RAIS WA BURUNDI KUWANIA TENA NAFASI HIYO KWAMUHULA WA TATU!!

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.
Msemaji wa Rais Piere Nkurunziza wa Burundi amesema kwamba kiongozi huyo atawania muhula wa tatu madarakani katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi wa Juni na kuahidi wanaharakati wanaosema kwamba hatua hiyo itakiuka katiba na kuhatarisha nchi hiyo kutumbukia kwenye ghasia.

Msemaji wake huyo Willy Nyamitwe amekaririwa akisema Nkurunzinza atagombea urais iwapo atachaguliwa kukiwakilisha chama chake cha CNDD-FDD katika kinyang'anyiro hicho "kwa kuzingatia katiba."

Tangazo hilo linakuja kufuatia kuzinduliwa kwa kampeni mapema mwezi huu na mashirika ya kijamii zaidi ya 300 nchini humo yakitowa wito kwa Nkuruzinza asigombee muhula huo wa tatu ili kuzuwiya kuzuka kwa ghasia nchini humo.

Kundi la mashirika hayo limemtaka rais huyo "kujifunza" kutokana na yale yaliyotokea nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambapo kulizuka maandamano ya maafa hapo mwezi wa Januari yaliosababishwa na hofu ya upinzani kwamba Rais Joseph Kabila alikuwa akijaribu kurefusha muda wake madarakani.

Lakini Nyamitwe ameonya kwamba mtu yoyote yule anayejaribu kuchochea maandamano atakabiliwa na mkono wa sheria.Amesema "yoyote yule anayetowa wito kwa wananchi kuandamana mitaani ......atahesabika kuwa mfanya fujo na atashughulikiwa vilivyo." Ameongeza kusema wananchi wa Burundi wanahitaji amani na haitokaa kimya pembeni katika kadhia kama hiyo.

Makundi ya haki za binaadamu yameonya juu ya kuongezeka kwa hofu kuhusiana na hatari ya kuzuka kwa ghasia kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo uliopangwa mwezi wa Juni wakati kukiwa na mfululizo wa mashambulizi ikiwa pamoja na mapigano ya siku tano mwezi uliopita kati ya jeshi la waasi.

Wanasiasa wa upinzani na wahakiki wanasema serikali inafanya kila iwezalo kuzima changamoto za kisiasa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo kwa kuwatia watu mbaroni,unyanyasaji na kukandamiza uhuru wa kutowa maoni.

Nkuruzinza alikuwa ameonyesha wazi kwamba alikuwa na nia ya kutumikia muhula wa tatu wa urais.
Katiba ya Burundi inaruhusu tu rais wa nchi hiyo kuchaguliwa mara mbili kwa kipindi cha jumla cha miaka 10 madarakani lakini hoja anayoitumia Nkunrunzinza ni kwamba alikuwa amechaguliwa moja kwa moja na wananchi mara moja tu.

Katika muhula wake wa kwanza katika wadhifa huo wa urais mwanzoni mwaka mwaka 2005 alikuwa amechaguliwa na bunge la nchi hiyo.
Ni mwezi uliopita tu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon alitowa wito kwa viongozi wa Kiafrika wasi'ngan'ganie madaraka na waheshimu matakwa ya wananchi wao.


Akizungumza katika Mkutano wa Kilele wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika makao makuu ya umoja huo mjini Addis Ababa Ethiopia BanKi-moon  amesema watu duniani kote wanaelezea wasi wasi wao kuhusu viongozi wanaogoma kun'gatuka baada ya kumaliza muda wao madarakani.
Amewataka viongozi wote barani Afrika na duniani kwa jumla kuwasikiliza wananchi wao na kusema kwamba "viongozi wa kisasa hawastahiki kupuuza matakwa na matarajio ya wananchi wao."

Hapo mwezi wa Oktoba ghasia zilizuka nchini Ivory Coast wakati wabunge walipokuwa wakijiandaa kupiga kura ya kumruhusu kiongozi wa nchi hiyo Blaise Compaore mwenye umri wa miaka 63 ambaye alichukuwa madaraka hapo mwaka 1987 katika mapinduzi kugombania uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mwezi wa Novemba 2015.Maandamano ya umma yalimlazimisha kujiuzulu.

Mapema mwezi huu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo takriban watu 42 waliuwawa katika maandamano ya kupinga kile kilichokuwa kikionekana kama jaribio la Rais Joseph Kabila kuendelea kun'gan'ania madaraka katika taifa ambalo ameliongoza kwa miaka 14.
Nchi zikiwemo Benin,Congo- Brazaville na Rwanda zote zinasemekana kufanya mabadiliko ya katiba kuwawezesha viongozi wake wawanie muhula wa tatu madarakani.

Mataifa mengine ya Afrika ambapo sheria zimebadilishwa ili kuwanufaisha viongozi waliokuwa madarakani ni pamoja na Algeria,Angola, Chad,Djibouti na Uganda.
Burundi ni nchi ndogo isiokuwa na bahari ilioko Afrika ya Kati kwenye eneo la Nchi za Maziwa Makuu.

Hali ya kisiasa inaendelea kuwa ya mvutano kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo wa bunge na urais hapo mwezi wa Mei na Juni.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment