Hamad Rashid (kushoto) Maalim Seif Sharif Hamad (kulia) |
Mwanasiasa mkongwe nchini, Hamad Rashid Mohamed, atavaana na Katibu
Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad katika
kinyang’anyiro cha urais visiwani Zanzibar.
Hamad Rashid amekuwa mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
tiketi ya CUF kwa takriban miaka 20 sasa, lakini katika siku za hivi
karibuni, alikwaruzana na chama hicho cha upinzani na kufukuzwa
uanachama. Hata hivyo, alibakiwa na ubunge wake kutokana na amri ya
Mahakama.
Katika mgogoro huo, Hamad Rashid alimtuhumu Seif ambaye ni Katibu Mkuu
wa chama hicho kuwa alifanya makusudi kuvunja amri ya Mahakama
iliyomtaka asitishe kikao kilichokuwa kikijadili hatima yake ndani ya
chama hicho.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, anatajwa
kuwa ndiye atakayekuwa chaguo la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kwa nafasi ya urais Zanzibar kutokana na CUF kuwa tayari imeshaota
mizizi visiwani humo.
Hiyo itakuwa mara ya tano kwa Maalim Seif kugombea urais Zanzibar kama
ataingia kwenye kinyang’anyiro hicho. Alianza kugombea nafasi hiyo mwaka
1995, akagombea tena 2000, kisha 2005 na mwaka 2010 na mara zote hizo,
amekuwa akishindwa kwa tofauti ya kura chache na wagombea wa Chama cha
Mapinduzi (CCM).
Kauli ya ADC
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC),
Doyo Hassan alisema jana kuwa kutokana na mgogoro uliopo na hasa Ukawa
kuwa tayari wameshagawana majimbo, chama hicho kitasimamisha wagombea
wake na Hamad Rashid ameshajitokeza kuutaka urais Zanzibar.
Alisema Hamad Rashid ameonyesha nia yake hiyo kwa viongozi wa chama na
sasa anasubiri muda wa kuchukua fomu ili aanze mchakato huo wa kuitafuta
Ikulu ya Zanzibar.
“(Hamad Rashid) anasubiri muda tu aje kuchukua fomu, lakini tayari
amekuja tumezungumza naye na amekubali kuja kugombea urais kupitia chama
chetu,” alisema Doyo ambaye alibainisha kuwa fomu hizo zitaanza
kutolewa Julai Mosi hadi Julai 30 mwaka huu.
Hata hivyo, Doyo alitoa wito kwa wanachama wengine wa chama hicho
kujitokeza kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi
pamoja na nafasi za ubunge ili kuleta ushindani utakaokiwezesha chama
kuwapata wagombea bora zaidi.
“Uchaguzi ndani ya chama kwa ajili ya kumpata mgombea urais, unatarajiwa
kufanyika mara baada ya watia nia kurudisha fomu mwishoni mwa Julai na
mgombea wetu atajulikana mwanzoni mwa Agosti,” alisema Doyo.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment