HOJA YA UKAGUZI WA RUZUKU ZA VYAMA VYA SIASA YALETA UTATA.

*CUF Wasema hata ikiwaita hawatakwenda kuhojiwa.
*Chadema, NCCR-Mageuzi wapigilia msumari.

HOJA ya ukaguzi wa ruzuku za vyama vya siasa iliyoibuliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto, imeendelea kuvivuruga vyama vya siasa.
Baadhi ya vyama vilivyotajwa na kamati hiyo vikidaiwa kushindwa kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa ruzuku kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, vimetoa misimamo yao inayoonyesha kutokukubaliana na kauli ya Zitto.

CUF kwa upande wake, kimetishia kwenda mahakamani endapo msajili ataamua kusimamisha ruzuku kama alivyoagizwa na Zitto kwa kile walichosema kuwa hakuna sababu za msingi chama chao kutopewa fedha hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro, alisema hawana wasiwasi na hesabu zao na kama msajili ataamua kuisimamisha, watakwenda mahakamani.

Alisema msajili wa vyama vya siasa hawezi kufuta ruzuku ya chama chao wakati wanao ushahidi wa nyaraka zinazothibitisha ofisi yake ilipokea hesabu zao zilizokaguliwa.

Mtatiro alisema kuwa, hesabu ambazo wao hawajapeleka kwa msajili ni za mwaka 2012/2013 na si miaka minne kama Zitto alivyosema. Kutokana na hali hiyo, alisema kuna uwezekano msajili aliyemaliza muda wake hawakukabidhiana baadhi ya nyaraka ndiyo maana inasemekana ukaguzi wa hesabu zao hauko vizuri.

“Sisi hatufanyi kazi na Kamati ya Zitto isipokuwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ndiye anapaswa kuhojiwa kama kuna upungufu katika jambo lolote,” alisema Mtatiro.

Kiongozi huyo wa CUF alisema kwamba, awali walikuwa wakifanya ukaguzi wao wa ndani na kupeleka hesabu kwa msajili, lakini mabadiliko yaliyowataka kumlipa mkaguzi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ndiyo yaliyowatia shaka.

Pamoja na hayo, alisema chama chake hakitakwenda mbele ya Kamati ya Zitto kujieleza, kwani hakiwajibiki kwao.

“CUF si Serikali, si utaratibu wala sheria kwa vyama vya siasa kutafuta mkaguzi wake binafsi, mtu hawezi kujikagua mwenyewe badala yake tutasababisha mgongano wa kimaslahi, hii ni aibu kwa Serikali kutokuwa na wakaguzi.

“Ingawa tunatambua Kamati ya Bunge ina uwezo wa kumwita mtu yeyote, tunasema hatutakwenda kwenye kamati hiyo japokuwa hatujapata wito rasmi na tunamtaka Zitto aache kutuchafua kwenye mitandao ya kijamii,” alisema Mtatiro.

Chadema wanena

Kwa upande wake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kipo tayari kuhojiwa na Kamati ya PAC kama watapelekewa wito rasmi.

Mkurugenzi wa Fedha wa chama hicho, Anthony Komu, aliliambia RAI Jumatatu, kwamba wako tayari kwenda mbele ya PAC kwa sababu wana uhakika na hesabu zao.

Alisema Kamati ya Bunge ni chombo kinachoheshimika, hivyo watatoa ushirikiano unaohitajika ingawa vyama vya siasa haviwajibiki kwa kamati hiyo.

Alisema, hesabu zao za mwaka 2009, 2010, 2011, zilishawasilishwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na walipatiwa barua ya kuonyesha amepokea nyaraka zao.

Alisema, hesabu za mwaka 2012/2013, hazikupelekwa kwa sababu ya mkanganyiko uliojitokeza wa kuvitaka vyama vitenge fedha za kumlipa mkaguzi.

Alisema kutokana na mkanganyiko huo, Serikali yenyewe kupitia kwa msajili na CAG, ndiyo wanapaswa kulaumiwa kwa sababu wamevunja sheria.

“Sisi tunafanya kazi na msajili wa vyama vya siasa, kwa hiyo, Kamati ya Bunge inapaswa kutuambia nani amesababisha haya, kama PAC inasema hesabu hazikukaguliwa, je kosa ni la nani?” Alihoji Komu.

NCCR Mageuzi

Kwa upande wake, Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR Mageuzi), Moses Machali ambaye ndiye msemaji wa chama hicho, alisema hapingi vyama kwenda kuhojiwa na Kamati ya PAC.

Alisema katika jambo hili, siyo sahihi kuvibana vyama vya siasa peke yake bali udhaifu ulioonyeshwa na ofisi ya CAG pamoja na msajili wa vyama vya siasa nao uangaliwe.

Machali ambaye alisema msimamo huo ni wa kwake binafsi, alisema CAG hapaswi kutoa mwaliko pale anapotaka kufanya ukaguzi kwa taasisi yoyote na kilichofanywa ni uvunjifu wa sheria.

“Huu utaratibu wa kuvitaka vyama vijikague vyenyewe ni udhaifu, inawezekana anaogopa baadhi ya vyama, hakuna sheria inayosema kutakuwa na bajeti maalumu ya CAG kukagua vyama vya siasa, kwani Bunge linapotenga bajeti ya CAG huwa ni kwa ajili ya kukagua fedha zote za umma, kitendo cha kushindwa kukagua fedha za vyama kina walakini ndani yake,” alisema Machali.

Kauli ya Nape

Wiki iliyopita, ikiwa ni siku moja baada ya taarifa ya Zitto, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema hesabu zao ziko vizuri kwa kuwa hukaguliwa kila mwaka.

RAI 
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment