MWANASIASA
mkongwe aliyewahi kuwa swahiba na mshauri mkuu wa Rais Jakaya Kikwete,
Kingunge Ngombale Mwiru, ametoa kauli nzito inayoonyesha hakubaliani na
msimamo wa Rais Kikwete na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kingunge akimkejeli
Rais na chama chake, ambacho yeye ni mmoja wa waasisi, alisema
walikurupuka kukubali na kuanzisha mchakato wa Katiba mpya.
Kwa mujibu
wa Kingunge, kabla ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza na kuanzisha
mchakato wa Katiba mpya, CCM haijawahi kufanya kikao na kuamua kuhusu
suala hilo, kama walivyofanya kabla ya mchakato wa kuingia kwenye mfumo
wa vyama vingi mwaka 1991.
Mbali na
kumshangaa Kikwete na chama chake, vile vile Kingunge aliwashambulia
wazee wenzake wanaounga mkono mapendekezo ya rasimu ya Katiba mpya
kuhusu muungano wa serikali tatu.
Katika hali isiyo ya kawaida, Kingunge alisema wazee hao ni “sawa na watu waliochanganyikiwa”.
Anasema
msimamo wake unatokana na ukweli kuwa CCM haijawahi kuwa na ajenda ya
kuandika Katiba mpya na kwamba ndiyo maana suala hilo halikuwa kwenye
ilani ya uchaguzi ya CCM 2010.
Alisema hoja ya Katiba mpya ni ya wapinzani, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kingunge alisema kimsingi aliyeafikiana na hoja ya wapinzani kuhusu Katiba mpya ni Rais, si CCM.
Kuhusu wazee
hao ambao alisema “wamechanganyikiwa” Kingunge alisema anashangaa kuona
wazee ni miongoni mwa wanaopendekeza muundo wa serikali tatu, kwani
baadhi yao walishiriki katika kuunda mfumo huu uliopo ambao umedumu
tangu mwaka 1964.
Alisema
muungano wa serikali mbili umeleta mafanikio kwa kujenga udugu na umoja
wa kitaifa na kwamba kwa sababu hiyo ungeachwa uendelee badala ya kupiga
kelele kwamba ufutwe, ziletwe serikali tatu.
Alisema
baadhi ya viongozi wameshindwa kuthamini mafanikio ya muungano na sasa
mawazo yao yote yamekuwa yakielekezwa kwenye vyeo vyenye marupurupu.
Aidha
alipinga kauli za baadhi ya viongozi wanaosema kuwa kuwepo kwa serikali
tatu kutasaidia kuimarisha muungano. Alisema serikali tatu zitaua
muungano.
Kingunge aliongeza kuwa kama serikali mbili ni sababu za kufa muungano huo, basi usingeweza kudumu kwa miaka 50 sasa.
“Huu ni
mpango wa wakubwa kutaka kujiwekea mazingira ya vyeo, kwani wapo ambao
tayari wamekwishajiandaa kuwania urais wa Tanganyika.
“Nilishangaa
sana hata huko bungeni watu wanapeana sifa za kuwa fulani anastahili
kuwa Rais. Huu ni upotoshaji mkubwa kwa taifa,” alisema, akirejea kauli
iliyotolewa juzi na Waziri asiyekuwa na wizara maalumu, Profesa Mark
Mwandosya, aliyemfagilia Spika wa Bunge, Anna Makinda, kwamba anafaa
kuwa Rais.
Kingunge
aliongeza kuwa kwa maoni yake lazima Katiba mpya iweke mipango ya
maendeleo ambayo itashirikisha wananchi wa ngazi zote.
Kingunge alisema isiwe mipango hiyo inapangwa na viongozi kutoka juu na kuishusha chini bila kujua wanahitaji nini kabla.
Alisema Katiba inayotakiwa ni ile itakayosimamia na kupatikana kwa maendeleo yanayofanana kati katika jamii.
Kuhusu uraia
wa nchi mbili, Kingunge alisema suala hilo lilikuwa linasemwa pembeni
lakini sasa wanataka suala liingizwe kwenye Katiba.
“Mwanzo
nilijua ni utani lakini nilishangaa suala hili kubwa kuliona limeingizwa
kwenye kijitabu kilichotolewa na chama changu na kupendekeza hivyo,”
alisema.
Alisema
suala la uraia ni la nchi, hivyo chama kilipaswa kutoa nafasi kwa
wananchi kujadili kwa kina jambo hilo na sio viongozi kujiamulia
wenyewe.
“Kwa mfano
nchi yetu ilipovamiwa na Nduli Idd Amini kama kungekuwa na vijana wenye
uraia wa nchi mbili wangejiweka upande gani, hii ni mipango ya watu
wanaopenda kunogewa na maisha kwenye nchi za watu,” alisema.
Alisema
amekuwa kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kwa muda mrefu
lakini hakuwahi kusikia hata siku moja kujadiliwa suala hilo ambalo
ameliita kuwa la hatari.
Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeeleza kuiunga mkono rasimu hiyo
kwa asilimia 80 kulingana na maoni ya watu milioni 3.4 waliokusanya.
Hata hivyo, CHADEMA imeainisha hoja 11 ambazo wananchi wamependekeza ziongezwe katika rasimu hiyo ya Katiba mpya.
Akizungumza
na waaandishi wa habari jana makao makuu ya chama hicho, Katibu Mkuu wa
CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa alisema mrejesho huo umepatikana baada ya
kuwazungukia wanachama wao na Watanzania wengine kwa wiki mbili.
Dk. Slaa
alisema maoni hayo yamekusanywa kupitia kanda 10 za chama hicho na
Watanzania waishio nje ya nchi kwa njia ya kisayansi huku yakiwa na
vithibitisho tofauti na vyama vingine vya kisiasa.
Huku
akieleza kuwa bado wanakusanya takwimu za Watanzania walioandika ambazo
zinatoka mkoani, hadi jana walikuwa wamekusanya maoni kutoka katika
mabaraza ya Katiba 117,274 yaliyoendeshwa na madiwani.
Alisema kuwa
waliendesha mabaraza ya wazi 3,200,889, ya ndani 130,004 na kukusanya
maoni yaliyotumwa kwa njia ya barua pepe 612, ujumbe kwa njia ya simu za
mikononi 12,345 na mitandao ya kijamii 1,681.
Dk. Slaa
alisema katika ziara hiyo, watanzania walisisitiza mambo 11 ambayo yapo
katika rasimu hiyo na mapya kwa ajili ya kuongezwa kwa lengo la
kuboresha rasimu hiyo kuwa ni pamoja serikali tatu yaani ya Jamhuri ya
Muungano, Tanganyika na Zanzibar.
Pili, ni kuitaja na kuiweka katika Katiba mpya mipaka ya Tanganyika na Zanzibar ili kudumisha amani ya nchi hizo na jirani zao.
Kuhakikisha
haki ya kila raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka 18
kupiga na kupigiwa kura katika uchaguzi wowote unaofanywa katika
jamhuri.
Hoja zingine
ni swala la haki ya kupatiwa malipo ya uzeeni pamoja na msaada wa
hifadhi ya jamii kwa gharama ya serikali wakati wa uzeeni, haki ya
kupatiwa msaada wa matibabu, haki ya jamii kumiliki rasilimali za asili
kama vile ardhi, madini, mafuta na gesi asilia, maji na misitu na
wanyamapori vitumike kwa manufaa ya Watanzania.
“Iwe
marufuku kwa mamlaka ya serikali ya jamhuri za washirika wake kutwaa
rasilimali asili kwa malengo ya kuzigawa kwa wawekezaji au kwa malengo
yoyote bila ya kupata ridhaa huru na ufahamu wa wananchi wanaoishi
kwenye eneo zinakopatikana rasilimali hizo,” alisema.
Pia suala la uraia wa nchi mbili, mtu hatapoteza uraia wa Jamhuri ya Muungano kwa sababu tu ya kuwa na uraia wa nchi nyingine.
Yapo pia
masuala ya muungano yaani maadili na miiko ya uongozi na utumishi wa
umma, haki za binadamu na wajibu wa raia, tume huru ya taifa ya uchaguzi
na masuala yote yanayohusu uchaguzi.
“Tume huru
ya uchaguzi itatangaza matokeo ya uchaguzi wa Rais haraka iwezekanavyo
na kwa vyovyote vile kabla ya kupita siku saba tangu tarehe ya uchaguzi
huo.
“Rais mteule
atakabidhiwa madaraka ndani ya siku tisini baada ya kutangazwa kuwa
ameshinda, wakati wote Rais akiwa madarakani na baada ya kuacha kushika
madaraka hayo anaweza kushtakiwa kwa ajili ya kosa lolote la jinai chini
ya sheria au chini ya mkataba wowote wa kimataifa ambao jamhuri ya
muungano ni mwanachama,” alisema.
Alitaja hoja
ya kumi kuwa ni siku ya kupiga kura isiwe ni siku ya kuabudu ya imani
ya dini yoyote ile, bali iwe siku ya kazi ambayo itapaswa kutangazwa
kama siku ya mapumziko.
Dk. Slaa
alisema pamoja na ibara 68 za rasimu ambazo zimetolewa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, CHADEMA wakati inazunguka imekutana na mambo 11
hayo ambayo yalikuwa yakisisitizwa na wananchi.
NCCR-Mageuzi
Chama cha
NCCR-Mageuzi kimependekeza kuwepo na serikali tatu ya Tanganyika,
Zanzibar na Shirikisho itakayokuwa chini ya mkataba wa kimataifa.
Pia alisifu
usikivu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba
kutokana na kurasimu baadhi ya mapendekezo ya chama hicho katika
ushiriki wake kuhusu utayarishaji wa rasimu hiyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa
chama hicho, Mosena Nyambabe, kuhusu maoni na mapendekezo yao kwa tume,
alisema wameona kuna haja ya kurejeshwa kwa nchi ya Tanganyika
itakayokuwa na mamlaka yake kamili sawa na Zanzibar.
Alisema chama hicho kimeona umuhimu wa mapendekezo 18 ya Muungano yaliyoakisiwa na Tume ya Mabadiliko kupewa kipaumbele zaidi.
Aliyataja
mambo hayo kuwa ni pamoja na suala la Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya
Muungano, Ulinzi na Usalama, sarafu za Benki kuu, mambo ya nje, vyama
vya siasa, ushuru wa bidhaa na mapato ya kodi yatokanayo na mambo ya
muungano.
HABARI kwa Hisani ya Chadema Blog.
0 comments:
Post a Comment