KATIBU wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, amewataka wananchi wasikubali kuandamana
kwa shinikizo la viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), ili kushinikiza Bunge Maalumu la Katiba lisitishe vikao vyake
kabla ya Oktoba 4,2014.
Bw. Nnauye aliyasema
hayo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Kisarawe,
mkoani Pwani na kusisitiza kuwa, maandamano hayo aachiwe Mwenyekiti wa
CHADEMA Taifa, Bw. Freeman Mbowe, familia yake na viongozi wengine.
Alisema chama hicho
kina utamaduni wa kutumia damu za Watanzania kama mtaji wake kisiasa
kwani vyombo vya dola vinapochukua hatua ya kuzuia maandamano,
wanaoathirika si viongozi wa chama hicho au familia zao ndio maana
wanaona fahari watu wanapokufa.
"Upinzani katika nchi
hii umegeuka kuwa laana, kazi kubwa ambayo wanaifanya ni kuchonganisha
watu na Watanzania ni mashahidi, maeneo ambayo CHADEMA wamefanya
maandamano, watu maskini wamepoteza maisha.
"Viongozi wa CHADEMA
wanabaki salama na familia zao hivyo kama Mbowe anataka kufanya
maandamano nchi nzima kushinikiza Bunge la Katiba lisitishwe, aanze
kutangulia yeye, mkewe na watoto zake, Watanzania wamechoka kushuhudia
damu za watu maskini zikimwagika," alisema Nape.
Aliwataka wananchi
kufahamu kuwa, Katiba haimpeleki mwanasiasa au mtu yoyote Ikulu badala
yake kura ndizo zinazoweza kumpeleka Ikulu ambapo CHADEMA, Chama cha
Wananchi (CUF) pamoja na NCCR-Mageuzi, wanaamini Katiba ikipatikana ndio
inayoweza kuwapa ushindi katika Uchaguzi Mkuu 2015.
"Vyama hivi vinataka
kuligawa Taifa kwa kutumia mchakato wa Katiba, umefika wakati wa
Watanzania kuachana na upinzani wenye kujenga chuki...CCM na viongozi
wake wamekuwa wakihubiri amani, mshikamano na umoja lakini wapinzani
wanatumia muda mwingi kuhubiri chuki," alisema.
Katika hatua nyingine,
Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Abdulrahman Kinana, amepongeza juhudi za
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma
Kikwete, kwa juhudi zake za kuwasaidia wanawake na watoto wa kike
kupitia taasisi hiyo.
Bw. Kinana alitoa
pongezi hizo juzi baada ya kutembelea Shule ya Wanawake ya Wama
Nakayama, inayomilikiwa na taasisi hiyo iliyopo kwenye Kijiji cha
Nyamisati, Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani.
Alis ema Mama Kikwete
amekuwa na mchango mkubwa nchini kutokana na jitihada zake za kusaidia
makundi mbalimbali wakiwemo watoto yatima na waishio katika mazingira
magumu.
Aliwataka wanafunzi
shuleni hapo, kusoma kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za Mama Kikwete
kwani wao ndio viongozi wa baadaye ambao watashika nafasi mbalimbali za
uongozi.
Kwa upande wake,
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Suma Mensah, alisema shule hiyo imekuwa
msaada mkubwa kwa wakazi wa Rufiji na nje ya Wilaya hiyo kwani inatoa
elimu kwa wanafunzi wasio na uwezo pamoja na yatima.
"Juhudi za Mama Kikwete
kwa watoto wa kike zimefanikiwa kwani watoto waliokuwa hawana mwelekeo
wa maisha, hivi sasa wanafurahia kupata elimu bora," alisema Mensah.
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
0 comments:
Post a Comment