KATIBA MPYA NJIA PANDA KUPATIKANA, UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA KUFANYIKA MWAKANI!!

 

Sasa ni dhahiri kuwa Katiba mpya iko njia panda kupatikana kinyume cha matarajio ya wengi kuwa ingepatikana kabla ya uchaguzi mkuu wa mwakani.

Matumaini ya kupatikana kwa Katiba mpya kwa muda huo sasa yamepotea baada ya kura ya maoni ya kuikubali au kuikataa itakayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba iliyokuwa ifanyike Aprili mwakani, kuahirishwa hadi baada ya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.

Aidha, uchaguzi wa serikali za mitaa ambao ulikuwa ufanyike baadaye mwaka huu nao umeahirishwa hadi mapema mwakani.Kuahirishwa kwa kura hiyo hadi baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwakani, kunamaanisha kwamba ni wazi kuwa itapigwa mwaka 2016.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), John Cheyo, wakati akitoa taarifa ya kikao cha viongozi wa kituo hicho na Rais, Jakaya Kikwete, kilichofanyika juzi mjini hapa.

Alisema hatua hiyo ina lengo la kutoa nafasi ya kufanyika maandalizi ya chaguzi hizo kubwa nchini.Cheyo katika mazungumzo hayo na waandishi wa habari alikuwa amefuatana na Mwenyekiti wa TLP, Dk. Augustino Mrema, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara, Philip Mangula, Mwenyekiti wa UPDP, Fahami Dovutwa.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mwisho wa mchakato wa Katiba Mpya ni kura ya maoni itakayofanyika Aprili, mwakani, hivyo kikao hicho na Rais kimeona endapo mchakato huo utaendelea hadi kura ya maoni kutaathiri uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwakani.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, baada ya Bunge Maalum kumaliza kutunga Katiba ingefuata hatua ya kura ya maoni kuthibitisha Katiba, kwa kutambua kuwa hatua ya kura ya maoni italazimisha uchaguzi mkuu 2015 kuahirishwa, tumekubaliana hatua hii iairishwe,” alisema na kuongeza: 

“Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, mwisho wa mchakato ni kura ya maoni itakayofanyika Aprili 15 na kama itabidi kura irudiwe kwa mujibu wa sheria iliyotajwa, kura itarudiwa Juni au Julai, 2015 muda ambao Bunge la Jamhuri la Muungano linatakiwa livunjwe kwa ajili ya uchaguzi mkuu.”

Alisema ili Katiba Mpya itumike katika uchaguzi mkuu unaokuja itabidi uhai wa Bunge na Serikali uongezwe zaidi ya mwaka 2015 jambo ambalo hawaliungi mkono.

Aidha, alisema katika kikao hicho na Rais walikubaliana Bunge Maalum la Katiba liendelee hadi litakapounda Katiba itakayopendekezwa Oktoba 4, mwaka huu.

“Bunge Maalum la Katiba kwa sasa linafanyakazi kwa mujibu wa tangazo la serikali namba 254 lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete, Agosti Mosi, 2014 tangazo hilo litatumika hadi Oktoba 4, 2014 ambapo Katiba inayopendekezwa inategemea kupatikana.” Alisema.

Hata hivyo, Cheyo alisema baada ya kupatikana Katiba hiyo inayopendekezwa hatua inayofuata ambayo ni kura ya maoni ambayo ilikuwa ifanyike Aprili, mwakani itasitishwa na kusogezwa mbele na kuendelea tena baada ya uchaguzi mkuu Oktoba, mwakani.

“Pamoja na kazi ya msingi inayofanywa na Bunge Maalum la Katiba, mchakato wa Katiba unaoendelea sasa hauwezi kutupa Katiba itakayotumika katika uchaguzi mkuu 2015 kwa kuwa muda hautoshi kukamilisha mchakato na kufanya mabadiliko yatakayohitajika ya sheria, kanuni na taasisi mbalimbali zinazohitajika kwa ajili ya uchaguzi huo,” alisema na kuongeza:

Uamuzi wa kikao hicho, unakwenda kinyume na ratiba iliyotolewa awali na uongozi wa Bunge Maalum la Katiba kuwa lingemaliza kutengeneza Katiba inayopendekeza Oktoba 31, mwaka huu.

UCHAGUZI WA MITAA
Cheyo alisema katika kikao hicho pia walikubaliana matayarisho kwa ajili ya uchaguzi wa vijiji, vitongoji na mitaa yaanze haraka iwezekanavyo kwa serikali kuchukua hatua za kisheria ili uchaguzi ufanyike mapema mwakani.


UCHAGUZI MKUU
Aidha, mwenyekiti huyo wa TCD, alisema katika kikao chao na Rais Kikwete walikubaliana kuwa uchaguzi mkuu wa 2015 ufanyike kwa kutumia Katiba ya mwaka 1977.


Hata hivyo, alisema wamekubaliana kufanyia mabadiliko mambo matano katika Katiba hiyo pamoja na sheria ya uchaguzi itakayowezesha nchi kufanya uchaguzi wa huru na haki.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi kusimamia Uchaguzi, Mshindi wa uchaguzi wa Rais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50, matokeo ya uchaguzi wa Rais yaweze kupingwa Mahakamani na kuruhusu mgombea binafsi.

Nyingine ni vyama vya siasa ambavyo vinapenda kupendekeza mambo mengine ya kurekebisha katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 vinaombwa kufanya hivyo mapema kwa kuwa muda uliopo wa kufanya mabadiliko ni mdogo.

Kwa maana hiyo kura ya maoni itapigwa mwaka 2016 baada ya mchakato wa kuunda serikali mpya mwishoni mwa mwaka 2015 au mwanzoni mwa mwaka 2016.

Alisema TCD kupitia vikao vyake itaratibu, itajadili mapendekezo hayo na kuyapeleka serikalini kwa hatua nyingine kabla ya mapendekezo hayo kujadiliwa katika Bunge la Jamhuri la Muungano la Novemba, 2014 na kama itachelewa Bunge la Februari, 2015.

Kuhusu wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliojitoa katika mchakato wa kutunga Katiba Mpya, Cheyo alisema uamuzi huo ni wa Ukawa binafsi hawezi kuwazungumzia.

“Unasababu zao za kutoingia Bungeni, tuheshimu maamuzi yao ila tumekubaliana kuendesha nchi hii katika njia za amani na kuweka mbele mambo ya msingi ya taifa letu,” alisema.

MBATIA ANENA
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amesisitiza wajumbe wa Bunge la Katiba (BMK) wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wataendelea hawataingia Bungeni licha ya kufikia makubaliano na Rais Jakaya Kikwete.


Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Mbatia, alisema makubaliano hayo kamwe hayafanyi uhalali wa kuendelea kwa Bunge hilo, hivyo hawatarejea bungeni hapo.

Alisema jambo la msingi waliloafikiana na Rais Kikwete, kwamba Bunge hilo liahirishwe ili kupisha uchaguzi mkuu, ni wajibu Mwenyekiti wa Bunge hilo kutumia busara zaidi kusitisha kuliko kuendelea hadi Oktoba 4 kama tangazo la serikali linavyotaka.

“Katika mazungumzo yetu hatukusema tunakubaliana na mwenendo wa Bunge, tuliweka wazi kwamba hatukubaliani nao, hivyo liahirishwe hadi tutakapomaliza uchaguzi mkuu turudi kwenye mchakato huo,” alisema Mbatia.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment