Jeshi la
Polisi limeingia katika kashfa nzito baada ya mkuu wake, Inspekta
Jenerali Said Mwema, kuibiwa upanga wa dhahabu ambao ni mali ya
Shirikisho la Wakuu wa Majeshi ya Polisi wa nchi za Kusini mwa Afrika
(SARPCCO).
Upanga
huo wenye uzito wa takriban kilo tatu na wenye thamani ya zaidi ya fedha
za Tanzania Sh600 milioni, ni kielelezo kwa nchi inayokabidhiwa uongozi
wa SARPCCO.
Mwaka
jana Tanzania ilikuwa mwenyekiti wa SARPCCO, ambapo upanga huo
ulikabidhiwa kwa IGP Mwema na Jenerali Magwashi Victoria 'Riah' Phiyega,
ambaye ni Kamishna wa Taifa wa Polisi wa Afrika Kusini aliyekuwa
amemaliza muda wake kwa wakati huo.
Hilo ni
tukio la pili la wizi la mali zinazohusu ofisi ya IGP, ambapo mwaka jana
ndani ya ofisi hiyo kuliibwa kompyuta ndogo (laptop), ikiwa na taarifa
muhimu za kipolisi. Hadi sasa hakuna taarifa za kupatikana kwa kompyuta
hiyo.
IGP Mwema
alikabidhiwa upanga huo Septemba 5, 2012, katika mkutano saba wa
SARPCCO uliofanyika Zanzibar na kuhudhuriwa na wakuu wa majeshi ya
Polisi kutoka nchi 13, pamoja na mashirika ya kimataifa.
Upanga
huo ambao unakwenda sambamba na bendera ya SARPCCO, ni moja ya vielelezo
vya nchi iliyochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa shirikisho hilo, ambaye moja
kwa moja anakuwa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi katika nchi husika.
Kwa
mujibu wa taratibu za SARPCCO, vielelezo hivyo hutakiwa kuwekwa ofisini
kwa kiongozi husika, ikiwa ni alama ya kila mgeni atakayeingia ofisini
hapo kutambua uwepo wa wadhifa huo wa kimataifa.
Uchunguzi
wa gazeti hili ulibaini kuwa IGP aligundua kutoweka kwa upanga huo wiki
iliyopita, wakati akijiandaa kwenda kuukabidhi kwa mwenyekiti mpya wa
SARPCCO, ambaye ni IGP wa Namibia.
Taarifa
za ndani ya jeshi hilo zilibaini kuwa, IGP alilazimika kuondoka bila
upanga huo alipokwenda Namibia wiki iliyopita kuhudhuria mkutano wa nane
wa SARPCCO, uliofanyika Jumapili iliyopita mjini Windhoek.
Kwa
mujibu wa uchunguzi, IGP Mwema alikabidhi upanga unaofanana na huo ambao
siyo wa dhahabu, alioazimwa kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi la
Namibia, Inspekta Jenerali, Luteni Jenerali Sebastian Ndeitunga, na
kukabidhiwa kama ishara ya kukabidhiwa uenyekiti wa SARPCCO kwa kipindi
cha mwaka mmoja.
Uchunguzi
ulibaini kuwa IGP Mwema alitoa ahadi ya kurejesha upanga halisi ndani
ya kipindi cha mwezi mmoja, au Serikali ya Tanzania italazimika
kutengeneza mwingine kulipa uliopotea.
Uchunguzi
wa gazeti hili unaonyesha kuwa kashfa hiyo ametupiwa Mkuu wa Polisi
Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa pamoja na dereva wake, ikidaiwa kuwa
upanga huo baada ya kupokewa na IGP Mwema, Septemba mwaka jana uliwekwa
kwenye gari la kamishna huyo.Kamishna Mussa ndiye alikuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Saba, na pia ofisa mwenyeji kwa
wajumbe wa mkutano huo uliofanyika Zanzibar.
Hata
hivyo, taarifa zingine zilidai kuwa IGP Mwema naye analaumiwa kwa
kutofuatilia kwa karibu zana za kazi, kwani baada ya kuupokea alitakiwa
kuhakikisha unakuwepo ofisini kwake kama alama ya uenyekiti wake.
Gazeti
hili lilipowasiliana kwa njia ya simu na Mkuu wa Polisi Zanzibar,
Kamishna Mussa Ali Mussa kuhusu madai hayo alisema, kitara (upanga)
hicho ni kweli kimepotea, lakini yeye hahusiki kwa kuwa kila kitu kina
utaratibu wake.
"Ni kweli
kitara kilikabidhiwa kwa afande IGP na mimi nilishuhudia kikikabidhiwa,
na ni kweli kitara hakijulikani kiliko, lakini mimi sihusiki na kupotea
kwake. Ni kweli mimi nilikuwa ofisa mwenyeji wa mkutano huo, lakini
siku hiyo zilitolewa zawadi nyingi, watu walipewa mikoba, kwa hiyo mtu
akipoteza mkoba wake niulizwe mimi?" alihoji Kamishna Mussa.
Alisema
kila kitu kina utaratibu wake na kwamba taarifa kwamba yeye amehojiwa
kutokana na upotevu wa kitara hicho au kuna kamati imeundwa, hazina
ukweli.
"Sijawahi
kuona kamati hiyo. Kamati hiyo kwanza imeundwa na nani na inatoka wapi?
Hayo maneno yanatengenezwa na watu wa nje," alisema Kamishna Mussa.
Alisema kinachofanyika hivi sasa ni kukitafuta ili kiweze kurejeshwa kunakohusika.
Taarifa
zingine zilidai hata bendera ya mezani ya mwenyekiti wa SARPCCO,
aliyokabidhiwa sambamba na upanga huo nayo kuna hatihati ilipotea.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema aulizwe kamishina wa polisi Zanzibar.
"Suala hilo muulize Kamishina wa Zanzibar ndiye anayejua," alisema Senso.
Uchunguzi
unaonyesha kuwa maofisa katika ofisi ya IGP na ile ya Kamishna wa
Polisi Zanzibar, wamehojiwa akiwamo Kamishna Mussa, na kwamba upelelezi
mkubwa umekuwa ukiendelea ndani ya jeshi hilo.
Hata
hivyo, juhudi za gazeti hili za kutaka kufahamu uamuzi wa SARPCCO katika
ofisi yake ya uratibu iliyopo kwenye ofisi za Makao Makuu ya Kanda ya
Polisi wa Kimataifa (INTERPOL), Harare, Zimbabwe, hazikuzaa matunda
baada ya baruapepe iliyotumwa kwa ofisa mratibu wa SARPCCO ambaye pia ni
mkuu wa ofisi ya Kanda ya INTERPOL, C. Simfukwe kutopata majibu.SARPCCO
ilianzishwa mwaka 1995, Victoria Falls, Zimbabwe, lakini kisheria
ilitambulika rasmi mwaka 2006 na lengo lake kuu ni kupambana na uhalifu
wa kuvuka mipaka.
Uenyekiti
wake ni mwaka mmoja, ambapo kwa sasa mwenyekiti ni Mkuu wa Jeshi la
Polisi la Namibia Inspekta Jenerali, Luteni Jenerali Sebastian
Ndeitunga, aliyepokea wadhifa huo kutoka kwa IGP Mwema.@Mwananchi
0 comments:
Post a Comment