Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye |
Siku
moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kusitisha makundi
yanayokwenda kumshawishi kugombea urais, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
CCM, Nape Nnauye, amempongeza kwa kutii agizo la chama hicho.
Nape
amesema hatua hiyo ya Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli ni nzuri kwa
kuamua kusitisha makundi kwenda kumshawishi agombee urais, ambayo kwa
siku chache mfululizo yalikwenda nyumbani kwake Monduli na mjini Dodoma
kwa nia hiyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana akiwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulahman Kinana wilayani Same, Kilimanjaro, Nape alisema anampongeza
Lowassa kwa kuwa amekubali kuheshimu kanuni, taratibu na Katiba ya chama
ambayo ndiyo inatakiwa kufuatwa na kila mwanachama wa CCM.
Jumanne
wiki hii, Nape alimuonya Lowassa kujiepusha na makundi hayo kwa kuwa
kufanya hivyo ni kukiuka kanuni na taratibu za chama na kwamba, hali
hiyo inamkosesha sifa ya kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM.
Nape
alisema walimtaka Lowassa, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC) ya CCM azuie makundi yanayokwenda nyumbani kwake kwa ajili
ya kumtaka agombee urais kwani kilichokuwa kinafanyika ni kuanza kampeni
kabla ya wakati.
“Kilichokuwa
kinafanyika ni kuanza kampeni kabla ya wakati na kwa mujibu wa chama
chetu ni makosa, maana anakiuka taratibu na kanuni za chama. Hatuwezi
kukaa kimya wakati kanuni zinavunjwa wazi, hivyo nimpongeze Lowassa kwa
kutii agizo la chama,” alisema Nape.
Kuhusu
shutuma kuwa kauli anazozitoa siyo za chama bali zake binafsi, Nape
alisema yeye ndiye msemaji pekee wa chama na hakuna msemaji mwingine,
hivyo kauli zinazotolewa ni za chama na siyo zake.
“Kanuni
na taratibu ambazo nazisimamia zipo miaka mingi kabla ya mimi kuzaliwa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM nchi nzima niko peke yangu, hivyo
lazima nisimamie misingi ya itikadi pamoja na kanuni na katiba ya chama
chetu. Kwa nafasi yangu siwezi kukaa kimya wakati kuna watu wanakosea,” alisema Nape.
Akizungumzia kuhusu wapambe wa makada wanaotaka urais, Nape aliwataka kuwa makini wasije wakawaharibia sifa wagombea wao.
“Ni
vizuri wataka urais wakawa makini na ushauri kutoka kwa wapambe wao
kwani wanaweza kuwasababishia kukosa sifa ndani ya chama, nawashauri
wote wanaotaka kugombea urais kupitia CCM kutowasikiliza wapambe wao kwa
kila wanachoambiwa, maana kuna ushauri mwingine unaweza kuwakosesha
sifa za kugombea urais,” alisema Nape.
Alisisitiza
kwamba, kwenye hilo si kwa wapambe wa Lowassa tu, bali ni kwa wapambe
wote waliopo nyuma ya makada wanaotaka kugombea urais mwaka huu.
“Ni
muhimu kwa makada wote kuhakikisha wanaheshimu kanuni, taratibu na
miiko ya chama ili wawe salama, kinyume cha hapo watajipoteza sifa,” alisisitiza Nape.
Aliwahakikishia
makada wa CCM kwamba chama hicho kitatenda haki kwa kila anayeomba
nafasi ya uongozi na hakuna atakayenyimwa haki yake.
“Kwa
wote ambao watakuwa makini katika kuzingatia kanuni na taratibu za
chama, haki zao zitalindwa, lakini wale ambao watakiuka kwa makusudi,
hao hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao,” alisema na kuongeza:
“Ndio
maana tunaendelea kuwakumbusha makada wote wazingatie kanuni na katiba
ya chama chetu. Kinyume cha hapo watakuwa wanajinyima wenyewe haki ya
kuomba ridhaa ya kugombea kupitia chama hiki.”
Juzi Lowassa aliwataka wanaotaka kumshawishi wasubiri utaratibu utakaotolewa na chama hicho kuhusiana na suala hilo.
Alitoa kauli hiyo baada ya kutembelewa na vijana 60 waendesha bodaboda kutoka wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya.
Kaskazini Watoa Tamko.
Zaidi
ya vijana 100 wakiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka mikoa ya Arusha,
Kilimanjaro na Manyara, wamekutana mjini Moshi na kutoa tamko linalodai
kwamba, iwapo Lowassa atapoteza sifa za kugombea urais, CCM kijiandae kisaikolojia kwa sababu kinaweza kupasuka na kushindwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Vijana
hao kutoka Jumuiya za Vyuo Vikuu vya Kanda ya Kaskazini na wengine
kutoka sekta binafsi, walitoa angalizo hilo jana mjini Moshi kwa
waandishi wa habari, ikiwa ni siku moja tangu Lowassa ajibu kauli ya
Nape aliyoitoa Jumanne akidai hawezi kuzuia mafuriko kwa mkono.
Akisoma
tamko hilo, Mratibu wa marafiki wa Lowasa wa Kanda ya Kaskazini, Noel
Nnko, alisema vijana katika mikoa hiyo hawatasita kuendelea kumshawishi
Lowassa kutangaza nia ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho kwa kuogopa
kauli ya Nape.
Walidai
kauli yake ambayo haina baraka za chama inawadhihirishia Watanzania
kwamba kuna mgombea wanayemtaka na si anayetakiwa na wananchi.
0 comments:
Post a Comment