Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali akichangia mjadala katika kikao cha Bunge, mjini Dodoma. |
Wabunge hao waliufananisha muswada huo na miswada
miwili ya habari ya mwaka 2015 ambayo itawasilishwa bungeni Jumanne
chini ya hati ya dharura kwa usiri uliopo na mpango wa kuiwasilisha bila
wadau kushirikishwa.
Awali, muswada wa Takwimu uliwasilishwa kwenye
mkutano wa 17 wa Bunge uliofanyika Novemba mwaka jana na wabunge
wakapinga vifungu vinavyobana waandishi wa habari kuhusu eneo la
takwimu, ndipo Serikali ilipoamua kuutoa kwa maelezo kuwa inakwenda
kuurekebisha hadi ilipourejesha jana na ukapitishwa kwa mbinde.
Jana, Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha
muswada huo, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alihoji juu ya
kifungu hicho kinachotoa adhabu kali na Serikali kujibu kuwa
imeshakifanyia marekebisho.
Hata hivyo, Mnyika hakukubaliana na maelezo hayo,
bali alisema kifungu hicho hakijafanyiwa marekebisho yoyote na Serikali
na adhabu bado inaendelea kuwa kali.
Mnyika aliungwa mkono na mbunge wa Viti Maalumu
(CCM), Ester Bulaya aliyehoji, “Iweje Serikali iweke kinga kwa mtumishi
wa Serikali anayetoa taarifa zisizo sahihi lakini ikaacha kuweka kwa
mwandishi anayepewa taarifa hizo zisizo sahihi na ofisa huyo wa
Serikali?”
Maelezo ya Bulaya yalimfanya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), George Masaju kusimama na kusema kwa kifupi kuwa
“mwandishi atakwenda kujieleza mahakamani au polisi.”
Ilivyokuwa mwaka jana
Kabla ya kuondolewa bungeni Novemba 2014 muswada
huo pamoja na mambo mengine, ulikuwa ukipendekeza faini ya Sh10 milioni
au kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa chombo cha habari
kitakachotoa taarifa za kitakwimu za uongo au zenye upotoshaji.
“Mtu yeyote, kwa kujifanya anatimiza majukumu
yake, iwapo anapata au anaomba kupatiwa taarifa ambayo haijaidhinishwa
kuipata na kuichapisha au kuisambaza atakuwa amefanya kosa ambalo adhabu
yake ni kifungo kisichopungua miezi 12 au faini isiyopungua shilingi
milioni mbili au vyote kwa pamoja,” ilisema ibara ya 37 (d) cha muswada
huo.
Muswada huo pia ulikuwa ukiainisha kwamba takwimu
rasmi ni zile ambazo zimetolewa na kuidhinishwa na taasisi zilizoelezwa
kwenye ibara hiyo ya 20 na ndizo pekee zinazoweza kutumika kama ushahidi
kwenye kesi.
Adhabu kali pia zimependekezwa kwenye muswada huo
kwa vyombo vya habari ambavyo vitatoa taarifa za takwimu
zitakazosababisha watu wasishiriki kwenye shughuli zilizoandaliwa na
Serikali zinazohusiana na masuala ya takwimu.
Muswada huo unapendekeza pia adhabu kali kwa watu ambao
watakataa kutoa ushirikiano kwa watu waliotumwa kufanya kazi za
ukusanyaji taarifa kama vile sensa na adhabu iliyopendekezwa ni faini
isiyopungua Sh5 milioni, kifungo kisichopungua miezi 12 au vyote kwa
pamoja.
Miswada yapita
Miswada mingine iliyopitishwa na Bunge jana ni
muswada wa Usimamizi wa Kodi wa Mwaka 2014, wa Sheria ya Marekebisho ya
Uhamiaji wa mwaka 2014 na Wakala wa Usimamizi wa Kodi wa mwaka 2014.
0 comments:
Post a Comment