za watu wanazihamishia kwenye kamati. "Watu hawasomi wanabeba mambo ya watu wengine wanayapeleka kwenye kamati."
Mkosamali, aliunga mkono upitishwaji wa kanuni hizo na kuwataka wapinzani wawe wanapinga mambo ya msingi badala ya kupinga vitu vidogo ambavyo havisaidii na kuchelewesha mchakato wa Katiba.

Alisema wanaopinga mapumziko wanapinga kwa hoja gani wakati siku hizo zimetolewa ili wajumbe wapate nafasi ya kufanya utafiti na kujenga hoja kwenye majadiliano yao.

“Wapinzani tupinge hoja mambo ya msingi siyo vitu vya namna hii, siyo unakuwa na wapinzani vigeugeu, mambo madogo madogo huna haja ya kuyapinga,” alisema
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment