Marekani imeelezea wasiwasi
mkubwa kuhusu mzozo unaozidi kutokota mashariki mwa taifa la Ukraine
ambapo makundi ya wanaharakati wanaoiunga mkono Urusi yameteka majengo
ya serikali na kutangaza baadhi ya majimbo katika eneo hilo kuwa
Jamhuri.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry ameionya Moscow kuwa kutakuwa na adhabu iwapo itaendelea na
hila ya kuivuruga Ukraine.Bwana Kerry alimwambia mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kuwa utekaji wa majengo ya umma ulionekana kupangwa kikamilifu katika miji mitatu Mashariki mwa Ukraine.
Alisema utekaji nyara huo ulionekana kuchochewa kwa ushirikiano na Serikali ya Urusi na akasisitiza kuwa mipango zaidi ya kuvuruga amani nchini Ukraine itasababisha kuwepo kwa masharti makali zaidi kuwekewa Urusi vikwazo zaidi.
‘Watu hawa hawana mamlaka yo yote ya kisheria kuchua hatua hizo. Ikiwa Urusi itaingia Mashariki mwa Ukraine, kwa njia moja au nyingine hali itakuwa mbaya zaidi. tunatoa wito kwa rais putin na serikali yake kusitisha hatua zote za kuvuruga ukraine.’
Mashauriano kati ya Bwana Kerry na Bwana Lavrov yanaendelea wakati Ukraine inapozidi kuwatuma maafisa wa usalama zaidi katika miji ya Mashariki ya Donetsk, Luhansk na Kharkiv kufuatia utekaji wa majengo ya Serikali na makundi yanayounga mkono utawala wa Urusi.
Katika Donetsk, watu walioshikilia jengo la Utawala wametangaza wanachotaja kama "Jamhuri ya wananchi".
Katika picha za video zilizonaswa na mmoja wa mashahidi wa tukio hilo na kupeperushwa na runinga ya Ukraine, mtu ambaye hakutambuliwa anasikika akisema kuwa Jamhuri iliyojitangaza itauliza Urusi iwatume wanajeshi katika eneo hilo iwapo Ukraine itapinga upigaji wa kura ya maoni.
0 comments:
Post a Comment