KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye |
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye amesema vyama vya
upinzani vitaendelea kuwa wasindikizaji wa CCM katika chaguzi mbalimbali
zitakaofanyika nchini kutokana na wananchi wengi kuendelea kukiamini chama
hicho.
Aidha amesisitiza kuwa Katiba
Inayopendekezwa itapita kwa kishindo wakati wa Kura ya Maoni itakayofanyika
Aprili 30, mwaka huu, pamoja na kelele na shinikizo la vyama vya upinzani
kutaka wananchi kususia upigaji kura wa Katiba hiyo.
Nape aliyasema hayo katika
maeneo mbalimbali ya wilaya ya Chamwino, wakati Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana alipofanya ziara wilayani humo katika mwendelezo wa ziara yake ya
kuutembelea Mkoa wa Dodoma.
Akizungumzia ushindi wa chama
hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa udiwani, ubunge na urais, Nape alisema
hakuna siri kuwa vyama vya upinzani vitaendelea kuisindikiza CCM ili kushinda
viti vingi vya udiwani, ubunge na kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi wa
urais.
“Ndugu zangu nataka niwaeleze
wazi kwamba vyama vya upinzani ni kama mpambe wa Bwana Harusi, ambaye pamoja na
kufanya shughuli zote za usaidizi na upambe kwa Bwana Harusi lakini safari yake
huishia sebule maharusi wanapofika nyumbani,” alisema Nape.
Alisema tayari ishara ya
ushindi wa CCM imeonekana katika uchaguzi wa serikali za mitaa, ambapo CCM
imeshinda kwa kishindo kwa kunyakua viti vingi kwenye vitongoji, mitaa na
vijiji, huku vyama vya upinzani vikiambulia ushindi katika baadhi ya maeneo.
“Nataka niwaambie wazi,
wananchi wa nchi hii bado wana imani kubwa na CCM, ukiona kuna mtu anakipenda
chama cha upinzani ujue anasumbuliwa na ushamba tu na si kitu kingine. Sisi
tumezunguka nchi nzima na tumegundua wakati CCM inazidi kuimarika na kupanda
juu, vyama vya upinzani vinazorota na kushuka chini, wenye macho na walione
hili,” alisena Nape
0 comments:
Post a Comment