HUKUMU YA FEDHA ZA EPA: Washtakiwa jela miaka 26.

Bahati Mahenge kifungo cha miaka sabManase(me) mitano, Eda(ke) miezi 1  Wawili waachiwa huru kwa kutokuwa na hatia.
Washtakiwa kesi ya EPA toka kushoto Bahati Mahenge, Manase Mwakele na Eddah Mwakale wakiwa mbele ya Mahakama ya Kisutu kusomewa shitaka lao na kufungwa jela.

Kesi ya wizi wa Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyounguruma kwa miaka mitano, jana imefikia tamati baada ya washitakiwa watatu kuhukumiwa kifungo cha jumla ya miaka 26 jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kukutwa na hatia ya wizi wa Sh bilioni 1.1.


Waliohukumiwa ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Bahati Mahenge (kifungo cha miaka saba), mshtakiwa wa pili na watano ambao ni mume na mke, Manase Makale (kifungo cha miaka mitano na Eda Makale (kifungo cha miezi 18).

Hukumu hiyo ilitolewa jana huku washtakiwa wa tatu Davis Kamungu, na wa nne Godfrey Mosha wakiachiliwa huru baada ya kukosekana na hatia katika mashtaka yote saba yaliyokuwa yakiwakabili.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jopo la Mahakimu Wakazi watatu, wakiongozwa na Mwenyekiti Sekela Mosha. Wengine ni Sam Rumanyika na Lameck Mlacha.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mlacha, alisema katika adhabu hizo, mshtakiwa wa kwanza na wa pili watatumikia kifungo cha miaka mitano jela, huku shitaka la pili lililowatia hatiani, watatumikia miaka mitano mingine.
Akifafanua jinsi ya kutumikia adhabu hiyo, Hakimu Mlacha alisema zitaenda sambamba.

Alisema shitaka la tatu lililomtia mshtakiwa wa kwanza hatiani, atatumikia miaka saba jela, shitaka la nne kwa mshitakiwa wa kwanza na pili, watatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.

Shitaka la tano lililowatia hatiani mshtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tano, watatumikia miezi 18 jela na shitaka la sita mshitakiwa kwanza na wa pili, watatumikia miezi 18 huku shitaka la mwisho mshitakiwa wa kwanza, atatumikia miaka mitano jela.

Baada ya kusoma majumuisho kutoka pande zote mbili na mashahidi pamoja na vielelezo mbalimbali vilivyoletwa mahakamani hapo, Hakimu Mlacha, alidai kuwa mshitakiwa wa kwanza na wa pili wameonekana kula njama ya kutenda kosa.

Alidai kuwa makubaliano yapo wazi kwamba Mahakama imekataa maelezo ya Wakili wa utetezi, kwamba mshitakiwa wa kwanza hakutenda kosa.

Pia alidai Mahakama imeshindwa kukubaliana na upande wa mashitaka katika majumuisho yao waliyopeleka mahakamani wakiitaka Mahakama ifungue milango kwamba mshitakiwa wa tatu na wa nne walitenda kosa kwa kutumia kielelezo namba 7, kilichopokelewa mahakamani hapo kama ushahidi.

Hakimu Mlacha alisema katika kielelezo hicho cha mshitakiwa wa tatu kilichoonyesha mshitakiwa alipewa Sh. milioni 41, kinaonyesha mshitakiwa huyo alilipwa fedha hizo kabla fedha za EPA hazijaibiwa.

Katika ushahidi uliotolewa kuhusu mshtakiwa wa nne, hakimu Mlacha alisema shahidi alidai mahakamani kuwa mshitakiwa huyo alilipwa Sh. milioni 200, lakini upande wa mashitaka haukuwasilisha hundi mahakamani kama kielelezo.

Alidai mshitakiwa wa kwanza, Mahenge, alisaini Memorandum Form namba moja yenye namba 14 na 15 kwa jina la Samson Mapunda, jina ambalo ni la kufikirika.

Aidha, alidai kuwa aliweka katika fomu hizo taarifa za uongo kuhusu anuani ya makazi, eneo la kampuni na taarifa hizo kampuni ya Changanyikeni Residential Complex kuwa ilisajiliwa na BRELA na kwa namba 47792.
Aliongeza kuwa katika utetezi, wazazi wa mshtakiwa Mahenge walidai mahakamani kuwa mtoto wao ana majina matatu.

Hakimu Mlacha aliendelea kudai kuwa Mahakama inafahamu si majina yote watu wanaopewa ni ya ubatizo ila inatia shaka pale mtu anapopewa majina mapya.

Alisema katika ushahidi huo wazazi hao walionekana kama hawakusema ukweli na kwamba Samson Mapunda ni jina la kufikirika.

Alidai ili kukamilisha lengo hilo mshitakiwa wa kwanza, alisaini Memorandum Form namba moja yenye namba 14 na 15 kwa jina la Samson Mapunda, jina ambalo ni la kufikirika na shahidi wa saba wa Jamhuri alithibitisha.
Katika shtaka lingine la kujipatia usajili wa kampuni, ushahidi uliotolewa na shahidi wa saba unathibitisha kwamba washtakiwa wa kwanza na wa pili, wanahusika.

Katika shtaka la kughushi linalowakabili washtakiwa wote Hakimu Mlacha alidai mshtakiwa wa kwanza alikubali kuwa alisaini na katika kielelezo cha 7 na 14 kilijaribu kumuunganisha mshtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tano.

Aliendelea kudai, washitakiwa hao walifungua akaunti benki ya CRDB Tawi la Kijitonyama na Agosti 31 mwaka 2005, Mahenge alisaini fomu nyingine kwa jina hilo la kufikirika na fomu hiyo ilionyesha kufanyika makubalino kati ya kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan na Changanyikeni Residential Complex na katika makubaliano alidai kwamba Changanyikeni imepewa kibali cha kukusanya deni la kampuni ya Marubeni.

Hakimu Mlacha alidai kuwa kielelezo namba 7 kilichowasilishwa mahakamani, kinaonyesha ni cha kughushi na mshtakiwa wa kwanza alidai kuwa kipo sahihi na upande wa utetezi uliomba ushahidi wa shahidi wa sita uangaliwe na jopo la Mahakimu limetofautiana nao.

Aliongeza kuwa hawakuona uzito kwenye ushahidi uliotolewa na shahidi wa sita na saba katika kesi hiyo na kudai kuwa pengine walitakiwa wawe pia washtakiwa katika kesi hiyo.

Aidha alidai shitaka la saba, limethibitishwa kwa washitakiwa wa kwanza na wa pili tu.
Hata hivyo, Mahakama iluitupilia mbali shitaka la nane na la tisa la wizi na ingizo la fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na washtakiwa wote waliachiwa huru katika mashtaka hayo.

Awali hati ya mashtaka katika kesi hiyo ilisomeka washtakiwa katika kesi hiyo ni Bahati Mahenge, Manase Makale, Davis Kamungu, Godfrey Mosha na Eda Makale ambao kwa pamoja walikuwa wakikabiliwa na mashtaka tisa. 

www.Info@Dira Yetu.Blogspot.com 
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment