WIZARA YA ELIMU YAKANUSHA KUONDOA MASOMO YA DINI, KIARABU KATIKA MITIHANI YA TAIFA.

baraza-la-wawakilishi1
NA Faki Mjaka-MAELEZO ZANZIBAR
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema Masomo ya Dini,Kiarabu na Masomo mengine hajafutwa na yataendelea kusomeshwa na kufanyiwa Mitihani katika ngazi zote kama ilivyokuwa hapo awali.

Aidha imesema Wizara hiyo haijakubaliana na Waraka wa Elimu kutoka Tanzania Bara wa kuyafanya Masomo hayo kuwa ya hiari na hivyo yasichangie asilimia yoyote katika ufaulu wa Mtahiniwa.
Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Zanzibar Abdallah Mzee ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari kwa lengo la kukanusha Taarifa zilizotolewa na baadhi ya Vyombo vya habari zilizodai kuwa Wizara hiyo imeondoa Mtaala wa Masomo ya Dini na Kiarabu kwenye Mitihani ya Taifa.
Amefahamisha kuwa Watendaji kutoka Wizara ya Elimu Tanzania Bara walikutana na Wenzao kutoka Zanzibar kwa lengo la kujadili Waraka wa Elimu waliokuja nao uliokuwa unataka kufanyike mambo mapya.
Mzee amebainisha kuwa katika Waraka huo Wenzao kutoka Bara walipendekeza kuwa Masomo ya Dini ya Kiislam, Dini ya Kikristo,Lugha ya Kiarabu,Kifaransa, Komputa, Mziki yawe ya Hiari kwa Mwanafunzi kuyasoma lakini pia yasisaidie ufaulu wowote katika viwango vya Madaraja ya Ufaulu.
“Waraka ulipendekeza Masomo hayo yakiwemo Dini na Kiarabu kuwa Optional na wala yasisaidie chochote katika kupandisha au kushusha Division ya Mtahiniwa” Alifafanua Mzee.
Aidha ilipendekezwa kuwa Utaratibu huo mpya uanzwe kufanyiwa kazi kwa Wanafunzi watakaoingia Kidato cha Kwanza mwakani ili ifikapo mwaka 2017 wanafunzi hao wautumie katika kidato cha nne.
Hata hivyo Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kuwa Watendaji wa Zanzibar waliupinga utaratibu huo kwa vile haukidhi matakwa ya Zanzibar.
“Watendaji wetu Waliupinga Waraka huo kwani hautufai na unatofautiana sana na Sisi kulingana na hoja zetu tulizotoa,lakini pia walikubali kuurudisha ili usiweze kufanyiwa kazi ” alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.
Alisema kwa Zanzibar, Wizara ya Elimu inatoa Mchepuo wa Masomo ya Lugha katika Skuli tofauti ikiwemo Sekondari ya Kiponda hivyo itakuwa vigumu kufuata utaratibu huo.
Kuhusu Somo la Dini Mzee amesema Somo hilo kwa Zanzibar ni muhimu sana na nimiongoni mwa masomo yenye Walimu Wazuri wa ngazi za Stashahada hadi Udaktari-PHD ambapo ufundishwaji wake huanzia darasa la kwanza hadi Chuo Kikuu hivyo kubadili utaratibu isingewezekana.
Aidha amefahamisha kuwa katika dunia ya sasa Somo kama Komputa ni muhimu sana hivyo kulifanya halina ulazima ni kujirudisha nyuma kimaendeleo.
Amesema licha ya mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Wizara kwa upande wa Zanzibar na Bara lakini Wao hawakushirikishwa katika Uanzishwaji wa Waraka huo.
Katika hali ya kuliweka sawa jambo hilo Mawaziri wa Wizara hizo Ali Juma Shamhuna na Mwenzake wa Bara Shukuru Kawambwa wanatarajia kukutana kesho kulijadili jambo hilo.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment