
Marehemu Tabu Ley Rochereau wa Congo
Tabu Ley Rochereau, mwanamuziki 
maarufu na mwanzilishi wa mtindo wa rumba wa soukous akijulikana 
kama"Mfalme wa Rumba la Congo" ambaye alikuwa mmoja wa wanamuziki 
waliopendwa barani Afrika, amefariki Jumamosi katika hospitali moja 
mjini Brussels, Ubelgiji.
Mwanamuziki huyo akiitwa Pascal-Emmanuel 
Sinamoyi Tabu alizaliwa wakati wa utawala wa Wabelgiji nchini Congo 
mwaka 1937 au 1940, kutegemea na vyanzo vya habari, alikuwa akiumwa 
tangu mwaka 2008 akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi. Kiongozi wa bendi 
ya Orchestre Afrisa International alikuwa ni kiongozi mbunifu ambaye 
uimbaji wake uliunganisha sauti za muziki wa Kiafrika, Cuba,na mirindimo
 ya Caribbean, na aliimba bila kuchoka na kubandikwa jina la "Sauti ya 
Mwangaza."
Muziki wa Tabu Ley unapatikana 
katika mamia ya santuri za LP. Miongoni mwa santuri hizo ni ile ya Ley, 
Ley, Seigneur Ley Rochereau. Pia kwa weledi mkubwa kazi zake 
zimekusanywa katika CD.
Mwanamuziki Tabu Ley ambaye alikuja kushirikiana
 kimuziki na hata kimapenzi na mwanamuziki wa kike kutoka huko Jamhuri 
ya Kidemokrasi ya Congo Mbilia Bel, alitikisa anga ya muziki wa rumba 
duniani, na hususan eneo la Afrika Mashariki na Kati.
Kwa mfano mwaka 1987 alifanya ziara nchini 
Tanzania, wakiwa na Mbilia Bel na kutembelea mikoa kadha, ikiwa ni 
kusherehekea miaka kumi ya kuzaliwa kwa chama tawala cha CCM, nchini 
Tanzania.
Miongoni mwa vibao vilivyompa umaarufu mkubwa 
Tabu Ley ni Muzina, Maze, C'est comme ca la vie, selikutu, Ibeba, Nadina
 na nyingine nyingi.
Wapenzi wa muziki wa rumba, watamkosa Tabu Ley, 
lakini wataendelea kuburudika na nyimbo zake ambazo alizitunga katika 
uhai wake, akiwa mwanamuziki.
Written by:BBC
POSTED BY:www.info@dirayetu.blogspot.com 
0 comments:
Post a Comment