Mgogoro wa uongozi umezuka
katika Bunge la Afrika Mashariki ambapo wabunge wa bunge hilo
wanakusudia kumwondoa madarakani spika wa bunge hilo.
Tayari wabunge hao wameshakusanya saini 36 kutoka kwa wabunge 45 wa bunge hilo ambazo zinatakiwa kwa mujibu wa kanuni.Akiongea na waandishi wa habari kiongozi wa wabunge hao kwa niaba ya wabunge wenzake wa bunge hilo Abudulla Ali Hassani Mwinyi, amesema wabunge hao wamefikia hatua hiyo ya kumwondoa spika huyo Margareth Zziwa kufuatia kukerwa na mwenendo wake.
Tayari wabunge hao wameshapeleka hoja ya kumwondoa spika huyo kwa Katibu wa Bunge hilo ikiwa na sahihi za wabunge 36 ili kutimiza matakwa ya utaratibu unaotakiwa kwa mujibu wa kanuni za bunge hilo ili kuanzisha hoja ya kumwondoa spika.
Je wabunge hao hawakuwa na njia nyingine kumaliza mgogoro huo hadi kufikia hatua ya kutaka kumwondoa spika huyo.
Mgogoro huu wa uongozi ndani ya bunge hilo umesababisha kuahirishwa kwa bunge hilo tangu jana kwa muda usiojulikana baada ya spika huyo kuamua kuliahirisha kwa muda usiojulikana.
Hii inafuatia malumbano yalijitokeza ndani bunge hilo ambapo mmoja wabunge alisema hoja hiyo isingeweza kujadiliwa.
BBC ilifanya juhudi za kuwasiliana na spika huyo Margareth Zziwa kwa simu yake ya mkononi ili kujibu tuhuma hizo hata hivyo alikataa kusema chochote ambapo alishauri apigiwe afisa habari wa bunge hilo ili atoe ufafanuzi.
Mgogoro huu wa uongozi ndani ya bunge hilo bado haijajulikana utamalizika lini lakini kwa vyovyote vile utakuwa umeathiri shughuli za Bunge hilo la Afrika Mashariki.
CHANZO:BBC
0 comments:
Post a Comment