MAHAKAMA kuu kanda ya Moshi, imewaachia huru washtakiwa 9 na kuwatia
hatiani wengine 3 wakiwemo Wakenya wawili na Mtanzania mmoja kwa kosa
la kumuua askari Polisi E6829 Michael Milanzi, aliyeuawa katika tukio
la Ujambazi lilitokea Julai 11mwaka 2007 kwenye Benki ya NMB tawi
laMwanga.
Akisoma uamuzi mdogo wa mahakama hiyo, Jaji mfawidhi Kasusulo Sambo alisema kwa mujibu wa sheria wa sheria 293 ya muendelezo wa ushahidi wa makosa ya jinai, kifungu kidogo cha 1, sura ya 20 kamailivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, mahakama imeridhia kuwa Jamhuri ilishindwa kabisa kujenga kesi dhidi ya watuhumiwa 9, Raia wa Tanzania, na hivyo inawaachia huru.
Jaji Sambo alisema katika uamuzi huo Mahakama vilevile ikiongozwa na sheria hiyo kifungu kidogo cha 2, sura ya 20 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002, imeona kwamba upande wa Jamhuri ilifanikiwa kujenga Kesi dhidi ya mshtakiwa namba 1, Samwel Gitau, Mshtakiwa namba mbili Michael Kimani, wote raia wa Kenya na mshtakiwa namba 3, Kalisti Joseph Kanje, Raia wa Tanzania.
"Mahakama ilitafakari ushahidi wote wa Jamhuri, na kufikia maamuzi kwamba mashahidi wote 18 waliofika mbele ya mahakama hii, walionesha ni jinsi gani Jamhuri ilivyoshindwa kujenga kesi dhidi ya washtakiwa namba 4,5,6,7,8,9,10,11, na 12,
"Aidha Mahakama hii tukufu imeridhishwa kwamba Jamhuri kwa kuzingatia sheria ya muendelezo wa makosa ya jinai, kifungu kidogo cha pili, sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ilifanikiwa kujenga kesi kwa kiwango kisicho mashaka dhidi ya washtakiwa namba 1,2 na 3,"alisema Jaji Sambo.
Katika uamuzi huo, Jaji Sambo aliongeza kuwa Mahakama inaamuru washtakiwa wote 4 hadi 12 walionekana kutokuwa na kesi ya kujibu dhidi ya tuhuma hiyo ya mauaji waachiwe huru maramoja isipokuwa kama wana kesi nyingine inayowakabili ambapo mtuhumiwa namba 10, ElizabethMsanze "Bella" ambaye anatuhuma za ujambazi alilazimika kuendelea kutumikia kifungo chake.
Washtakiwa walioachiwa huru ni mshtakiwa namba 4, Deodat Temu, mshtakiwa namba 5, Afande Nathaniel Wanyama, mshtakiwa namba 6, Emmanuel Mziray, mshtakiwa namba 7, Florian Kimati "Babylon", mshtakiwa namba 8 Devotha Msanze.
Wengine ni mshtakiwa namba 9, Juliana Msanze, Mshtakiwa namba 10 Elizabeth Msanze, mshtakiwa namba 11, Ntibasalila Msanze na mshtakiwa namba 12, Salome Materu ambaye alikuwa ni Mhasibu wa Benki hiyo wakati wa uvamizi.
Wakati huo huo upande wa utetezi unaomtetea mshtakiwa namba 3, Kalisti Joseph, unaowakilishwa na wakili wa kujitegemea, Prof. Jonas Itemba, umetoa ombi la kuwasilisha mashahidi wawili mahakamani hapo kwa ajili ya kutoa ushahidi wa utetezi kwa mteja wake.
Mashahidi hao ni Josephine Kalisti, ambaye ni mke wa Mshtakiwa huyo, raia wa Tanzania anayetuhumiwa kushiriki na kufadhili tukio la ujambazi lililopelekea mauaji, na mwengine ni Dafrosa Joseph.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa tena Aprili 10 mwaka huu, baada ya Mahakama kuridhia ombi la Washtakiwa namba 1 na 2 ambao hawana mashahidi, ya kutaka kuruhusiwa kuwasilisha mahakamani, maelezo ya Shahidi namba moja aliyoandika kwa mkono wake ambaye ni meneja wa Benki hiyo wakati huo, Robert Marandu.
0 comments:
Post a Comment