Kitendo cha Bunge Maalumu la Katiba kukusanya maoni ya makundi na wananchi mbalimbali, kimepokewa kwa hisia tofauti, baadhi ya wasomi wakisema ni kinyume cha sheria na kuonyesha kutapatapa huku Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akisema linafanya kazi ambayo tayari tume yake ilishaifanya.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad amesema litaendelea kupokea mapendekezo kutoka kwa watu na makundi mbalimbali hadi hapo litakapohitimisha kazi yake.
Kwa muda sasa, wawakilishi wa taasisi mbalimbali wamekuwa wakifika Dodoma kuwasilisha mapendekezo yao wakitaka yazingatiwe kwenye Katiba Mpya kwa maelezo ya kutoonekana katika rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Suala hilo limezua mjadala hasa katika mitandao ya kijamii ambako watu mbalimbali wamekuwa wakihoji sababu za Bunge hilo kufanya kile kinachotafsiriwa kuwa ni ‘kukusanya maoni’, kazi ambayo tayari ilishafanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Akitetea hoja hiyo, Hamad alitetea akisema wananchi, watu au taasisi zinazotoa mapendekezo yao zinashirikiana na wabunge katika mchakato wa kile kinachoendelea bungeni hivi sasa.
“Tutaendelea kupokea maoni ya wananchi kwa sababu na sisi tunaendelea kujadili, kwa hiyo kadri makundi yatakavyoleta maoni yao, tutayapokea na kuyapitisha kwenye mchakato wa kuyawezesha kuzingatiwa kama yataonekana yanafaa,” alisema Hamad.
Warioba na wasomi
Akizungumzia hatua hiyo, Jaji Warioba aliponda kitendo cha kukusanywa upya kwa maoni hayo akisema yalishachukuliwa na Tume yake na kuingizwa katika Rasimu ya Katiba.
“Nyaraka zote za maoni, yakiwamo ya makundi hayo tuliziwasilisha, sasa wanakusanya maoni mapya ili iweje? Wanatakiwa kufuata maoni ya wananchi na si ya makundi na kama wanafanya hivyo basi maoni ya makundi hayo yakusanywe hadharani ili wananchi wayasikie ili nao waweze kuchangia,” alisema jana.
Alitolea mfano wa maoni yaliyotolewa na Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT), kwamba ni makosa kuchukua maoni hayo na kuyaacha yaliyotolewa nawananchi.
“Naona kuhusu ardhi eti wamechukua maoni ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi, hii si sahihi kabisa. Kama wanajadili suala la serikali za mitaa, ardhi na maliasili wanatakiwa kuyaongeza mambo hayo katika mambo ya muungano kwa sababu hivi sasa mambo hayo si ya muungano na ndiyo maana Tume hatukuyaingiza katika Rasimu ya Katiba,” alisema
.
.
0 comments:
Post a Comment