NRA YAWAITA UKAWA WAREJEE BUNGENI!!

Wenyeviti wa Vyama vya Siasa na wajumbe wengine wameombwa kurudi ndani ya Bunge Maalum la Katiba kwa ajili ya kutengeneza katiba ambayo ni muhimu kwa Watanzania.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na mjumbe wa bunge Maalum la Katiba, Rashid Mtuta, alipokuwa akichangia katika Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba.

Mtuta alisema wanasiasa siku zote ni watetezi wa wananchi na itakuwa jambo la ajabu kama hawakufikiria kuwa yametumika mabilioni ya fedha tangu wakati wa kukusanya maoni na hadi sasa wapo bungeni.

“Nawaomba sana wenyeviti wenzangu wa vyama vya siasa na wafuasi wetu, turudi bungeni mabilioni ya fedha yametumika hadi sasa na sisi tukaingia mitini itakuwa ni jambo la ajabu sana…tutawapa Watanzania shida sana,” alisema na kuongeza:

“Tutakuwa kabisa tunawasaliti, nasema yote tunayosema bungeni itakuwa ni sema ya kinafiki au vinginevyo itakuwa kama ni sawasawa na Kaole Sanaa Group itakuwa haina maana yoyote, hapa ndiyo mahala pekee tunapoweza kutengeneza Katiba ambayo wananchi wanahitaka.”

Mjumbe huyo alisema pamoja na bunge hilo maalum kuendelea, lakini hali ya hewa ndani humo haiko sawa kutokana na baadhi ya wajumbe kutoka nje.

“Katika jambo hili hatuhitaji kuwa washabiki hata kidogo, tunahitaji kuwa makini kwa sababu ya mustakabali bora wa Taifa letu,” alisema na kuongeza:

“Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeagizwa Katiba ya Tanzania…Katiba ambayo ilikuwa ni kilio cha muda mrefu sana, na leo tayari tupo ndani ya ukumbi huu, sheria zilizopo zimetuelekeza kwamba majadiliano yote tutayafanya ndani ya ukumbi wa Bunge.”

Alisema akiwa kama mwenyekiti wa NRA pamoja na wanachama wenzake wanaamini kuwa katika mvutano na mgogoro njia pekee ni kukaa mezani na kuzungumza.

“Naomba niwaambie ndugu zangu, kwa vyoyote vile tukiwa kwenye jambo kama hili ni lazima kutakuwa na mvurugano, kwa sababu ya mawazo tu, hivyo basi ni vema sana tukatumia busara kila kundi likaheshimu kundi lingine, na mimi naamini katika makundi yote tunayoyafahamu yapo mawazo mazuri tu yanayotoka kundi namba moja na yapo mawazo mazuri tu yanayotoka kundi namba mbili…kwa hiyo ni muhimu sana makundi haya yote yakawa yanaheshimu kundi lingine ili tuweze kupata mawazo mazuri ili tuweze kupata katiba itakayowafaa Watanzania,” alisema.

Mtuta alisema iwapo wajumbe wote wataamua kugoma na kutoka nje ya mchakato huo watakuwa wamefanya usaliti kwa Watanzania ambao tegemeo lao kubwa ni katiba mpya.

Alisema kwa upande wake alikuwa akiunga mkono mawazo yanayotolewa na Ukawa na si kwa umoja huo tu bali hata kwa kundi lingine lolote linaloonekana lina mawazo mbadala yatakayoboresha katiba ya Watanzania.

Aliongeza kuwa Watanzania wanasubiri Katiba na Katiba hiyo haiwezi kupatikana hadi makundi hayo mawili yawe pamoja na lisipatipake kundi ambalo linaona linaweza kutengeneza katiba hiyo.

Aidha, alisema lugha ambazo zimekuwa zikitumika ndani ya bunge hilo hazifai na ni lugha zenye kuudhi, hivyo alimshauri Mwenyekiti wa bunge hilo, Samuel Sitta, kutumia lugha ya ukali kwa wajumbe.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment