NIONAVYO MIMI: AZAM FC HAIWAPENDI WATANZANIA!!





Siwezi kushangaa siku moja nikiamka asubuhi na kusikia taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa, wamiliki wa timu ya Azam wameamua kununua Ndege yao kwa lengo la kurahisisha Usafiri wa kwenda mikoani kucheza michezo yao ya ligi kuu na ile ya barani Afrika ambayo timu hiyo imekuwa ikishiriki kwa msimu wa pili sasa mfululizo. Kila nchi duniani ina tamaduni zake na moja ya tamaduni za kitanzania ni kushirikiana kwenye matukio muhimu ya kijamii.
 
Watanzania pamoja na tofauti zao za dini, kabila, kipato daima wamekuwa pamoja kwenye mambo ya kijamii kama vile misiba.harusi n.k Hata kama utakuwa na pesa kiasi gani, kama huna tabia ya kushiriki na wenzako kwenye mambo ya kijamii, siku yakikukuta utaona cha mtema kuni! Hii inatuonyesha kuwa ushiriki na mahusiano mazuri kwenye jamii yako ni muhimu kuliko vikapu vya pesa ulizonazo.

Klabu ya Azam ilianzishwa mwaka 2007 na kufanikiwa kucheza ligi kuu msimu wa 2008/2009 kwa mara ya kwanza na kumaliza kwenye nafasi ya 8. Msimu wa 2009/2010 ilifanikiwa kumaliza kwenye nafasi ya 3 huku wakiweka histori ya kumnunua mshambuluaji wa klabu ya Yanga Mrisho Ngassa kwa mamilioni ya pesa za Kitanzania. Azam waliweza kumsajili kiungo wa Rwanda marehemu Patrick Mafisango, Kally Ongala, Jabir Azizi, Ramadhani Chombo Redondo na mastaa kibao na hapa ndipo walipoanza kuteka taratibu hisia za watanzania kama timu itakayoleta mapinduzi ya soka nchini.

Watanzania baada ya kuona timu ya Azam inakuja na mbinu ambazo zinaendana na soka la kisasa, wengi wakaamini kuwa hii ndiyo timu ya kuishabikia. Azam wamejenga uwanja wao, wana timu bora ya vijana, wana hosteli za wachezaji wao na mambo mengi mazuri lakini, hawana mashabiki! Hata wale wachache ambao huwa wanaonekana timu hiyo ikicheza wanapiga piga ngoma ni kama mashabiki bandia tu.Tayari Azam wamefanikiwa mara 2 mfululizo kucheza mashindano ya kombe la shirikisho barani Afrika, kwa timu iliyoanzishwa mwaka 2007 haya ni mafanikio.

Watanzania wengi sana wanaipenda timu ya Azam lakini, wanashindwa kujiweka wazi kutokana na namna timu hiyo inavyoendeshwa.Uendeshwaji wa Azam fc haujampa nafasi mwananchi kushiriki na hii inatokana na timu hiyo kujiweza kifedha. Azam wanasahau kuwa timu tajiri kama Real Madrid, Barcelona, Bayern Munich, Manchester United na nyingine kibao, mafanikio yao yamechangiwa zaidi na mashabiki lukuki wanaonunua bidhaa za timu hizo na kuingia uwanjani kila mwishoni mwa wiki.

Shabiki duniani kote ni mchezaji wa 12 na ndiyo maana klabu kama ya Bayern Munich ya nchini Ujerumani hairuhusu mchezaji wake yoyote kuitumia jezi namba 12 kwa sababu wanaamini jezi hiyo inavaliwa na washabiki wao wanaokuja kuitazama timu kwenye kila mechi wanayocheza. Azam FC ni lazima wawape nafasi mashabiki ya kuwa sehemu ya timu yao, kuna uwezekano wakafanya kila kitu ila kukosa mashabiki, itaendelea kuwagharimu kila siku. Kwa kutumia kigezo cha mapato ya mlangoni tu, unaweza kugundua kuwa huenda klabu Yanga ndiyo inaongoza kwa idadi kubwa ya mashabiki huku ikifuatiwa na klabu ya Simba kwa karibu sana. Mbeya city wanaweza kuwa nafasi ya 3 na Coastal Union kushika nafasi ya 4. Azam fc hamjifunzi tu?

