YANAHUSU MAONI YA KATIBA, WARIOBA AGOMA
TUME ya
kukusanya maoni ya Katiba mpya inayoongozwa na Jaji mstaafu, Joseph
Warioba, jana imegoma kupokea maboksi 17 ya maoni yaliyokusanywa na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na badala yake ikapokea
vitabu viwili vya randama kwa ajili ya maoni hayo.
Kutokana na
tume hiyo kukataa kupokea ushahidi wa kile kilichoandikwa katika randama
mbili zilizowasilishwa na CHADEMA, chama hicho kupitia kwa Katibu Mkuu
wake, Dk. Willibrod Slaa, kimesema mpango huo unaashiria dhamira ya tume
hiyo kuvibeba vyama ambavyo havina ushahidi wa ukusanyaji wa maoni
kutoka kwa wananchi.
Maoni hayo
ya wananchi kuhusu rasimu ya Katiba, yamekusanywa kupitia mikutano mbali
mbali iliyofanywa na CHADEMA yalifikishwa katika ofisi za tume jana
majira ya saa 5:56 asubuhi yakiwa katika gari aina ya Range Rover yenye
namba T 162 CDA, ambapo ndani ya gari hilo alikuwamo Dk. Slaa, huku
maofisa wengine wa CHADEMA wakiwa katika magari tofauti.
Mara baada
ya kukabidhi maoni hayo ya wananchi, Dk. Slaa alisema amesikitishwa na
hatua ya tume hiyo kushindwa kubaki na maoni yaliyokusanywa kupitia
taasisi zinazoeleweka kwa kile alichoeleza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa
tume hiyo kupokea maoni ya watu waliojifungia ndani na kusema maoni
hayo yametoka kwa wananchi.
Alisema tume
inaweza kuibua maswali kutoka kwa taasisi na wananchi namna inavyoweza
kujiridhisha na maoni yanayofikishwa kwao kwa kile alichoeleza kushindwa
kupokea maoni ya awali kutoka kwa wananchi.
Aidha, Dk.
Slaa alisikitishwa na utaratibu wa tume hiyo kushindwa kuwa na mpango
maalumu wa kupokea maoni na kuweka kumbukumbu ya upokeaji huo.
“Sijui kama
hawa watu walijipanga juu ya upokeaji wa maoni, angalia sisi kama
tusingelazimisha watugongee muhuri kwa ajili ya uthibitisho wa upokeaji
tungeondoka hivi hivi, sasa hali hii wamefanyiwa watu wangapi ambao
hawana kitabu cha kusaini?” alihoji Dk. Slaa.
Aliongeza
kuwa katika randama walizowasilisha kwa tume, wameweka hoja 66 baada ya
kujiridhisha na hoja nyingine zilizoko katika rasimu ya Katiba yenye
hoja 240.
Alisema hoja
ambazo hazijaguswa katika randama waliyowasilisha ni zile ambazo
zinakubaliwa na CHADEMA pamoja na wananchi waliotoa maoni kupitia
mikutano ya CHADEMA.
Namna walivyopata maoni
Kuhusu idadi
ya watu waliotoa maoni yaliyowasilishwa jana, Dk. Slaa alisema hadi
juzi walipokuwa wakifunga randama, kulikuwa na watu zaidi ya milioni 3.4
waliotoa maoni kwa njia mbalimbali.
Alitaja njia
hizo kuwa ni mabaraza ya wazi ambapo walikusanya maoni ya watu
3,200,889 kutoka katika majimbo 81 waliyoyafikia, katika mabaraza ya
ndani walifika kata 586 na kukusanya maoni 11,7274.
Njia
nyingine zilizotajwa na Dk. Slaa ni ngazi ya majimbo ambapo walifanya
mikutano ya ndani katika majimbo 189 ya Tanzania Bara na kukusanya maoni
130,000, kwa njia ya barua pepe walipata watu 612 waliotoa maoni huku
kukiwa na ujumbe mfupi wa simu kutoka kwa watu 12,345 pamoja na mitandao
ya kijamii na kufanya jumla ya watu waliotoa maoni kuwa 3,462,805.
Dk. Slaa
alisema ushahidi wa maoni hayo upo wazi kwao na kuwataka tume
ijiridhishe kwa vyama vingine vinavyosema wameshakusanya maoni ya watu
zaidi ya milioni mbili.
“Sisi
tumefanya haya na wenzetu walete ushahidi kama huu badala ya kukaa
vyumbani na kuwatengenezea Watanzania maoni na vitu vya kuingizwa katika
Katiba. Hapa tunaililia Tanzania tuitakayo na si kwa masilahi ya chama
chochote,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza
kuwa mazingira na matamko yanayotolewa na Chama Cha Mapinduzi kuwa
wamekusanya maoni ya wananchi wengi na hayawezi kufikiwa na vyama
vingine yana nia mbaya kwa nchi na hayaleti taswira nzuri kwa tume.
Usiri wa Tume kwa waandishi
Dk. Slaa pia
alisema licha ya tume kuweka suala la uwazi kuwa ni moja ya tunu za
taifa, bado imeshindwa kudhihirisha uwazi huo kwa kuwazuia waandishi wa
habari kuingia na kushuhudia makabidhiano yanayofanywa katika ofisi za
tume.
Alisema
suala la Katiba ni la Watanzania wote na vyombo vya habari ni mhimili
mkubwa wa serikali usio rasmi wenye kutegemewa kwa kiasi kikubwa na
wananchi kutoa taarifa sahihi, lakini vinapozuiwa kushuhudia matukio
hayo kwa uwazi ni kuwanyima fursa Watanzania kupata habari sahihi.
Aliongeza
kuwa kama tume ya Katiba inafanya usiri katika kupokea maoni ya
wananchi, wanaweza vipi kuwaridhisha Watanzania kuwa maoni waliyotoa
ndiyo yaliyofanyiwa kazi.
Kuhusu Kingunge
Akizungumzia
kauli ya Kingunge Ngombale- Mwiru, aliyoitoa juzi kuhusu umuhimu wa
serikali mbili, Dk. Slaa alisema Watanzania wanapaswa kumsamehe mzee
Kingunge kwa kuwa sasa amechoka.
Alisema
katika vitu alivyopaswa kuvifanya Kingunge katika muda wake wa utumishi
serikalini ni pamoja na kusimamia kero mbali mbali zinazolalamikiwa leo,
hivyo kuendelea kuwaambia wananchi wasifikirie juu ya muundo wa
Muuungano ni kuwakosea heshima.
“Mimi
ninamsamehe mzee wangu huyu ila atambue muungano ulio bora ni ule
unaoridhiwa kwa hiari na si kulazimisha mfumo unaoonekana una matatizo,”
alisema Dk. Slaa.
@Chadema Blog
0 comments:
Post a Comment