Rais
Dkt Jakaya Mrisho Kikwete amekumbuka enzi za kuwa mwalimu katika Chuo
cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania cha Monduli, Arusha, alipotoa
mhadhara katika Chuo cha Taifa cha ulinzi (National Defence College
-NDC- ) kilichopo Kunduchi jijini Dar es salaam ambako aliahidi kwamba
baada ya kustaafu Urais mwakani atakuwa mwalimu chuoni hapo. Pichani
anaonekana Rais Kikwete akisikiliza swali kutoka kwa mmoja wanafunzi
hao baada ya mhadhara wake.
Rais
Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Wahadhiri na wanafunzi wa Chuo cha
Taifa cha ulinzi (National Defence College -NDC- ) kilichopo Kunduchi
jijini Dar es salaam ambako aliahidi kwamba baada ya kustaafu Urais
mwakani atakuwa mwalimu chuoni hapo.(PICHA NA IKULU).
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa hana wasiwasi na hali ya mjadala mkali uliotawala Bunge
Maalum la Katiba kwa sababu ni muhimu kwa mjadala kuhusu Katiba Mpya
ukawa wa kina ili kuweza kupata Katiba bora kwa Watanzania.
Aidha, Rais
Kikwete amesema kuwa Katiba ya Tanzania haitapatikana kwa mikutano ya
kisiasa nje ya Bunge Maalum la Katiba bali ndani ya Bunge hilo ambako ni
dhahiri kuwa mjadala utatawaliwa na nguvu ya hoja na busara.
Rais
Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama
ametoa ufafanuzi huo, Ijumaa, Juni 20, 2014, wakati alipotoa Mhadhara
(Lecture) kuhusu Usalama wa Taifa (The Security of the Nation) kwenye
Chuo cha Taifa cha Ulinzi – National Defence College – kilichoko
Kunduchi, Dar Es salaam.
Wakati wa
kipindi cha maswali na majibu, ofisa mmoja wa Jeshi la Kenya alimwuuliza
Rais Kikwete kama alikuwa na wasiwasi kuhusu mjadala unaoendelea nchini
kuhusu Katiba Mpya unaweza kuvuruga usalama wa Tanzania.
Rais Kikwete amemjibu: “Sina
wasiwasi hata kidogo kwa sababu hatukutarajia kuwa mjadala wa Bunge
Maalum la Katiba kuhusu jambo hili kubwa ungekuwa rahisi. Yalipojitokeza
maoni ya Tanzania kupata Katiba Mpya, tuliunda Tume na tume hiyo ikatoa
ripoti yake ambayo ndiyo inajadiliwa katika Bunge Maalum. Hatukutarajia
kuwa mjadala kuhusu ripoti ungekuwa rahisi kwa wajumbe kutoa majibu ya
ndiyo ama hapana.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kinachoendelea
ni jambo muhimu na la lazima…najua wakati mwingine majadiliano yalikuwa
makali mno lakini hili ni jambo zuri. Aina ya mfumo na muundo wa
Serikali lilizusha mjadala mkali lakini hayo ni matokeo ya hali halisi
ya masuala yanayojadiliwa.”
“Ni
imani yangu kuwa tutafikia mwisho. Mwisho upi, hilo ni suala la Wajumbe
wa Bunge Maalum la Katiba kuamua. Muhimu ni kwamba Katiba Mpya inaweza
kupatikana kutoka Bungeni tu siyo kupitia mikutano ya hadhara nje ya
Bunge. Huko hakuna Katiba huko kuna mikutano ya hadhara na siasa tu.
Katiba itapatikana kwa mijadala na kwa nguvu ya hoja ndani ya Bunge
letu.”
0 comments:
Post a Comment