KASHFA YA MISS TANZANIA YAHUSISHWA NA SIASA!!



Miss Tanzania 2014 na baba yake, Abbas MtemvuWAKATI mtoto wa mbunge wa Temeke, Sitti Mtemvu akiandamwa na kashfa ya kughushi umri baada ya kushinda Miss Tanzania 2014, baba mzazi wa mrembo huyo, Abbas Mtemvu, ameibuka na kudai sakata hilo ni vita ya kisiasa inayoratibiwa na wapinzani wake ndani ya CCM.
Tangu Sitti atangazwe mshindi Miss Tanzania katika shindano lililofanyika Oktoba 11 katika ukumbi wa Mlimani City, wadau mbalimbali wa urembo wamekuwa wakipinga ushindi wake wakidai hakustahili kutokana na kukosa sifa ikiwamo ya kutokuwa na umri stahiki.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika uzinduzi wa Vicoba kwenye klabu ya Jogging ya Temeke A jijini Dar es Salaam, Mtemvu alisema inasikitisha watu wanaolitaka jimbo hilo kumwandama kwa kashfa binti yake kwa maslahi yao binafsi ya kisiasa.
Mbunge huyo, alisema kama mtu anataka jimbo hilo aende kwa hoja na sio kwa majungu na kubainisha kwamba, yeye alichaguliwa na wana- Temeke, hivyo anayelitaka jimbo hilo aende kwa hoja kwa wananchi na si kupakana matope.
“Sikilizeni…hili jambo lisifanywe kisiasa, yule binti wanamdhalilisha sana, inasikitika mtu anaratibu majungu, tena ni matusi makubwa. Sitti wanamchafua tena wanamwambia kuwa binti niliyemzaa mimi eti mtoto wake, ambaye ni Tamia Abbas Mtemvu…haya ni matusi, kisa siasa,” alisema Mtemvu na kuongeza.
Wanapita wanasema Mtemvu kahonga milioni 62 za jimbo, jamani hivi fedha za mfuko wa jimbo zinatoka kwa namna hiyo, haya yote ni…MNEC (mjumbe wa NEC), kama utaka jimbo njoo kwa hoja si majungu na kuchafuana.
“Kwanza kwa taarifa yenu mimi sikuja hapa nikitokea mtaani, nilitoka kwenye kazi yangu, mimi nilikuwa DC (Mkuu wa Wilaya) tena faili langu hadi leo linaonyesha niko likizo…embu waambieni hao, kwanza nani kwaambia watu wa Temeke hatuna hela,” alisema Mtemvu huku akishangiliwa na baadhi ya wana kikundi hicho.
Licha ya kutomtaja mlengwa lakini wachambuzi wa siasa za Temeke walisema kuwa kauli hiyo ilielekezwa kwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Phares Magesa, ambaye inadaiwa kuwa ameonesha nia ya kugombea ubunge jimboni humo mwakani.
Magessa, kwa nyakati tofauti amekuwa akishiriki matukio mbalimbali ya kuimarisha chama hicho Wilaya ya Temeke, huku akitoa misaada mbalimbali kwa makundi ya kijamii ikiwamo vikundi vya Jogging na wasanii.
Misaada ya hivi karibuni ni pamoja na kuchangia mradi wa maji mtaa wa Tambukareli na Oktoba 24, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Jamvi la Katiba.
Alipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo, Magesa alisema hakuna ukweli wowote na kwamba hawezi kutumia u-NEC wake kumchafua kiongozi yeyote wa chama chake.
“Mimi kazi yangu ni kuhakikisha wabunge wangu yeye (Mtemvu) na Ndugulile wanatekeleza vema ilani ya chama chetu ili ukifika wakati wa uchaguzi tukainadi kwa wananchi, hivyo siwezi kumhujumu,” alisema.

Source:Mtanzania Daima
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment