Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu
na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini
Dar es salaam kutoa taarifa ya mfumuko wa bei nchini unapimwa kwa kipimo
cha mwezi.
( Na. Aron Msigwa/MAELEZO - Dar es salaam)
Ofisi ya Taifa ya
Takwimu imeeleza kuwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Machi umeongezeka ikilinganishwa na
mwezi uliopita kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma
mbalimbali.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na
sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraimu Kwesigabo amesema kuwa mfumuko wa bei wa
Taifa kwa mwezi Machi 2014 umeongezeka na kufikia asilimia 6.1 kutoka asilimia
6.0 mwezi uliopita.
Amesema kuwa kasi
ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Machi 2014 imeongezeka kidogo
ikilinganishwa na ile iliyokuwepo mwezi Februari huku kukiwa na ongezeko
dogo la upandaji wa bei kwenye baadhi ya bidhaa na huduma mwezi huu
ikilinganishwa na bei za mwezi Machi mwaka jana.
Ameeleza kuwa
mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na migahawa kwa mwezi Machi umeongezeka
hadi asilimia 7.9 kutoka asilimia 6.9 za mwezi Februari mwaka huu huku badiliko
la fahirisi za bidhaa zisizo za vyakula likipungua hadi asilimia 5.2 kwa mwezi
Machi 2014 kutoka asilimia 6.2 za mwezi Februari.
Amefafanua kuwa mwenendo
wa bei za bidhaa za vyakula kama samaki, mbogamboga, ulezi na matunda, ndizi za
kupika na maharage zimeonyesha kuongezeka kwa kiwango kikubwa kwa mwezi Machi
ikilinganishwa na bei za bidhaa hizo kwa mwaka uliopita huku bei za bidhaa
zisizo za vyakula za vitambaa vya suti za wanaume, gharama ya usafi wa nywele
na usafi binafsi, Petroli, mkaa, huduma za matibabu pamoja na tiketi za
kutazama mpira wa miguu ligi kuu zikionyesha ongezeko.
Kwa upande wa
mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi,ameeleza kuwa kumekuwa na
ongezeko dogo kwa asilimia 0.6 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 1.4
kwa mwezi Februari mwaka huu, huku fahirisi za bei za taifa zikiongezeka hadi
kufikia 149.49 kwa mwezi Machi kutoka 140.93 za mwezi Machi mwaka uliopita huku
fahirisi za zinazopimwa kwa kipimo cha mwezi zikifikia asilimia 149.49 kutoka
148.62 za mwezi uliopita.
Amezitaja bidhaa
zilizochangia ongezeko la fahirisi za bei nchini kuwa ni pamoja na nyanya,
viazi vitamu, matunda, mchele, tambi na kuku wa kisasa ambao wameongezeka kwa
asilimia 1.8.
Aidha kufuatia
hali hiyo ya mfumuko wa bei Bw. Kwesigabo ameeleza kuwa uwezo wa
shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii kwa mwezi
Machi umepungua na kufikia shilingi 66 na senti 90.
“Kupungua kwa thamani ya
Shilingi kunamaanisha kwamba, kama mtu alikuwa na uwezo wa kununua bidhaa kwa
Shilingi 100 mwaka jana, basi kwa mwaka huu itampasa aongeze zaidi ili aweze
kununua kitu kama kile kile, kwa mfano badala ya shilingi 100 inabidi atumie
shilingi 134”
Kuhusu ulinganifu
mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki amesema
kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya
umepungua kidogo na kufikia asilimia 6.27 kwa mwezi Machi kutoka asilimia
6.86 za mwezi Februari, huku Uganda ikiwa na mfumuko wa asilimia 7.1
kwa mwezi Machi ikilinganishwa na asilimia 6.8 za mwezi uliopita.
0 comments:
Post a Comment