Waziri wa Katiba na Sheria Dk Asha-Rose Migiro. |
Migiro amesema kuwa mpaka kufikia Februari 9, mikoa 11 nchini
ilikuwa tayari imeshapatiwa nakala hizo na kwamba Serikali imepanga
kuchapisha nakala milioni 2 kwa ajili ya kuzisambaza nchi nzima.
Ameendelea kwakusema kuwa hapa nchini kuna zaidi ya kata 3,800 na lengo la
Serikali ni kusambaza nakala hizo kwenye vijiji, vitongoji na mitaa
kupitia Ofisi za wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za
miji, manispaa na majiji.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, (Terminal one)
akitokea mkoani Dodoma, Dk Migiro alisema mbali na
nakala hizo, Katiba Inayopendekezwa pia imewekwa katika tovuti za
Wizara ya Katiba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bunge.
“Wananchi waliokuwa katika miji na vijiji siyo
wote wanaweza kupata nakala katika mtandao. Ukiwa na nakala halisi
unaisoma wakati wote kwa hiyo Serikali imekuwa na nia ya kuwapatia
watanzania nakala halisi haraka iwezekanavyo,” alisema.
Alisema Serikali ilipoanza mchakato wa uchapaji wa
nakala hizo liliibuka tatizo la mitambo kwa baadhi ya wachapishaji na
hivyo kucheleweshwa kuzigawa, lakini kwa sasa nakala nyingi
zinaendelea kusambazwa kadri zitakavyokuwa zikichapwa.
“Karibu nusu ya mikoa yote imepelekewa nakala
hizo. Tumeweka utaratibu mzuri ambao kila mkoa utapata nakala kutokana
na wingi wa kata zake, hatuwezi kugawa nakala sawa kutokana na
kutofautiana kwa idadi ya kata” alisema.
Aliitaja mikoa ambayo imepata nakala hizo na idadi
yake katika mabano: Katavi (15,640), Rukwa (27,040), Ruvuma (47,740),
Mbeya (78,640), Simiyu (34,840), Mara (52,540), Tabora (58,540) na
Kigoma (41,440).
Mikoa mingine ni Kagera (54,340), Geita (36,940),
Mwanza (57,040) na Pwani ambapo usambazaji umeanza kwa wilaya ya Mafia
ambayo imepata nakala 2,400.
Alipotakiwa kufafanua kama nakala hizo zitatosha
ikilinganishwa na idadi ya Watanzania alisema, “Jambo la muhimu ni
utolewaji wa elimu kuhusu Katiba Inayopendekezwa. Nakala hizi zinatosha
kwa sababu Katiba ni waraka wa kisheria unaweza ukausoma na bado ukabaki
kuhoji baadhi ya mambo.”
Alisema nakala 1,800,000 zinasambazwa Tanzania Bara na nakala 200,000 zinasambazwa Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment