Msigwa akerwa majibu mepesi ya serikali!!


MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA), ameshangazwa na majibu mepesi ya serikali juu ya kulipwa staili zao wafanyakazi wa Kiwanda cha TAN-CUT-Almasi cha mjini Iringa kichofungwa na serikali mwaka 1988.
Msigwa alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akiuliza swali la msingi.
“Serikali ina kumbukumbu zote za wafanyakazi waliokuwa katika kiwanda hicho ni kwanini isilete kumbukumbu hizo ili wafanyakazi hao walipwe haki zao kwa kulitumikia taifa badala ya kutoa majibu yanayowadhalilisha?” alihoji Msigwa.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Rita Kabati, alitaka kujua kauli ya serikali juu ya kuwalipa wafanyakazi hao na ni lini itawalipa.
“Mwaka 1988 serikali ilikifunga kilichokuwa Kiwanda cha Almasi-Iringa, lakini waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho hawajalipwa mafao yao hadi leo. Je, serikali inatoa kauli gani?” alihoji Kabati.
Akijibu swali la Mchungaji Msigwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Mary Nagu, alisema serikali inalichukua suala hilo na kulifanyia kazi, ili wafanyakazi hao waweze kulipwa haki zao.
Awali akijibu swali la Kabati, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema Kampuni ya kukata na kuchonga almasi-Tanzania ‘Diamond-Cutting Company’, ijulikanayo kwa kifupi TAN-CUT-Almasi, ilianzishwa ili kuiongezea thamani almasi iliyokuwa ikichimbwa Mwadui ili isiendelee kuuzwa ikiwa ghafi.
Alisema wafanyakazi wa  kampuni hiyo kama ilivyokuwa kwa watumishi wa mashirika ya umma hawakuwa watumishi wa serikali bali wa kampuni husika.
Alisema uamuzi wa serikali kulipa mafao ya watumishi wa mashirika ya umma ulichukuliwa wakati wa sera ya kurekebisha mashirika ya umma miaka ya 2000 baada ya makubaliano baina ya wafanyakazi, serikali na malipo ya watumishi.
Aidha, alisema malipo hayo hayakutokana na bajeti ya serikali, bali mapato yalitokana na kuuza mashirika ambayo yalisimamiwa na Tume ya Rais ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma (PSRC).
Alisema Kampuni ya TAN-CUT-Almasi ilifungwa zaidi ya miaka 10 kabla ya zoezi la urekebishaji wa mashirika ya umma kuanza na kwa kuwa watumishi wake hawakuwa waajiriwa wa serikali, serikali haiwajibiki kulipa mafao ya watumishi hao.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment