Mamia ya wananchi wenye hasira katika
Kijiji cha Bashay kilichoko wilayani hapa wamepambana na polisi kwa
kuwarushia mawe kwa kile walichodai kuishinikiza Serikali kuweka matuta
katika Barabara ya Karatu hadi Ngorongoro.
Tukio hilo lililotokea saa 4 asubuhi baada ya
watoto wawili Priska John(5) na Happiness Filbert (5) walipogongwa na
gari wakati wakivuka barabara ambapo mmoja alifariki dunia papo hapo
huku Priska akikimbizwa hospitali.
Wananchi hao walifikia uamuzi huo wa kufunga
barabara na kuzuia magari yakiwamo ya watalii kwa nia ya washinikiza
mkuu wa wilaya kwenda kuwasikiliza na ndipo polisi walipojaribu kuondoa
mawe hayo bila mafanikio.
“Tumechoka kuwaona polisi wakiokota maiti za
watoto wetu barabarani kama wanaokota mizoga ya mbwa na leo(jana)
tunawapiga mawe mpaka wakitumwa tena kuja kuchukua maiti ya aliyegongwa
na gari wakatae,”alisikika mama mmoja akipaza sauti kwa uchungu.
Vurugu kati ya wananchi na polisi zilianza huku
wananchi wakiporomosha mawe pasipo kujali wanarushia polisi au magari
yaliyokuwa yakipita huku polisi walipambana kwa kurusha mabomu ya
machozi kwa takribani saa mbili.
Hata hivyo katika vurugu hizo hakuna aliyeripotiwa
kuumia huku wananchi wakiitupia lawama Serikali kwa kushindwa kuweka
matuta katika barabara hiyo ambapo mara kwa mara ajali zimekuwa
zikiripotiwa kutokea katika Barabara ya Karatu hadi Ngorongoro.
Akizungumzia tukio hilo Mtendaji wa Kijiji cha
Bashay, Joseph Surumbu alikiri kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema,
ajali katika eneo hilo zimekuwa zikitokea mara kwa mara huku akiitupia
lawama Seriklai kwa kushindwa kuweka matuta katika eneo hilo.
Hili ni tukio la pili kutokea kwa kipindi cha
miezi mitatu kwa wananchi kupambana na polisi baada ya watoto kugongwa
wakishinikiza barababa hiyo kuwekwa matuta.
Daktari kiongozi wa Hospitali Teule ya Wilaya,
Daniel Simpa alithibitisha kuupokea mwili wa mtoto Happiness Filbert
huku mwenzie akiwa amejeruhiwa na anaendelea na matibabu.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
POSTED BY:www.info@dirayetu.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment