TFF: MABADILIKO
Rais Mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania Jamal Malinzi
Shirikisho la Kandanda nchini (TFF) linatarajia kufanya mabadiliko makubwa ya wakuu wa idaara mbalimbali kwa lengo la kuleta kasi na ari mpya baada ya uongozi mpya kuingia madarakani.
Mabadiliko hayo yanatarajiwa kufanyika mara baada ya wakuu mbalimbali wa Idara kumaliza muda wao ifikapo Desemba 31 mwaka huu na hakuna mpango wa kuwaongezea mkataba baadhi ya wakuu wa idara hao.
Habari za uhakika kutoka kwa mmoja wa viongzi wa juu wa TFF zilisema kuwa shirikisho hilo linatarajia kutangaza nafasi za kazi kwa upande wa wakuu wa Idara ifikapo Novemba 15 na mpaka sasa, kitengo cha habari chini ya Ofrisa Habari, Boniface Wambura pekee ndicho hakitaathirika na mabadiliko hayo.
Hatua ya kumbakiza Wambura inatokana na ufanisi katika kazi yake na kuvutiwa na Kamati ya Utendaji na kufikia hatua ya kumteua kuwa Kaimu Katibu Mkuu baada ya kupewa likizo yenye malipo kwa aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo, Angetile Osiah.
Taarifa hizo zimesema kuwa Wambura anapigiwa chapuo kubwa kushika wadhifa huo kutokana na utendaji wake bora wa kazi.
“Tumeamua kufanya kazi ya kuleta maendeleo katika soka la Tanzania, hivyo chukulieni mabadiliko haya ni ya kawaida na hasa kwa uongozi ambao unataka kuweka historia ya maendeleo ya soka nchini.
“Mabadiliko hayana muda maalum, hakuna cha kusubiri kwani mtu anapimwa kutokana na ufanisi wake na wala si vinginevyo, kuna watu wamesema mamuzi ya kumsimamisha Katibu Mkuu ni ya kisasi, siyo kweli kwani ni maamuzi ya pamoja,” alisema mmoja wa viongozi wa TFF.
Alisema kuwa kampuni ya KPMG inatarajiwa kupewa kazi ya kuwatafuta wafanyakazi wapya (wakuu wa idara) wa shirikisho hilo na kuwataka wadau wa michezo kukaa ‘mkao wa kula’ ili kutuma maombi yao.
Nafasi ambazo zinatarajiwa kutangazwa ni Mkurugenzi wa Idara ya Fedha ambayo ipo chini ya Kaimu Mkurugenzi, Yonaza Seleki, Mkurugenzi wa Utawala na Wanachama (tupu), Mkurugenzi wa Mashindano (Saad Kawemba), Mkurugenzi wa Masoko na Matukio (James Kabwe) na Mkurugenzi wa Ufundi iliyo chini ya kocha maarufu Sunday Kayuni.
0 comments:
Post a Comment