Klabu za Simba na Yanga hapa nchini,zinamashabiki wengi sana na hali hii inatokana na sababu nyingi,chache kati ya hizo ni ukongwe wa vilabu hivyo na mafanikio makubwa waliyoyapata kwenye ligi kuu nchini na mashindano mbalimbali ya Afrika Mashariki na kati.Ingawa timu za Coastal Union toka jiji la Tanga,Tukuyu Stars toka jiji la Mbeya na Mtibwa sugar toka Morogoro nazo kwa nyakati tofauti zimewahi kutwaa Ubingwa wa ligi kuu lakini ni wazi kuwa,Simba na Yanga ndo watawala wa ligi hiyo.

Ni ukweli uliowazi kuwa vilabu vya simba na yanga ukichunguza namna vinavyoendeshwa utagundua kuwa ni kama miradi ya watu binafsi ambao wanatumia wafuasi lukuki wa timu hizo kujiongezea kipato.Wachezaji wengi wanaonunuliwa kwa bei kubwa hasa wale wanaotoka nje ya nchi,wanaletwa kwa pesa za watu binafsi,wanapewa magari,nyumba na mishahara yao kutoka mifukoni mwa watu wanaoziongoza klabu hizo.

Watanzania wa leo si sawa na wale wa mwaka 47,siku klabu ya Pamba ya Mwanza au Ujenzi ya Rukwa zitakapopanda daraja na kushiriki ligi kuu,itakuwa ni sawa na ujio mpya wa Mbeya City. Kutokana na Propaganda za kila siku ndani ya klabu za Simba na Yanga, watu wamechoka na wanachosubiri ni kuja kwa timu ambayo wataamini imekuja kuleta mabadiliko ya kweli kama unavyoona watu wa Mbeya na timu yao. Azam Fc wanatakiwa kujifunza faida ya mashabiki na kubadilisha mwelekeo wao na kama wataendelea na tabia yao ya kuamini kuwa pesa ndo kila kitu, kuna uwezekano watakuja kuzidiwa mashabiki hata na timu ya Lipuli fc kutoka Iringa.

Kuna timu nyingi tu duniani zinazomilikiwa na watu binafsi kama ilivyo kwa Azam FC, Chelsea inamilikiwa na Roman Abramovic, Manchester City inamilikiwa na Sheikh Mansour, AC Millan inamilikiwa na Silvio Berlusconi na nyingine kibao.Sio Azam FC tu inayotumia watoto wa mmiliki kuwa sehemu ya bodi ya timu hiyo hata AC Millan pia inamtumia Barbara Berlusconi binti wa mmiliki wa klabu hiyo kama sehemu ya wakurugenzi wake lakini, bado mashabiki wamepewa kipaumbele cha juu achilia fedha walizonazo wamiliki wa klabu hiyo.

Kitu kikubwa kinachowasumbua Azam FC ni kutaka kupambana na klabu za Simba na Yanga ndani ya jiji la Dar es Salaam na kusahau kuwa,Tanzania ina mikoa zaidi ya 25 kwa sasa.Azam FC ni wageni kwenye viwanja vyote vya ligi kuu Tanzania hadi kwenye uwanja wao wenyewe wa Azam Complex pale Chamazi jiji Dar es Salaam na hili lilijidhihirisha kwenye mchezo wao dhidi ya Mbeya City kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi kuu Tanzania bara ambapo karibu maelfu ya wakazi wa Mbeya walivamia kiwanja cha Azam Complex.

Timu ya Mbeya City imejenga tabia ya kutembelea wagonjwa waliolazwa Hospitalini wakiwa mbeya na nje ya mkoa huu kwenda kuwajulia hali na kuwapa mkono wa pole.Hii kitu unaweza usiielewe kwa haraka lakini,inatengeneza mahusiano mazuri sana kati ya timu na wananchi.Azam FC mnaweza kufanya kitu kingine hata kujichanganya na watoto wa shule mikoani.Hii inaweza kuondoa taswila iliyopo sasa kuwa Azam haijichanganyi,wamejitosheleza n.k Watanzania wanawahitaji,wapeni nafasi kwenye timu yenu.
 
na shafii dauda.com
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment