BUNGE LA KATIBA SASA PATASHIKA; SITTA AWAJIA JUU MAASKOFU!!

MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta

MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, amewaonya Maaskofu akisema watadharauliwa endapo tu wataendelea na tabia zao zisizofaa za kuvuruga mchakato wa kupatikana Katiba Mpya kwa kuendelea kuruhusu nyaraka za uchochezi zisomwe makanisani.

Alisema hatua hiyo ikiachwa iendelee inaweza kuliingiza Taifa kwenye udini, ambao unaweza kuvuruga mshikamano uliopo miongoni mwa Watanzania kwa miaka mingi sasa.

Sitta alitoa kauli hiyo jana bungeni mjini Dodoma alipokuwa akitoa tahadhari kuhusu kusambazwa waraka unaodaiwa kuandikwa na maaskofu ambao unapinga mchakato wa Bunge hilo huku wakiruhusu usomwe makanisani.

Alisema kuwa kama kazi ya maaskofu hapa nchini ni kuwatisha wanasiasa, basi waendelee na kazi hiyo, lakini si kukosoa hata mambo mazuri yanayofanywa na Bunge hilo.

Sitta alisema kuwa waraka huo una lugha zinazotumiwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na hivyo ikiwa nchi itaruhusu nyaraka za siasa zitumike makanisani, basi nchi itaenda mahali pabaya.

Aidha, aliwataka maaskofu hao ambao walikusanywa na UKAWA jijini Dar es Salaam kujitokeza hadharani na kuweka misimamo yao wazi kwa kuwa hakuna siri, kwani Mungu anaona na kanisani pia kuna watu wasiopendezwa na vitendo hivyo vinavyofanywa na viongozi hao wa dini.

Katika waraka huo aliousoma bungeni ambao unamtaka Rais Jakaya Kikwete, kusitisha Bunge hilo, kurudisha tume, na kutaka Bunge kutunga kanuni itakayolinda rasimu ya pili pamoja na kuitaka wizara husika kurudisha tovuti ya Tume, lugha ambayo alisema inatumiwa na UKAWA na si kwamba hayo ni maelekezo ya kiroho.

Hata hivyo, Sitta, alihoji kama yeye anatumia ubabe bungeni mbona anatukanwa na mbaya zaidi Tume imekuwa ikiendelea kufanya kazi ya kukosoa kazi inayofanywa na Bunge hilo kila kukicha?

Alisema kuwa watu wamekuwa wakieneza chuki na kufikia hatua baadhi ya wajumbe wanatukanwa, kutishiwa maisha pamoja na kufungiwa ndani ili wasiweze kupiga kura kitu ambacho hakiwezi kukubalika.

"Juzi mjumbe mmoja amefungiwa ndani ya chumba chake cha hoteli ili asiweze kupiga kura, eleweni kwamba kumfungia mtu ndani ni kosa la jinai, msiotutakia mema kwa haya mazuri tumieni njia nyingine ila msitumie njia za kijinai kufanikisha malengo yenu," alisema.

Alisema kuwa watu hao ambao hawapendi mchakato huo uendelee wamekuwa wakiwatisha wajumbe na kuwataka waondoke haraka na wasibaki bungeni.

Alisema kuwa vitisho vinavyofanywa na watu hao ambao hawaitakii mema nchi wanataka kwa upande wa Zanzibar Katiba isipite,lakini hawawezi kufanikiwa hata kidogo.

"Wanadhani kwamba kura za Chama cha CUF, zikipungua Katiba haitapita, la hasha! Mimi naona wanapoteza muda, watumie njia nyingine si vitisho," alisema Sitta.

Pia, alimtaka Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika kumheshimu kwa kuwa yeye ni mzee katika nchi hii na pia ni kama baba yake mzazi, hivyo aache tabia ya kutumia lugha za matusi dhidi yake.

Alisema kuwa Mnyika amekuwa akijipendekeza kwa kutumia majukwaa na kutoa lugha zisizofaa na kusema kwamba hizo ni siasa za vyuoni na za kitoto na kwamba hawawezi kushika madaraka kwa kutumia mbinu za kitoto.

Wakati huo huo, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA); vimetoa tuhuma nzito dhidi ya Bunge Maalumu la Katiba, vikidai wabunge wake upande wanashinikizwa kupiga kura za kuikubali rasimu iliyopendekezwa na Bunge hilo ili kurahisisha upatikanaji wa theluthi mbili zinazohitajika.

Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Ufundi ya UKAWA imeitisha kikao cha dharura cha siku mbili kuanzia jana na leo ili kujadili matukio yanayoendelea katika Bunge hilo.

Kikao hicho, ndicho kinachotarajiwa kutoa maazimio ya kuwashauri viongozi wa vyama vinavyounda umoja juu kuhusiana na hatua za kuchukua.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya UKAWA wa Chama cha Wananchi (CUF),Joramu Bashange, alisema lengo la hatua hiyo ni kutaka kuonesha jamii ni kwa namna gani viongozi Bunge la Katiba, wanavyoshinikiza wajumbe kusaini karatasi za kura na kuwapa ahadi za vishawishi ili kurahisisha kuchakachua matokeo na kupitisha rasimu hiyo.

Alitoa mfano, akisema tangu UKAWA watoke bungeni, Aprili 16, mwaka huu wajumbe waliobaki walifanya mabadiliko ya kanuni na kupitisha rasimu ya CCM kuonesha kuwa ni maoni ya wananchi yaliyotolewa na Tume iliyoongozwa na Jaji Warioba.

Alifafanua kwamba, awali walisema kura zitapigwa ibara kwa ibara, lakini Agosti 5 walibadilisha na kusema Ibara zote zitapigwa kwa pamoja kwa mujibu wa Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo ili kuweza kuwalazimisha wajumbe kukubaliana na matakwa yao.

Mjumbe kutoka CHADEMA, John Mnyika, alisema wanayo majina ya wajumbe kutoka chama chao ambao wamefuatwa na kushawishiwa kusaini fomu ili wapige kura kupitia mtandao.

Huku akitaja jina la aliyewafuata kwa lengo la kuwashawishi, Mnyika aliwapongeza wale waliopiga kura za hapana wazi wazi na kuendelea kusisitiza kuwa lazima Bunge hilo lifahamu kuwa Katiba haitengenezwi kwa mtutu.

Alisisitiza kuwa Katiba inayofaa inatokana na maoni ya wananchi na si ya Chama tawala. Alisisitiza kuwa Bunge linaloendelea si halali na kwamba watahakikisha haki inatendeka ili wananchi waweze kupata Katiba waliyoipendekeza.

Pia alilaani kitendo chaMwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, wakidai amekwenda kinyume cha kanuni na kutoa kauli mbaya kwa viongozi wa dini.

Alisema kauli ya Mwenyekiti huyo kuwataka viongozi hao wadharauliwe ni matendo yanayoonesha jinsi gani anavyotumia mabavu kuibadilisha rasimu hiyo.

Pia aliwalaani tabia ya baadhi ya wanaharakati kutumika vibaya kuhalalisha mambo ambayo yako kinyume cha sheria na kuwataka wale wenye nia njema na nchi kuendelea kupambana ili kuweza kupata katiba itakayofaa inayoendana na maoni ya wananchi.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment