SERIKALI WILAYANI HAI YAWATAKA WANANCHI WA KATA YA KIA KUTULIA WAKATI MGOGORO WA ARDHI UKITATULIWA!!

Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga akizungumza katika mkutano wa kutatua mgogoro wa kata ya KIA uliofanyika eneo la P.6
Mbunge wa Hai,Mhe.Freeman Mbowe akitoa nasaha katika mkutano wa kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na uwanja wa ndege wa KIA
Mmoja kati ya wananchi akitoa maelezo katika mkutano wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe Leonidas Gama akizungumza na wananchi wa jamii ya wafugaji wa Kimasai kuhusiana na mgogoro wao wa mipaka na uwanja wa ndege wa KIA

Mkuu wa wilaya ya Hai Novatus Makunga amewaeleza viongozi wa jamii ya Wamaasai wanaofahamika kama Malaigwanani kutoka vijiji vya kata ya KIA hawakuwa na sababu ya jamii hiyo kuandamana na kufunga barabara inayoelekea katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa kilimanjaro(KIA) wakati serikali imeshafungua meza ya majadiliano ya kupata suluhu ya mgogoro wao na uwanja huo wa ndege.

Makunga ametoa kauli hiyo wakati alipokutana na viongozi hao wa kimila wa jamii wa wafugaji wa Kimaasai kutoka katika vijiji vya Sanya Stesheni,Tindigani na Mtakuja kuzungumia mgogoro wa mipaka kati ya vijiji hivyo na uwanja wa Kia

Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kuwa baadhi ya watu katika jamii hiyo wamekuwa wakipotosha nia njema ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mheshimiwa Leonidas Gama na kamati yake ya ulinzi na usalama ya mkoa ya kumaliza kabisa mgogoro huo uliodumu kwa zaidia ya miaka ishirini.

"Tulikutana kule Moshi mwishoni ni mwezi Februari mwaka huu kwa pamoja na wataalamu kutoka wizara ya ardhi,ofisi ya waziri mkuu,tawala za mikoa na serikali za mitaa,mkoa wa Kilimanjaro na Arusha pamoja na halmashauri ya wilaya ya Hai na madiwani wa maeneo yenye mgogoro  na kupitia ramani na baadaye kupendekeza njia bora ni ya kuweka mapipa kwa muda ili kubaini tatizo kwa pande zote mbili'"alieleza Makunga 

Alifafanua kuwa baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema wamekuwa wakipotosha ushauri na kueleza kuwa serikali imetoa wiki mbili ya kuwataka wananchi hao waondoke kwa hiari yao.

Makunga amesema kuwa mpaka sasa hakuna amri yoyote ya serikali kwa kuwa mchakato wa kutafuta suluhu ya mgogoro huo bado haujakamilika.

Aliwaeleza kuwa pamoja na kutokubaliana na pendekezo hilo la kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wao kama jamii inayohusika na mgogoro huo ilitakiwa nao kutoa mapendekezo yao ya namna bora ya kutatua mgogoro huo badala ya kuanzisha harakati ambazo haziwezi kusaidia kufikia muafaka.

Aidha Makunga aliwaasa viongozi hao wa kimila kuacha mpango wa kuwachangisha wananchi fedha kwa ajili ya kwenda mjini Dodoma kupeleka malalamiko yao kwa Waziri mkuu mheshimiwa Mizengo Pinda,

Makunga amewaeleza kuwa suala hilo lipo katika uwezo wa serikali ya mkoa ambayo imeshaweka mkakati wa kulitatua na kazi hiyo imeaanza kwa kuwa na timu ya kikosi kazi kinachowajumuisha wataalamu wa serikali waliobobea katika mauala ya ramani na ardhi.

Alisema kuwa wilaya iliamua kulishughulikia tatizo hilo Mwezi Oktaba 2012 baada ya yeye kuunda timu ya wataalamu ambayo ilitengeneza taarifa ya kina hata hivyo ilishindwa kuanza mchakato kwa kuwa mgogoro huo pia unavihusisha vijiji vingine viwili vya wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.
Makunga alisema ndipo  baadaye wizra ya uchukuzi mnamo mwezi Machi 2013 iliunda kikosi kazi kilichojumuisha maofisa kutoka wilaya za Hai na Arumeru,halmashauri za Hai na Meru,mikoa ya Arusha na Kilimanjaro pamoja na wataalamu kutoka mamlaka ya viwanja vya ndege,wizara ya ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi pamoja na ofisi ya waziri mkuu,tawala za mikoa na serikali za mitaa.

"Zoezi hilo ni shirikishi ambapo kila hatua ambayo tutaifanya lazima tuwashirikishe wananchi na lengo ni kuhakikisha mwananchi haonewe lakini pia uwanja wa ndege bado unahtajika na ni muhimu kwa uchumi na maendeleo ya taifa letu,"alifafanua.

Akitoa ufafanuazi wa historia ya mgogoro huo,Makunga ameeleza kuwa eneo la KIA lilitengwa na serikali mwaka 1970 kwa ukubwa wa hekta 11,085 sawa na kilometa za mraba 110 na michoro pamoja na uwekaji wa mawe ya mipaka kufanyika mwaka 1989 huku hati miliki kwa Mamlaka ya viwanja vya ndege ikitolewa mwaka 2005.

Alisema kuwa kamati ya ulinzi na usalama iliamua kushughulikia mgogoro huo ambapo ilikutana na wananchi wa vijiji hivyo chini ya mkuu wa mkoa mnamo Februari 13,2014 katika eneo la P.6

Ramani hiyo ya uwanja wa ndege kwa kiasi kikubwa imechukuwa sehemu kubwa maeneo ya vijiji hivyo vyote vinne.

Kwa upande wa vijiji,viliandikishwa wakati huo wa operesheni vijiji vya ujamaa kati ya mwaka 1975 na mwaka 1999 kutegemeana na jinsi vilivyoanza kwani vingine vilizaliwa kutoka katika vitongoji ndani ya vijiji vya awali.

Ramani ya vijiji vyote hivyo ilitolewa mwaka 2006 ambapo nayo ilikuwa na makosa makubwa kwa kuwa ilipita juu ya ramani ya awali ya uwanja wa ndege bila kuonyesha uwanja huo wa ndege

Makunga alieleza kuwa kimsingi tatizo la mgogoro huo wameshalitambu na kwamba kinachotakiwa na kwa wataalamu na pande zenye mgogoro kuanza kupitia na kutoa mapendekezo ya pamoja kwa mamlaka zinazhusika na uwekaji wa mipaka na ramani ambapo jukumu hilo lipo kwa Waziri wa ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wao wa kimila,diwani wa kata ya KIA,mheshimiwa Sinyoki ameahidi ushauri huo kuufikisha kwa wananchi na viongozi wenzao ambao hawakuweza kuhudhuria ili kujadili kwa pamoja na kutengeneza mapendekezo.
Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro(KIA) unamilikiwa kwa asilimia mia moja na serikali huku ukiendeshwa na kampuni ya serikali ya KADCO ambayo miaka ya nyuma iliuza hisa kwa makampuni matatu ya kigeni kabla ya serikali mwaka 2010 kuamua kuzinunua hisa zote
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment