Vigogo
ambao tathmini ya mwenendo wao inasubiriwa baada ya kikao hicho ni
pamoja na waliokuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine
ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba
ambaye ameshatangaza nia ya kugombea urais, Waziri wa Kilimo na
Ushirika, Stephen Wassira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Mwanzoni
mwa wiki hii, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alitoa
taarifa kwa vyombo vya habari, ikielezea kuwepo kwa kikao cha Kamati Kuu
leo kitakachoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Ingawa
ajenda za kikao hicho hazikuwekwa wazi, lakini tayari duru za siasa na
wachambuzi mbalimbali, walishaanza kuzungumzia umuhimu wa ajenda ya
tathmini ya hukumu ya makada hao, kwa kuwa muda wa kutumikia adhabu hiyo
ya mwaka mzima ulikamilika katikati ya mwezi huu.
Vigogo
hao wanaotajwa kutaka kuwania urais, walipewa adhabu hiyo ya onyo kali
na Kamati Kuu Februari 18, mwaka jana baada ya kuthibitika kuanza
kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati, kinyume na
kanuni za uongozi na maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)
(i).
Vilevile
baada ya kuhojiwa, walithibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili
ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani
ya jamii.
Kutokana
na adhabu ya onyo kali, vigogo hao kwa mwaka mzima walikuwa katika hali
ya kuchunguzwa, ili kuwasaidia katika jitihada za kujirekebisha.
Pia
kamati ndogo ya udhibiti iliagizwa kuchunguza na kuchukua hatua kwa
wote waliohusika kwa namna moja au nyingine, katika vitendo hivyo
vilivyovunja kanuni za chama.
Moja
ya vitu vinavyosababisha wachambuzi wa siasa kuamini umuhimu wa ajenda
hiyo katika kikao cha leo, ni tamko la chama hicho lililotolewa Januari
mwaka huu, baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu.
Katika
tamko hilo, CCM iliweka wazi kuwa baada ya kukamilika kwa adhabu hiyo,
Kamati Kuu ndio kikao ambacho kingefanya tathmini ya utekelezaji wa
adhabu hiyo kwa vigogo hao.
Tamko
hilo lilienda mbali zaidi na kubainisha kuwa, vigogo ambao watabainika
katika kikao hicho cha tathmini, kuwa walikiuka masharti ya adhabu
hiyo, adhabu zao zingeongezwa.
Kabla
ya kuhukumiwa kutojihusisha na masuala ya kampeni kwa mwaka mmoja,
Kamati ya Maadili ya CCM, inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM
Tanzania Bara, Philip Mangula, iliwahoji watuhumiwa hao.
Miongoni
mwa wajumbe walioshiriki kuhoji watuhumiwa hao mbali na Mangula,
alikuwepo Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, William Lukuvi ambaye
ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Shamsi Vuai
Nahodha, ambaye alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Ajenda
nyingine inayotarajiwa kunguruma katika kikao hicho ni kuhusu vigogo wa
chama hicho, waliokumbwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kikao
cha Kamati Kuu ya CCM cha Januari kilichoketi Zanzibar, kilieleza
kusikitishwa kwake na baadhi ya viongozi wake walio katika dhamana ya
kisiasa kukumbwa na kashfa hiyo.
Aidha,
kiliagiza Kamati ya Maadili kuchukua hatua za kimaadili kwa wale wote
waliohusika na ukiukaji wa maadili kwenye sakata la Escrow, ambao wako
kwenye vikao vya uamuzi vya chama.
Wanaotuhumiwa
na kukiuka maadili katika fedha hizo ni pamoja na Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge, Ngeleja na Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Mwingine katika tuhuma hizo, ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
0 comments:
Post a Comment