Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Rene Meza, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, kuhusu mwenendo wa kibiashara wa kampuni hiyo. |
Kampuni nyingine kubwa ya mawasiliano, Tigo
imeahidi kutoa ufafanuzi wa suala hilo kesho wakati Airtel imesema
haijafanya mabadiliko yoyote kwenye gharama za vifurushi vyake.
Kumekuwapo na mijadala mingi katika mitandao ya
kijamii kupinga bei mpya za vifurushi hivyo ambazo zimeelezwa kuwa ni
megabati nane kwa vifurushi vyote vya saa 24, na megabati 60 kwa
vifurushi vya wiki.
Bei hizo zinaelezwa kuwa zimeanza kutumika kwa
wateja wanaotumia mitandao ya kampuni za Vodacom na Tigo, ambazo
zinachuana vikali sokoni, huku baadhi ya wateja wa kampuni ambazo
hazifanya mabadiliko ya gharama hizo wakiwashiwishi wenzao kuhama ili
kutokuwa hewani kutokana na kukosa vifurushi.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma
alisema kuwa tayari mazungumzo kati ya mamlaka yake na kampuni hizo za
mawasiliano yameshafanyika na kilichobaki ni wao kutoa maelezo ya hatua
walizoichukua.
“Matumizi ya intaneti yameongezeka nchini na
wananchi wengi wamekuwa hawajui namna ya kutofautisha vifurushi vya muda
wa maongezi na vile vya intaneti. Lakini nimezungumza na kampuni zote
na tumefikia mwafaka. Ndani ya wiki hii watatoa tamko lao pamoja na
msimamo wa bei za vifurushi,” alisema Profesa Nkoma.
Machi, 2013, Profesa Nkoma alisema angehakikisha
kampuni za simu zinawasilisha kwake makubaliano kuhusu punguzo la
gharama za kupiga simu kwa mwingiliano wa mawasiliano, kutoka wateja wa
kampuni moja kwenda nyingine.
Mabadiliko ya gharama na ukubwa wa vifurushi
yalianza kujitokeza mwishoni mwa wiki iliyopita, hali iliyoibua mijadala
mingi katika mitandao ya kijamii. Kilichojitokeza ni kwamba makampuni
hayo yamepunguza ukubwa wa vifurushi vya intaneti na kutoathiri vile vya
muda wa maongezi na ujumbe mfupi hali, iliyozusha hamaki kwa wateja
wengi wanaotaka kujua sababu za mabadiliko hayo.
Baada ya mijadala hiyo kuongezeka, Naibu Waziri wa
Sayansi na Teknolojia, January Makamba aliwaondoa wasiwasi wateja baada
ya kuandika katika ukurasa wake wa facebook kuwa serikali imechukua
hatua mara moja.
“Nimeongea na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa
John Nkoma na nimemuagiza azungumze na kampuni za simu juu ya mabadiliko
ya bei za bundles (vifurushi): ukubwa, ughafla na upamoja (mitandao
yote). Nimewaagiza pia watoe majibu kwa umma haraka iwezekanavyo.
Kampuni za simu hazipaswi kupanga au kuratibu kwa pamoja bei; tukigundua
hilo limetokea ni ukiukwaji wa kanuni za ushindani wa soko,” inasema
sehemu ya ujumbe huo.
Katika ujumbe wake, Makamba anafafanua kuwa Sheria
ya udhibiti wa mawasiliano haiipi serikali nguvu ya kupanga bei,
isipokuwa gharama za muingiliano
“Inawezekana gharama za uendeshaji, ikiwamo umeme,
zinapanda, lakini hakuna kodi mpya ya Serikali tangu baada ya bajeti.
Huko nyuma ushindani ulishusha bei kwa sababu hakukuwa na bei elekezi. Bado niko nje ya nchi kwa safari ya kiserikali, lakini nimekuwa nalifuatilia suala hili kwa karibu. Pia nimeongea na Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Rene Meza, kuhusu suala hili leo asubuhi,” aliandika Makamba.
Huko nyuma ushindani ulishusha bei kwa sababu hakukuwa na bei elekezi. Bado niko nje ya nchi kwa safari ya kiserikali, lakini nimekuwa nalifuatilia suala hili kwa karibu. Pia nimeongea na Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom, Rene Meza, kuhusu suala hili leo asubuhi,” aliandika Makamba.
Mkurugenzi huyo wa Vodacom alisema ongezeko la bei za kupiga
simu na kupungua kwa ukubwa wa vifurushi limesababishwa na ongezeko la
kodi hivyo mabadiliko hayo yamefanywa kama hatua ya kubadili mazingira
ya kibiashara ili kuepuka hasara.
“Tunafanya hivi ili tusipate hasara na tuendelee
kuwekeza, kodi ni kubwa na lazima tufanye kila tuwezalo ili na sisi
tuendelee kufanya kazi kwa faida,” alisema Meza.
Meza alisema hata hivyo kampuni ya Vodacom
imepunguza viwango vya malipo vya upigaji simu ambapo mwaka 2013 dakika 1
ilitozwa Sh58 wakati hivi sasa dakika 1 inatozwa Sh24. Akaongeza kuwa
bei hizo zimeshuka hata kwa vifurushi na kutoa mfano kuwa mwaka 2013
mteja alitozwa Sh9 kwa MB 1 na mwaka huu mteja anatozwa Sh5 kwa MB 1.
“Hili punguzo la bei ni kubwa na linatuumiza kwa
sababu kodi zinakwenda juu, sisi tukishusha gharama lakini kodi
zinaendelea kupanda. Kwa mfano mwaka 2012 kodi ilikuwa asilimia 5 na
mwaka huu kodi imepanda hadi kufikia asilimia 79,” alisema.
Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Airtel, Jackson
Mbando alisema kampuni yake haijabadili chochote katika muda wa maongezi
wala katika vifurushi vya intaneti badala yake alisema Airtel imekuwa
ikitoza gharama nafuu kuliko mitandao yote.
“Sisi tunatoa kila kitu kwa bei nafuu, kama kuna
kampuni zinazoongeza gharama, hao waulizwe. Hapa kila kitu unapata
zaidi,” alisema.
Hata hivyo, Mbando alisema hata kama kuna
ongezeko, kampuni yake inatoza gharama nafuu za vifurushi vya intaneti
kuliko kampuni nyingine za simu nchini.
Meneja Mawasiliano wa Tigo, John Wanyancha alisema amepata malalamiko hayo na kuahidi kuyatolea ufafanuzi mapema.
Wateja wengi wa kampuni hizo walilalamika kuwa
wakiweka fedha kwenye akaunti zao wakati mwingine salio huisha hata
kabla ya kupiga simu au kujiunga na kifurushi.
Mmoja wa wateja wa kampuni hizo alilalamika kwenye
mtandao wa kijamii kuwa gharama hizo zimepanda kwa kuwa wananchi hawana
pa kukimbilia.
“Sasa hivi mwisho kutuma video za kilobaiti mbili
ili kuepuka kuwa nje ya mtandao baada ya kumaliza vifurushi vyetu.
Wanajua hatuna pa kukimbilia ndiyo maana wameamua kutufanyia hivi,”
aliandika mteja huyo katika akaunti yake ya WhatsApp.
Wengi wanalalamika kuwa vifurushi hivyo havikidhi
mahitaji wala kuendana na thamani ya fedha wanazotumia. Mabadiliko haya
yanakuja ikiwa ni baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji
(Ewura) kushusha gharama za umeme kwa shilingi nane kwa kila uniti moja
agizo linaloanza kutekelezwa kuanzia jana.
Wateja wengi wa Kampuni ya Tigo walilalamika kuwa wakijiunga na kifurushi cha muda wa maongezi, kwa mfano cha Minikabang cha Sh649 wanapata dakika 11 wakati zamani walipata dakika 14.
Wateja wengi wa Kampuni ya Tigo walilalamika kuwa wakijiunga na kifurushi cha muda wa maongezi, kwa mfano cha Minikabang cha Sh649 wanapata dakika 11 wakati zamani walipata dakika 14.
“Nashangaa siku hizi nakatwa Sh649, napata dakika
11 tu, halafu sielewi zinaishaje ishaje yaani nikipigia watu wawili,
watatu, kifurushi kimeisha,” alisema, Pendo Malya, mkazi wa Tabata.
Kadhalika wateja wa mitandao ya Airtel na Vodacom
nao walilalamika kukatwa fedha nyingi katika muda wa maongezi licha ya
kampuni hizo kutangaza kuwa zimepunguza gharama.
Abdul Mfinanga, mkazi wa Msasani alisema anakatwa fedha nyingi hata wakati wa kufanya miamala katika huduma ya MPESA.
Asilimia kubwa ya wateja wa simu za mitandao yote walikiri kupaa kwa gharama za kupiga simu bila ya kujiunga na vifurushi.
Kwa mfano, Anuciata Mwigalula, wa Kibamba alisema
akijiunga na muda wa maongezi anapata unafuu kidogo lakini akiweka Sh500
bila kujiunga, basi hawezi kuzungumza hata kwa dakika tatu hata akipiga
kwenda mtandao ule ule.
“Wanatuibia sana, wakati mwingine unapewa ofa ya
kuanzia saa sita usiku, sasa ukeshe ndiyo unufaike na huduma hizo?”
alihoji Mwigalula.
Hata hivyo, Novemba mwaka jana, Makamba alikiri
mbele ya Bunge kuwa kuna tatizo katika kampuni za simu nchini la
kuwaibia wateja wao.
0 comments:
Post a Comment