Wakati tukijiandaa kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka ujao mwezi Octoba JINA la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, limeanza kutumiwa na baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukusanya na kugawa fedha kwa kile kinachoitwa “mbio wa kusaka urais.”
Taarifa zilizotufikia zinasema kuwa wajumbe hao wamesema mbio za Pinda kusaka urais zimekuwa na kishindo kikuu kwa sababu ya sera yao kwamba “pesa itaongea.”
Huku baadhi yao wamefikia mahali pa kumtambia Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ambaye naye anatajwa kuwania urais, huku mmoja wa wapambe wake akisema, “Walidhani wao ndio wana pesa tu. Sasa tutawaonyesha kazi.”
Hatahivyo baathi ya wajumbe wamenukuliwa wakisema kuwa Pinda ndiye tishio jipya la Lowassa, na katika hatua ya kwanza ameshauriwa atumie fedha ya kutosha kufikia wajumbe wengi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi, wanaojulikana kama Wanec.
Inafahamika kwamba, kwa muda mrefu, Lowassa ndiye amekuwa na nguvu kubwa miongoni kwa wanec wa mikoa mingi.
Ili kukabiliana na nguvu hiyo, timu ya Pinda inadaiwa kuteua familia moja yenye madaraka makubwa ya kisiasa jijini Dar es Salaam, kushika mikoba yake. Taarifa zinasema mume akipita huku, mke anapita kule.
“Kazi ya kwanza waliyo nayo ni kulainisha wanec ambao ndio wapiga kura za maoni watarajiwa. Lengo ni kuvuta kasi ya waliomtangulia, ambao walishakuwa na mitandao imara ya wafuasi ndani ya NEC,” anadai mnec mmoja ambaye anadai kushuhudia matukio kadhaa ya makundi ya watu kupewa fedha kwa jina la Pinda.
Habari za ndani zinasema mtandao huo unafadhiliwa na matajiri na wawekezaji kadhaa wanaowekeza katika maeneo nyeti, akisaidiwa na baadhi ya watendaji wa serikali katika wizara nyeti ambayo imekuwa na migogoro mingi kwa miaka tisa mfululizo. Wanakusanya fedha kutoka kwa matajiri hao.
Baadhi ya wawekezaji wanaofahamika hadi sasa ni waziri mmoja mwenye makeke na majivuno na katibu wake mkuu, ambao wanadiwa kukusanya fedha kutoka kwa wawekezaji wa rasilimali za nchi ambazo zimekuwa zinaleta mvutano na utata kati ya serikali na wananchi, kiasi cha kuchafua hali ya kisiasa katika mikoa kadhaa ya Kusini mwa Tanzania.
Yumo pia tajiri mmoja anayemiliki mabasi, mbunge mmoja wa Zanzibar na mzazi wa mbunge mmoja mwenye asili ya Kiasia, ambao wote kwa pamoja ni wawekezaji katika biashara ya sukari.
Zipo taarifa kuwa mkubwa wanayempigania amesaidia kurahisisha wapate vibali ya kuingiza sukari kwa wingi. Wamo pia wamiliki wa super market moja maarufu ambayo imekuwa na utata katika miezi ya karibuni.
Ili kuwasilisha fedha hizo kwa wahusika, zinatumika fursa, sehemu na staili mbalimbali katika kugawiana pesa.
Miongoni mwa matukio makubwa yanayotajwa yanayohusisha wapambe na wanec hao ni haya yafuatayo:
Tarehe 20 Oktoba 2014, katika jengo moja la kisasa, jijini Dar es Salaam, jirani na Hospitali moja maarufu yenye kutafiti na kuibu magonjwa sugu nchini, mke wa mshika mikoba alikodi ofisi ambayo aliitumia kukutana na wanec kadhaa na kuwagawia fedha.
Miongoni mwao ni wanec kutoka Kigoma Vijijini, Shinyanga na Bungeni, ambao kila mmoja walipewa dola za Kimarekani 600, sawa na sh. milioni moja ya Kitanzania.
Majina ya wanec hao tunayahifadhi kwa sasa. Tarehe hiyo hiyo, vijana kadhaa wa UVCCM kutoka Ilala, nao walikutana na mshika mikoba huyo, akawagawia sh. 200,000 kila mmoja.
Tarehe 16 Oktoba 2014, katika majengo ya NHC Dodoma, nyumbani kwa mbuge mmoja wa Viti Maalumu kutoka Singida, mke wa mshika mikoba huyo anadaiwa kupokea sh. milioni 24 kutoka ofisi moja ya umma, iliyo chini ya mabosi hao wa wizara waliotajwa. Inasemekana fedha hizo zililetwa kwa agizo la katibu mkuu husika, baada ya fungu la awali walilokuwa wamesafiri nalo kwenye mabegi kuisha.
Baada ya kupokelewa na mshika mikoba, alikabidhiwa mnec mmoja kutoka Mbozi, akazigawa kwa baadhi ya wanec kutoka Zanzibar.
