VIKUMBO UENYEKITI BUNGE LA KATIBA!!

Vigogo watajwa,kuchaguliwa kesho
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.

Mchuano wa kumpata Mweyekiti wa Bunge Maalum la Katiba linalotarajiwa kuanza kesho umepamba moto, huku baadhi ya vigogo wakitajwa kupigana vikumbo kuipata nafasi hiyo.
Mpambano huo unadaiwa pia kuyahusisha makundi yanayotajwa kusaka urais wa mwaka 2015 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tayari kuna taarifa zinazowataja Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na Spika wa Baraza la Wawakishi Zanzibar, Amir Pandu Kificho, kuingia katika kinyang’anyiro hicho.


Zipo taarifa pia kwamba Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, kutokana na nafasi aliyonayo kama mkuu wa mhimili wa Bunge anaweza kuchaguliwa kushika nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba iwapo atashawishiwa na kukubali kugombea.

Kikao cha Bunge hilo kitaanza kesho kikijumuisha wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete.

Taarifa ambazo NIPASHE imezipata jana kutoka mjini Dodoma zimeeleza kuwa, mchuano huo unaweza kuwa mgumu kwa sababu baadhi ya wanachama wa CCM ambao wana mpango wa kugombea urais 2015 wamejipanga kuweka watu wao wagombee nafasi hiyo.

Taarifa zaidi kutoka Dodoma zimebainisha kuwa wapambe wa Sitta, Chenge, Makinda na Kificho wameshaanza kupigana vikumbo kwa kufanya kampeni za chini kwa chini ingawa wahusika wenyewe bado hawajaweka wazi kama watagombea nafasi hiyo.

Baadhi ya wajumbe na wabunge wa Bunge hilo waliozungumza na NIPASHE walisema mchuano huo utakuwa mgumu sana hasa kutokana na wagombea wanaotajwa wakitoka ndani ya chama tawala ambao pia wana makundi yao ya urais wa 2015.

Kikao cha kwanza cha mkutano huo kitafanyika kesho pamoja na masuala mengine, kitahusisha uchaguzi wa mwenyekiti wa muda atakayesimamia upitishwaji wa kanuni na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge hilo.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Peter Kuga Mziray, alipoulizwa kama vyama vya upinzani vimeweka mkakati wowote wa kumpata Menyekiti wa Bunge hilo, alisema hakuna mkakati wowote uliowekwa.

Mziray ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha APPT Maendeleo, alisema mashaka yaliyopo ni kwamba makundi ya urais wa 2015 yaliopo ndani ya CCM ni lazima yanaweza kujipenyeza katika mchuano wa nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba.

“Kimsingi hakuna mkakati wowote uliowekwa na wapinzami katika kuwania nafasi hiyo, ninachokiona ni kwamba wagombea urais wanaweza kujipenyeza katika suala hili,” alisema.

Chenge alipoulizwa na NIPASHE kwa simu kama ana mpango wa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, alikata simu bila kujibu lolote dakika chache tu baada ya kuulizwa swali hilo.

Kwa upande wake Sitta alipotafutwa, simu yake ilipokelewa na msaidizi wake ambaye alisema kuwa yupo kwenye kikao.

Hata hivyo, haikufahamika Sitta alikuwa anahudhuria kikao gani, lakini jana Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM ilikuwa ikikutana mjini Dodoma. Sitta ni mjumbe wa kikao hicho

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Kificho alipotafutwa mara kadhaa hakupatikana katika simu yake.

ATAKAVYOPATIKANA
Utaratibu wa kuwapata Mwenyekiti na Makamu wake wa Bunge la Katiba umetangazwa.

Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kushirikiana na Ofisi ya Baraza la Wawakilishi zilitangaza jana kuwa, mkutano wa bunge hilo utaanza kesho kwa kumchagua mwenyekiti wa muda ambaye atasimamia kuandaa na kupitishwa kwa Kanuni za Bunge Maalum.

Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Bunge la Muungano, Dk. Thomas Kashililah alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.

Dk. Kashililah alisema mwenyekiti huyo wa muda baada ya kuchaguliwa atasimamia na kuongoza Bunge Maalum katika kusimamia uandaaji na upitishwaji wa kanuni za Bunge hilo.

Aliongeza kuwa mwenyekiti huyo wa muda kesho hiyo hiyo ataendesha uchaguzi wa Mwenyekiti na makamu wake kwa mujibu wa kifungu cha 22(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

“Mwenyekiti wa muda atachaguliwa kwa taratibu zilizowekwa na Katibu wa Bunge la Jamhuri na Katibu wa Baraza la Wawakilishi hayo ni masharti na sheria ya kifungu cha 22A(1) cha Mabadiliko ya Katiba kinatupa nguvu ya kuandaa na kutafuta namna ya kumpata mwenyekiti wa muda,” alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na sheria inavyosema, baada ya mwenyekiti na makamu wake kupatikana na Katibu na Naibu wake watapatikana.

“Kwa sababu sheria imeainisha kwamba mwenyekiti akitoka upande mmoja wa Muungano basi Katibu anatoka upande wa pili wa Muungano...na makamu vile vile..kwa hiyo sasa hivi hatuna Makatibu wa Bunge hili, sasa hivi tuna Katibu wa Baraza la Wawakilishi na Katibu wa Bunge tunasimamia mchakato wa mwanzo wa kuhakikisha kwamba Bunge hili linaanza, lina kanuni na miundo yote inayotakiwa,” alisema.

Aidha, alisema Mwenyekiti akishachaguliwa hataapishwa kwanza hadi hapo Katibu na Naibu wake watakapokwenda kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

“Baada ya hapo ndiyo sasa shughuli rasmi za Bunge maalum zitakapoanza...kwani Katibu atakapoapishwa naye atakuja kumuapisha mwenyekiti na makamu wake...na mwenyekiti atawaapisha wajumbe wote wa Bunge hilo,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment