TENDWA AMLAUMU KIKWETE KUACHA MSIMAMO WAKE!!
Aliyekuwa msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa amesema Rais Jakaya Kikwete aliteleza kueleza msimamo wake na ambao baadaye ulibainika kuwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba, Machi 21.
Tendwa, ambaye alistaafu Agosti mwaka jana na nafasi yake kuchukuliwa na Jaji Francis Mutungi, alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Tendwa, ambaye alikuwa Msajili kwa miaka 13, alisema akiwa kiongozi mkuu, Rais Kikwete alipaswa kutoa mwongozo wa uendeshaji wa Bunge Maalum la Katiba.
“Sikuwapo nchini, lakini kwa kadri ninavyoelezwa, kama hiyo ni kauli yake, basi alijisahau kusemea msimamo wa chama chake, (CCM) na sera yake ya serikali mbili katika bunge hilo,” alisema.
“Rais ni mtendaji, alipaswa kutoa guidelines (miongozo) ya jinsi ambavyo Bunge Maalum la Katiba linatakiwa kufanya. Alichokisema, aliteleza.
“Alijisahau na kurudi kwenye chama kwa sababu hiyo ndiyo sera ya chama chake, ” alisema Tendwa.
“Na siyo yeye tu (Kikwete) kwani nimemsikia hata Dk Shein (Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi), akisema kuwa msimamo wa CCM ni serikali mbili,” aliongeza Tendwa.
“Nimemsikia Makamu wa Pili wa Rais (Balozi Seif Ali Iddi) akisema hivyo na Rais wangu (Kikwete) katika mikutano mbalimbali ya hadhara, naye amelisema hilo.”
Tendwa ambaye katika uongozi wake wa miaka 13 alikuwa akituhumiwa mara kwa mara na vyama vya upinzani kuwa anakibeba chama tawala, alisema: “Nadhani na yeye (Rais Kikwete) kasema. Nadhani alijisahau kuwa ni kiongozi wa taifa.”
“Rais ni mtendaji na mimi nasema aliteleza. Turudi katika hoja kwa kujadili rasimu iliyoko mezani.”
Kauli hiyo imekuja kipindi ambacho baadhi ya viongozi wakiwa
mo wa vyama vya siasa nchini, Dk Wilbroad Slaa (Chadema), Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad na pia aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, pia kumkosoa Rais Kikwete.
Kwa nyakati tofauti, wameeleza kuwa Kikwete ndiye mtu pekee anayeweza kutuliza mvutano ulioibuka katika mchakato huo unaoendelea kwenye Bunge la Katiba.
Machi 21, wakati akifungua Bunge Maalum la Katiba, Rais Kikwete aliipinga Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba, akigusia mambo saba ya msingi yaliyomo katika rasimu hiyo na kutaka yatazamwe kwa kina, kubainisha kuwa mengine hayawezi kutekelezeka.
Miongoni mwa mambo hayo ni muundo wa Muungano kuwa wa serikali tatu uliopendekezwa katika rasimu hiyo.
Kikwete, ambaye alisema anatoa maoni yake binafsi, alipinga waziwazi pendekezo la serikali tatu na kuegemea katika muundo wa serikali mbili unaoungwa mkono na CCM, huku akifafanua kuwa idadi ya watu waliopendekeza muundo wa serikali tatu ilikuwa ndogo.
Julai 7, wakati akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na televisheni ya ITV, Maalim Seif alimtupia lawama Rais Kikwete kuwa amechangia kuukoroga mchakato wa katiba kwa kufuata msimamo wa chama chake, badala ya maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu ya pili ya katiba.
Maalim Seif, ambaye alilenga kauli iliyotolewa na kiongozi huyo wa nchi wakati akifungua Bunge la Katiba, alisema kauli ya Rais Kikwete imeondoa imani ya wananchi kuhusu kupatikana kwa katiba inayotokana na maoni yao.
Alisema mchakato huo hivi sasa unamtegemea Rais pekee, huku akisisitiza kuwa hakuna binadamu aliyekamilika na kumshauri kutafuta uwezekano wa kuweka mambo sawa, ili kujenga tena imani kwa wadau wote.
Julai 4, Dk Slaa, wakati akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jijini Dar es Salaam, alimtaka Rais Kikwete kujitokeza hadharani kutafuta suluhu ya kupata mwafaka wa mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa hakuna mamlaka nyingine zaidi inayoweza kuunusuru.
Naye Jaji Warioba kwa nyakati tofauti amemshauri Rais Kikwete kuchukua hatua zitakazoondoa matatizo katika Bunge la Katiba ili kuwezesha mchakato huo kukamilika.
Alisema ni muhimu kiongozi huyo mkuu wa nchi kuweka kando tofauti za mawazo na mitazamo ili kupata Katiba Mpya kwa masilahi ya Taifa.
0 comments:
Post a Comment