Tarehe 14 Oktoba 2014, wapambe hao na mshika mikoba walikutana nyumbani mwa kigogo mkubwa serikalini, Masaki, Dar es Salaam, wakawezesha wanec kadhaa kutoka Dar es Salaam, Tanga, Pwani na Zanzibar, kiasi cha sh. milioni moja kila mmoja.
Baadaye, katika hoteli moja maarufu nje kidogo ya mji wa Dodoma, na nyingine maarufu katikati ya mji, katika siku ya kwanza ya kikao cha NEC, wanec wapatao 42 wanadaiwa kupokea sh. 200,000 kila mmoja kutoka kwa mshika mikoba huyo na mkewe.
Kati ya tarehe 15 hadi 18 Oktoba 2014, mshika mikoba huyo na mkewe waligawa fedha kwa wanec kwa viwango vya sh.300,000; 500,000 na 700,000. Makatibu wa Wilaya wanadaiwa kupewa sh.150,000 hadi 300,000.
Tarehe 18 Oktoba 2014, asubuhi kabla ya wajumbe kuondoka, wanec kadhaa kutoka Mkoa wa Kagera wanadaiwa kupokea sh. milioni moja kila mtu.
Hali hii ndiyo ilimfanya Makamu Mwenyekiti wa CCM Phillip Mangula, wakati anawasilisha taarifa ya kamati ya maadili kwenye NEC, akasema kwamba amegundua kuwa pale Dodoma kumezuka ATM mpya. Alionya kuwa wahusika wataitwa na kuonywa.
Kutokana na makeke ya wapambe hawa wanaotumia jina la Pindi kugawa fedha, zipo taarifa kwamba tayari kamati ya maadili imemuita na kumuonya waziri mkuu kuhusiana na tuhuma hizi.
Kauli za wahusika
Nae Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye,amenukuliwa akisema kuhusu ukweli wa taarifa hizo, alisema: “Mimi nazisikia kutoka kwako, kama mmeziokota bafuni au chooni mtajua ninyi lakini mimi ndiyo nazisikia kutoka kwako,”
Mnec kutoka Kigoma alipoulizwa kuhusu fedha hizo, alikanusha, lakini alikiri kwamba juzi alikuwa katika jengo jirani na Hospitali ya Ocean Road.
Alisema jengo lile ni la ofisi, na kwamba alienda katika moja ya ofisi ya jengo hilo kwa shughuli zake binafsi. Alikana kukutana na mke wa mshika mikoba huyo, lakini akasisitiza kuwa alikwenda pale kwa shughuli zake binafsi.
Katika hatua ya kujichanganya, Mnec huyo aliuliza kama kuna taarifa zozote zinazomuhusu. Alipoelezwa kuwa zipo bila kujua ni taarifa gani, alianza kujitetea kuwa kwa nafasi yake, yeye ni mtu mdogo asiyeweza kuhusishwa katika makundi ya wawania urais kupitia CCM.
“Mimi ni mtu mdogo sana tena mkulima wa mihogo kutoka Kigoma. Hayo makundi ni ya watu wakubwa. Kwanza hata pombe sinywi sasa nitakaa nao wapi?”alihoji.
Alipoulizwa sababu ya kujitetea kuwa hayupo katika makundi hayo ilihali mwandishi hajamueleza kama habari aliyonayo inahusiana na makundi ya urais, Mnec huyo aliomba kukutana na mwandishi katika hoteli ya Harare Inn, Dar es Salaam, jambo ambalo halikutekelezwa na mwandishi.
Mnec mwingine atokaye Shinyanga, alipoulizwa kuhusu fedha alizopokea juzi, alisema mwandishi amemfananisha na mtu mwingine, kwani yeye hahusiki.
Alipoulizwa ataje mtu aliyefananishwa naye, aliomba mwandishi ampigie simu baadaye kwa kuwa muda huo alikuwa katika mkutano. Jitihada za gazeti hili kumpigia simu hazikuzaa matunda baada ya namba yake kuita bila kupokewa na wakati mwingine simu ilikatwa.
Mnec wa Tabora alidai kwamba hajawahi kufika katika jengo hilo kwa ajili ya kupokea fedha kutoka kwa mke wa mshika mikoba wa Pinda.
Alisema kuwa tangu alipopata ajali hajaweza kufanya shughuli yoyote hata kuhudhuria vikao vya kamati ya bunge vilivyoanza juzi jijini Dar es Salaam, na kwamba kwa muda huo alikuwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya.
“Ninyi si mnajua kuwa ninaumwa nilipata ajali ya gari hata gazeti lenu liliandika ajali hiyo sasa iweje niende huko wakati sijaanza kutoka? Lakini nikwambie wewe ni mtu wa pili kunipigia simu na kuniuliza swali hilo wa kwanza ni kaka yangu Hussein nikamueleza kuwa sijaenda kuchukua fedha kwa mtu yeyote yule,” alisema.
Source:Mtanzania Daima
Source:Mtanzania Daima
0 comments:
Post a Comment