SAKATA la winga wa timu ya Simba, Ramadhan Singano ‘Messi’, akidai
mkataba wake umechezewa na klabu yake hiyo sasa limefika rasmi kwenye
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili utata wake kumalizwa.
Messi amekuwa na mvutano mkubwa na klabu yake akidai mkataba wake wa
miaka miwili umechezewa kwa kuongezewa mwaka mmoja zaidi unaoisha Julai
mwakani, tofauti na ule alionao yeye unaomalizika mwezi ujao.
Katibu Msaidizi wa Chama cha Wanasoka Tanzania (Sputanza), Abeid
Kasabalala, aliliambia MTANZANIA kuwa wameshayafanyia kazi malalamiko
hayo ya Messi kwa mujibu wa vielelezo alivyoviwasilisha na jana asubuhi
wamelipeleka suala hilo TFF kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.
“TFF ndio wenye mpira wao, tumelipeleka suala hilo huko leo asubuhi
(jana), wenyewe wamelichukulia kwa uzito mkubwa na wameahidi kulifanyia
kazi kwa haraka kwa kulipeleka kwenye kamati husika.
“Suala hilo limefika sehemu nzuri kwani kilichopo TFF watalinganisha
mikataba waliyokuwa nayo na ile ya Messi ambayo inadaiwa kuwa na utata,
wala hamna kazi kubwa sana tunaamini haki itatendeka,” alisema.
Uongozi wa Simba kupitia Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Haji
Manara, jana ulisema kuwa haujachezea mkataba wa nyota huyo huku ukifika
mbali zaidi na kudai wapo kwenye mchakato wa kumwadhibu Messi kutokana
na kuichafua klabu hiyo.
Manara pia alieleza kuwa wanaiomba TFF kutoa tamko kuhusu sakata hilo,
kwani wana vielelezo vyote vya mikataba wanayoingia na wachezaji wao
akiwemo Messi, huku wakidai wapo tayari suala hilo lichunguzwe na vyombo
vya dola.
Azam FC imeonyesha nia ya kumsajili Messi lakini wamedai kuwa hawataanza
taratibu zozote za usajili wake mpaka pale matatizo na klabu yake
yatakapomalizika.
Wakati huo huo mshambuiaji mahiri wa timu ya Taifa ya Burundi na klabu
ya Vital, ‘O Laudit Mavugo, anatarajia kutua rasmi Simba Juni 16 mwaka
huu kumalizana na timu hiyo tayari kwa kujiunga na wenzake kwenye
maandalizi ya michuano ya Kagame inayotarajia kuanza Julai 12, Dar es
Salaam.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu
hiyo, Zacharia Hanspoppe, alisema asilimia kubwa ya mazungumzo yao na
mchezaji huyo yamekamilika kinachosubiriwa ni yeye kutua nchini na kutia
saini mkataba wake.
“Tumeamua kumwacha kwa muda ili kuweza kukamilisha ratiba ya michuano na
timu yake ya Taifa, baada ya hapo atatua nchini kwa ajili ya
kukamilisha taratibu zilizobakia,” alisema.
Alisema kwa sasa wamejipanga kufanya usajili kwa utulivu na hawataki
kukurupuka, kwani wanahitaji mabadiliko kuanzia kwenye michuano hiyo ya
kiamataifa hadi ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2015/2016.
Hadi sasa Simba imesajili wachezaji Mohamed Fakhi (JKT Ruvu), Samir Nuhu
(Azam), Mohamed Abraham (JKU Zanzibar), Peter Mwalyanzi (Mbeya City) na
Mussa Hassan ‘Mgosi’ (Mtibwa).
Wakati wakijiandaa na michuano hiyo, hatima ya kupatikana kwa kocha
mpya, wachezaji watakaoiaga timu hiyo na watakaoenda kwa mkopo kwenye
timu nyingine itapatiwa ufumbuzi kwenye kikao cha ndani cha klabu hiyo,
kilichofikia tamati jana baada ya kudumu kwa muda mrefu.
Timu hiyo inatarajia kuanza mazoezi rasmi Jumatatu wiki ijayo Uwanja wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kujiandaa na michuano hiyo ya
Kagame.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment