KUTOLEWA
hadharani kwa Hati ya Muungano, kumeanza kuwachanganya baadhi ya wajumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa).
Hali hiyo
imejitokeza wakati baadhi ya wajumbe wa Ukawa walipozungumza na gazeti
hili kuhusu hatua ya Serikali kuweka hadharani hati hiyo juzi.
Akizungumzia
hatua hiyo ya Serikali, Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe alijikuta
akianza kumlinda mjumbe mwenzake maarufu, Tundu Lissu, kwamba alisema
hati hiyo haipo kutokana na mazingira.
Alidai kuwa
mazingira hayo yanatokana na baadhi ya Tume na viongozi wa Serikali
kudai kuiona hati hiyo bila mafanikio, huku akidai bado watatafuta hoja
ya kutaka kuhakiki uhalali wake.
Lakini
wakati Mbowe akitoa hoja hiyo, Mjumbe Ismail Jussa Ladhu, aliishukuru
Serikali kwa kuitoa hadharani hati hiyo na kusema Serikali imetambua
umuhimu wa matakwa ya Ukawa.
Wajumbe hao
wa Ukawa, walitumia muda mrefu katika Bunge hilo hilo kupotosha umma
kuwa hati hizo hazipo, na walipopewa sheria ya kuridhia Muungano, nayo
wakaipinga wakidai imechakachuliwa.
Msingi wa
kudai haki hiyo huku wakipotosha kuwa haipo, ulikuwa kujenga hoja ya
kubatilisha Muungano uliodumu kwa miaka 50 na kuipa nguvu hoja ya muundo
wa serikali tatu.
Kutokana na
upotoshwaji huo, Rais Jakaya Kikwete aliridhia hati hizo zioneshwe
hadharani na nakala zilizothibitishwa kisheria zipelekwe bungeni kuondoa
upotoshwaji huo na kuwekwa katika Makumbusho ya Taifa, kwa ajili ya
wananchi kujionea.
Kuoneshwa
Juzi Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ilipokuwa akionesha hati hiyo,
alisema hati hiyo ipo, ilikuwepo siku zote na kufafanua kuwa ni lazima
baadhi ya hati muhimu zihifadhiwe kama mboni ya jicho.
“Lazima
tukubaliane kuwa zipo hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama
Taifa huru, Jamhuri huru na Muungano huru, ambazo tunazihifadhi kama
mboni ya jicho. “Hati hizo ni pamoja na Hati ya Uhuru wa Tanganyika ya
mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962, na Hati ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964. “Hati za aina hii
zinahifadhiwa maeneo maalumu ambayo ni salama ili zisipotee wala
kuharibika. Kwa kawaida hatuzitoi, tunazihifadhi kwa namna yoyote ile,”
alisema Balozi Sefue.
Mjadala ufungwe
Wakizungumza
jana na gazeti hili katika Viwanja vya Bunge, mjini hapa kuhusu
kupatikana na kutolewa kwa hati hiyo, baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo
walisema kwa nyakati tofauti kuwa, mjadala kuhusu kuwepo ama kutokuwepo
kwa Hati ya Muungano unapaswa kufungwa sasa.
“Kimsingi
hati kuwepo ama kutokuwepo haikuwa hoja ya msingi, hata ikiwa
zimepatikana, wapo watakaokuja na jipya, wapo watu wanataka kukwamisha
Muungano, wanahoji hati leo wakati waliapa kutii Jamuhuri ya Muungano,
Muungano upi wasioutambua walipoapa? “Ni sawa na mtoto kuhoji ndoa ya
baba na mama si halali ilifungwa na Mzungu ama Mwafrika, si sawa,”
alisema Mjumbe wa Bunge hilo, Charles Mwijage.
Mjumbe
mwingine, Ali Keissy alisema mjadala kuhusu hati haupaswi kuendelea
kupoteza muda, unatakiwa kufungwa na kutoa fursa kwa wajumbe kuunda
Katiba yenye tija na maslahi ya umma, huku akionya mwendelezo wa mipasho
ndani ya Bunge hilo, ni ukuta mwingine unaozuia kupatikana kwa Katiba
nzuri.(Martha Magessa)
“Katika
jambo la msingi kama hili, watu walidai hati, imefika, suala hili
tulifunge, tusiibue mapya, ila kinachosikitisha zaidi ni mwenendo wa
Bunge hili, ni mipasho na utoto mtupu ndani humo, kwa mwenendo huu,
hakuna Katiba mpya yenye tija, watu wanachambuana mambo binafsi ya
kuolewa, kuoa na kuwa na watoto, hatujatumwa hayo na Watanzania,”
alisema Keissy.
Hati za Pemba, Unguja
Katika hatua
nyingine, Mjumbe, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Waride
Bakari Jabu, alisema Wazanzibari wanaunga mkono muungano wa serikali
mbili na wanaopinga, wengi wao walikwenda Zanzibar kwa mbio za Mwenge.
Alimtaka
Makamu wa Kwanza wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad, kutowalaghai
Watanzania kwamba Wazanzibari hawataki Muungano wakati wanachama wa CUF
ndio wasioutaka. Alisema wapo wachonganishi wa muungano na hao ndio
wanaohoji uhalali wa Muungano wakitaka uvunjike.
“Na sisi
tunataka Hati ya Makubaliano kati ya Unguja na Pemba iletwe hapa
tunataka kuiona, Wanzanzibari wa CUF ndio wanataka kuvunja Muungano,
wanasema Wazanzibari wote hii si kweli,” alisema Jabu.
Hoja ya Mbowe yajibiwa
Naye Mjumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba, Ezekiel Maige, alipokuwa akizungumzia hoja
ya gharama za serikali tatu, alitumia takwimu zilizowasilishwa na Mbowe
kuelezea umuhimu wa serikali mbili.
Alimkariri
Mbowe akielezea kushangazwa na hoja ya gharama katika muundo wa serikali
tatu, wakati asilimia takribani 35 hadi 40 za fedha nchini zinatumika
vibaya kwa mafisadi na masuala mengine yasiyo na tija kwa wananchi.
Maige yeye
alisema kama mianya hiyo ya rushwa na ufisadi itakomeshwa, fedha hizo
zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo na sio kugharimia muundo wa
serikali tatu.
Alipokuwa
akizungumzia faida za Muungano, alisema ni wazi Zanzibar imenufaika,
ingawa pamoja na manufaa hayo yote bado yapo malalamiko kwamba upande
huo unanyonywa.
Alisema
Muungano una faida kwa pande zote na suala la kusema Zanzibar imeonewa
sio kweli kwani hata sasa wilaya zote 10 za Zanzibar zina barabara za
lami na miundombinu yao ni mizuri kuliko wilaya za Bara.
Naye mjumbe
Mwigulu Mchemba, alisema Tanzania Bara imekuwa ikikusanya Sh trilioni
7.7 kwa mwaka na kati ya hizo Sh trilioni nne zimekuwa zikitumika kulipa
mishahara.
Alifafanua
kuwa Sh trilioni tatu zinazobakia, ndizo zimekuwa zikipelekwa
kuwahudumia wananchi katika kutoa elimu, maji, mikopo ya elimu ya juu na
kadhalika.
Alihoji kwa
kuwa rasimu ya Katiba inataka Sh trilioni tatu zitumike kuendesha
serikali ya Shirikisho, fedha za maji, miundombinu, elimu na huduma
zingine zitatoka wapi?
Alisema kama
serikali tatu zitapita, ataongoza kundi la vijana wasio na ajira
kupinga ongezeko la gharama katika utawala na uendeshaji, ili fedha
zaidi zipelekwe katika kuhudumia wananchi waone thamani ya fedha ya kodi
zao.
Mkataba wa CUF
Naye Mjumbe
Panya Ali Abdallah, alielezea kuwashangaa wajumbe wa bunge hilo
wanaotoka Ukawa upande wa Zanzibar, wanaounga mkono hoja ya kuwa na
serikali tatu.
Alisema wajumbe hao wa Zanzibar wamedandia hoja hiyo kwani wameikuta Dodoma na hoja waliyokuja nayo ilikuwa serikali ya Mkataba.
“Hao
wachache kutoka Zanzibar wasiseme Wazanzibari wote hawataki Muungano,
waseme ukweli wao wanataka serikali ya mkataba tena wanaita ”nkataba”
ndio hoja yao toka Zanzibar sasa wamefika hapa wamekuta hoja ya serikali
tatu na wao wanaidandia, si wakweli hao, waseme hiyo yao ya “Nkataba”
mbona hawaisemi?” Alihoji Panya.
“Sisi
tunaamini mapinduzi ya mwaka 1964 na ndio msimamo wetu hatutaki
kurudishwa nyuma kwanza Zanzibar tuna wasiwasi wa kuja tena kwa Sultani,
ila wapo wanaobeza na hatuwashangai kwa sababu hawataki Muungano
wanatafuta njia nyepesi ya kurudi kwa mkoloni”, alisema Panya.
Alisema
awali Wazanzibari waliomba wawe na serikali ya Umoja wa Kitaifa na leo
wameipata, lakini cha ajabu hata serikali hiyo haijamaliza kipindi cha
kwanza cha utawala wanaibuka watu na kutaka kuvunja Muungano huo.
“Tusivunje
Muungano eti kwa kuwa kuna kero za Muungano, hata binadamu tuna kero na
huenda zipo muda mrefu kuliko hata hizo za Muungano, tunaangalia jinsi
ya kuzitatua na tuendelee na muundo wa serikali mbili na sio tatu,”
alisema Panya.
Akisisitiza
hilo alimuomba Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad,
kukaa na wenzake na kukubaliana kuendelea kusimamia amani ya nchi na sio
kuivunja kwani kufanya hivyo ni kuvuruga wananchi.
Akiunga
mkono hoja hiyo, mjumbe kutoka Zanzibar Waridi Bakari Jabu alisema
Muungamo wa Zanzibar na Tanganyika una historia ndefu hivyo wanaoubeza
ni wachache na wengi wao wanatoka Chama cha Wananchi (CUF).
“Wanaotaka
kuvunja muungano ni CUF , na sio Wazanzibari wote, kwani ubaguzi
umeanzia Pemba, na Seif Sharif Hamad ambaye aliiba nyaraka za Abdu Jumbe
na kumpelekea Mwalimu Nyerere akidhani atapewa yeye madaraka,” alisema
Panya.
Kwa upande
wake mjumbe kutoka Zanzibar, Mwinyi Haji Makame, alisema hoja ya
serikali tatu kwa hao wachache wanaoitaka wameikuta Dodoma na kwamba
muundo huo ni kutaka kuvunja Muungano.
“Huyo
Sultani alitawala Zanzibar zaidi ya miaka 300, alivyoondoka aliwaachia
nini Wazanzibari, hakuna lolote, lakini leo tunaona miaka 50 ya Muungano
kuna manufaa mengi, tunaamini Mapinduzi ndio Muungano na
havitenganishwi kamwe , asiyeweza arudi kwao,” alisema Makame.
CHANZO:HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment