Jaji Joseph Warioba (wa pili kutoka kulia). |
Ikulu imesisitiza kuwa haikuwa na madaraka wala mamlaka, kuibadilisha.
Aidha, Ikulu imeanika viwango vya posho, ambavyo wajumbe wa tume hiyo, walikuwa wakilipwa vya kati ya Sh 100,000 na Sh 500,000 kwa siku.
Imesema wanaodhani Serikali ina uwezo wa kulipa kila mjumbe kiinua mgongo cha Sh. milioni 200, wanajidanganya.
Hayo yamo kwenye Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana Dar es Salaam.
Ilikuwa ikifafanua madai mbalimbali, yaliyotolewa na magazeti mawili tofauti ya jana; moja likimnukuu Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba akidai Ikulu imewatupia virago.
Gazeti lingine lilikuwa na habari chini ya kichwa : 'Bilioni 6 kuipoza Tume ya Warioba' , ikimkariri mjumbe mmoja wa Tume hiyo, ambaye hakutajwa jina. Mjumbe huyo alidai tume hiyo inatarajia kupewa Sh bilioni sita, ikiwa ni kiinua mgongo, ambapo kila mjumbe atapata Sh. milioni 200.
Katika taarifa hiyo, Ikulu ilisema tangu mwanzo wa mchakato mzima wa Katiba Mpya na utendaji kazi wa Tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, hapakupata kuwepo shaka kuhusu siku ya tume kumaliza kazi zake.
"Mwenyekiti wa Tume, wajumbe wote wa Tume, Sekretarieti ya Tume na Watanzania wote waliijua fika siku ya mwisho ya tume kukamilisha shughuli zake. Kwa mtu kujitia ameisahau siku hiyo leo ni kiwango cha juu sana cha unafiki," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ya ikulu, inatokana na habari iliyochapishwa jana kwenye gazeti la Raia Mwema, ikimnukuu Jaji Warioba akidai kuwa tume ilifukuzwa kazi kwa maana kwamba haikupewa muda wa kuandaa na kuwasilisha nyaraka.
Habari hiyo, ilimnukuu Jaji Warioba akidai kwamba wajumbe wa Tume hiyo, waliporwa magari ambayo yamewekwa Ikulu.
Pia, habari hiyo ilidai Tume hiyo inatarajiwa kupewa Sh.bilioni sita ikiwa ni kiinua mgongo ambacho kila mjumbe atapata kiasi cha Sh. milioni 200.
Katika ufafanuzi huo, Ikulu ilieleza kuwa moja ya mijadala mikali ya awali kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, ulihusu lini Tume ya Mabadiliko ya Katiba imalize muda wake.
"Wengine wakitaka Tume imalize muda wake baada ya kukabidhi ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba, wengine wakitaka Tume imalize muda wake baada ya Mwenyekiti wake kuwasilisha Rasimu yake Bungeni na hata wengine wakitaka wajumbe wa Tume wawe sehemu ya Bunge Maalum la Katiba."
Hatimaye, ilikubaliwa shughuli za tume zingefikia ukomo wake baada ya Mwenyekiti wake kuwasilisha Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Baada ya Jaji Warioba kuwasilisha rasimu katika Bunge Maalum la Katiba, Machi 18, mwaka huu, siku iliyofuata kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Rais alitia saini tangazo la Serikali la kuvunja tume hiyo lilichapishwa kwenye gazeti la Serikali, Machi 21.
"Siku hiyo ya mwisho iliwekwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, na Ikulu haikuwa na madaraka wala mamlaka yoyote kubadilisha tarehe hiyo. Hivyo, madai ya Ikulu kuitupia virago Tume ya Mabadiliko ya Katiba hayana msingi wowote na ni jambo la kutunga tu," ilisema taarifa.
Ilifafanuliwa kuwa tangu Jaji Warioba alipokabidhi Ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba kwa Rais, Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Desemba 30, 2014, jijini Dar es Salaam, Sekretarieti ya Tume ilitakiwa kuandaa ripoti ya makabidhiano.
"Kwa maana hiyo, tokea Desemba 30, mwaka jana, kupitia miezi ya Januari, Februari mpaka Machi 18, mwaka huu, Sekretariati ilikuwa na muda wa siku 77, zaidi ya miezi unusu, Ékatika muda wote huo, ilikuwa inafanya nini badala ya kuandaa ripoti ya makabidhiano na wakati maofisa wake walikuwa wanaendelea kulipwa mshahara na Serikali? Kwa nini walalamike hadharani leo kwa jambo ambalo lilikuwa ni la wajibu wao na wakashindwa kulifanya kwa wakati?," imehoji.
Ikulu ilikiri wajumbe wa Tume, walitakiwa kurudisha Ikulu magari, ambayo walikuwa wanatumia kikazi, kwa sababu kazi ya Tume ilikuwa imemalizika ;na kwamba ilifahamu yalitakiwa kupelekwa Dodoma kwa matumizi ya shughuli za Bunge Maalumu la Katiba.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali ilichukua uamuzi magari hayo yapelekwe Dodoma, kwa sababu lisingekuwa jambo la busara kwa Serikali kutumia fedha za umma, kununua magari mengine mapya wakati ya Tume bado yanafaa, kufanya kazi na wala hakuna bajeti ya kufanya manunuzi ya magari mapya.
Ilikiri, "ni kweli magari hayo yako Ikulu, Dar es Salaam, yakisubiri kukamilika kwa taratibu za kuyapeleka Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma."
Suala lingine ambalo linadaiwa kupotoshwa ni kuhusu taarifa kwamba wajumbe wa tume hiyo, walilipwa kiinua mgongo cha Sh milioni 200 kila mmoja.
Ikulu ilikiri wajumbe wa tume hiyo, kufanya kazi nzuri na kueleza kuwa wanastahili pongezi nyingi za wananchi.
Lakini, ilisema kama wanadhani Serikali ina uwezo wa kumlipa kila mjumbe kiinua mgongo cha Sh. milioni 200, wanajidanganya.
Imefafanuliwa kwamba alichozungumza Rais Kikwete tangu mwanzo wa mchakato ni kwamba, atafikiria kuwalipa wajumbe wa tume aina fulani ya kifuta jasho, ambacho kiwango chake atakiamua yeye na kwa wakati mwafaka kulingana na raslimali za Serikali. "Mpaka sasa hajafanya uamuzi juu ya jambo hili," ilieleza taarifa hiyo ya Ikulu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ukweli ni kwamba wajumbe wa Tume walikuwa wanalipwa Sh. 200,000 kama posho ya vikao kwa siku. Taarifa hiyo ilikanusha kwamba wajumbe hao wa tume walikuwa wakilipwa Sh 500,000 kwa siku.
0 comments:
Post a Comment