Wakazi wa mtaa wa Eastleigh ambako watu sita waliuawa katika shambulizi la kigaidi siku ya Jumatatu, wanalalamika kuwa polisi wanatumia nguvu kuwahangaisha huku wakiendelea kufanya msako wa kudhibiti usalama katika mtaa huo.
Wakazi wengi ambao ni wasomali wanasema kuwa polisi wanawachapa na kuwakamata kiholela huku operesheni hiyo ya usalama ikeindelea kwa siku ya tatu.
Baadhi waliohojiwa wanasema kuwa wanalazimika kuwahonga polisi kwa sababu hawana hatia na hawataki kukamatwa.
Polisi wamewakamata watu 1,000 mtaani Eastleigh na viunga vyake katika msako huo.
Kwa mujibu wa waziri wa usalama Joseph Ole Lenku operesheni hiyo itaendelea hadi pale washukiwa wa ugaidi na wale ambao wanaeneza itikadi kali za dini ya kiisilamu watakapokamatwa.
Mnamo siku ya Jumatatu, magaidi walishambulia mkahawa mmoja mtaani Easteligh na kuwaua watu 6 huku wengine 30 wakijeruhiwa.
Siku iliyofuata muhubiri tatanishi muisilamu, Sheikh Makababri akapigwa risasi na kuuawa nje ya mahakama ya Shanzu mjini Mombasa.
Kenya imekuwa ikikumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara tangu wanajeshi wake kuingia nchini Somalia kwa vita dhidi ya wanamgambo wa kisomali wa Al Shabaab.
Wapiganaji hao wameahidi kufanya mashambulizi Kenya hadi wanajeshi hao watakapoondoka Somalia.
Lakini serikali ya Kenya imesema kuwa kamwe haitaondoa wanajeshi wake Somalia kwani kwa sasa ijulikane kwamba wako vitani na kundi hilo la kigaidi.
0 comments:
Post a Comment