RUSHWA INASHUSHA MAADILI YA VIONGOZI NCHINI-SUMAYE.


WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. Federick Sumaye (Picha na Maktaba)

WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. Federick Sumaye, amesema vitendo vya kuomba na kupokea rushwa vinavyofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa idara za umma, binafsi nchini, vinaporomosha maadili ya viongozi hao na watendaji husika.

Bw. Sumaye aliyasema hayo juzi katika mdahalo maalumu wa kitaaluma uliolenga kuchochea mageuzi ya taaluma kupitia mitandao ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Askofu Mihayo Tabora (AMUCTA) kupitia kitivo chake cha Mahusiano ya Umma.

Alisema watu wanaotafuta uongozi kwa kutoa rushwa, hawana maono wala dira ya kile ambacho watakifanya maada ya kuingia madarakani na ufanisi wao katika kutekeleza jukumu ambalo watapewa utakuwa mdogo kwa sababu watakachoangalia ni maslahi binafsi kwanza.

Aliongeza kuwa, rushwa ni tatizo kubwa katika nchi nyingi duniani ambayo inachangia kuharibu utendaji wa viongozi wengi, kuvuruga amani na utulivu wa Mataifa mbalimbali.

"Viongozi wengi wanaotafuta madaraka hutumia pesa nyingi na wakipata madaraka, hufikiria namna ya kurudisha pesa zao kwanza badala ya kuwatumika wananchi.

"Kimsingi viongozi wanaoingia madarakani kwa rushwa hawawezi kupambana na rushwa wala kuwakemea viongozi wenye tabia hiyo," alisema Bw. Sumaye ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa viongozi wastaafu mwenye nia ya kutaka kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Alisema kupambana na rushwa kunahitaji viongozi waadilifu, wasiotanguliza masilahi binafsi, wenye dira ambapo kiongozi anayeweza kupambana na rushwa ni yule asiyekuwa na hulka ya kutoa rushwa.

"Tunahitaji viongozi wenye dhamira ya kupambana na rushwa, kuikemea na kusimamia dhana ya utawala bora," alisema.

Akizungumzia rasilimali za nchi, alisema Tanzania ni moja ya Mataifa kadhaa duniani iliyobahatika kuwa na rasilimali nyingi zenye utajiri mkubwa lakini watu wake ni maskini kutokana na kukosekana wasimamizi wazuri wa rasilimali hizo na uwepo wa viongozi wanaojali maslahi binafsi.

"Tanzania ina utajiri mwingi kama madini, mbuga za wanyama, mlima Kilimanjaro, mito, maziwa na misitu...cha ajabu utakuta watu wanakata misitu ovyo na kuondoa uoto wa asili, kuchoma moto misitu, kufanya biashara haramu ya mbao na mkaa, hali hii inachangiwa na usimamizi mbovu wa rasilimali hizo.

Alisema wingi wa rasilimali zilizopo nchini hauendani na maisha anayoishi mwananchi bali watu wachache ndio wanaonufaika.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment