MWANASHERIA AIBUA MTAFARUKU BUNGENI ATOLEWA NJE CHINI YA ULINZI MKALI!!


 

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman (mwenye Kaunda suti ya kijivu) akisindikizwa kutoka nje ya viwanja vya Bunge Maalum la Katiba leo mjini Dodoma na Askari Polisi mara baada ya kushutumiwa na baadhi ya Wajumbe wa Zanzibar.

MWANASHERIA Mkuu wa Zanzibar na Mjumbe Maalum wa Bunge la Katiba, Othman Masoud Othman, amekataa ibara nyingi za Katiba inayopendekezwa kwa kupiga kura ya hapana hali iliyozua mtafaruku mkubwa bungeni, huku wajumbe wengine kutoka Zanzibar wakimtaka ajiuzulu wadhifa huo.

Hatua ya mjumbe huyo ambaye ni miongoni mwa viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alikataa ibara ya 2, 9, 70-75, 86, 87, 158,159,160,161,243-251 huku akikubaliana na ibara nyingine zilizobaki.

Baada ya kupiga kura hiyo bungeni mjini Dodoma jana, Othman alianza kusakamwa na wajumbe wengine kutoka Zanzibar wakimtuhumu kufanya uamuzi usio sahihi na kushinikiza Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, amfute kazi mara moja kwani amekuwa si kiongozi mzalendo kwa Zanzibar.

Hata hivyo, wajumbe hao kutoka Zanzibar walimzomea na kudai kuwa hafai tena kuwa Mwanasheria wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Othman ambaye alipiga kura ya wazi ambapo alianza kuchambua baadhi ya ibara hizo ambazo hakubaliani nazo kwenye rasimu hiyo hali iliyoibua mtikisiko mkubwa bungeni kutokana na wadhifa alionao katika Serikali ya Zanzibar.

Mjumbe mmoja kutoka Zanzibar alisimama na kusema kuwa mwanasheria huyo anapiga kura kwa cheo chake na kujifanya msomi, lakini hafai hata kidogo kuendelea kushikilia wadhifa huo.

"Anajifanya msomi, kwanza amechelewa kuingia bungeni hafai na cheo chake cha kuteuliwa," alisema mjumbe huyo huku wajumbe wengine wakipiga makofi na wengine wakisikika kusema kwamba amekimbia vita.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, alilazimika kuingilia kati mzozo huo na kueleza kuwa si jambo la busara kujadili kura ya mtu, kwani ametumia vizuri haki yake ya kisheria ya kupiga kura.

Sitta alisema wajumbe hao hawapaswi kumhukumu Othman kwa cheo chake, bali watambue amefanya hivyo kwa dhamira yake binafsi kama mjumbe halali ya Bunge hilo la Katiba.

Hata hivyo, mara baada ya kuahirishwa kwa Bunge hilo, Mwanasheria huyo Mkuu wa Zanzibar aliondolewa ukumbini chini ya ulinzi mkali ili kulinda usalama wake baada ya wajumbe wengi kutoka Zanzibar kutoridhika na uamuzi huo.

Hili ni tukio la kwanza la kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupiga kura ya hapana hali ambayo imetafsiriwa kuwa ni ishara mbaya kwa mchakato huo kuelekea kupatikana kwa Katiba Mpya.

Hata hivyo, tangu kuanza kwa kazi ya upigaji kura baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar wamekuwa wakipiga kura za wazi za hapana huku wengine wengi wakipiga kura za siri.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment