HALMASHAURI KUU YA CCM (NEC) KUKUTANA KUJADILI MCHAKATO WA KURA YA MAONI NA UCHAGUZI MKUU!!


 Wakati Rais Jakaya Kikwete akitarajiwa kutua mjini hapa mwishoni mwa wiki hii kuendesha kikao cha Baraza la Mawaziri, huku Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), ikitarajiwa kukutana muda wowote kuanzia wiki ijayo kujadili pamoja na mambo mengine, mchakato wa Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo CCM imeanza hatua ya kwanza kuelekea Uchaguzi Mkuu wakati kikao cha NEC kikitarajiwa kufanyika mwezi huu kupanga tarehe na utaratibu mzima wa uchukuaji na urejeshaji fomu kwa wagombea wa chama katika ngazi za urais, ubunge na udiwani.
Tayari Rais Kikwete amepuliza kipenga cha mbio za urais kwa CCM katika sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa kwake wakati wa maadhimisho yaliyofanyika mkoani Ruvuma, akiwataka wenye sifa wajitokeze kuchukua fomu huku akisema: “Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu wa kupata rais wa awamu ya tano, utakuwa wa kihistoria.”
Hadi sasa makada wa CCM waliotangaza nia kuwania urais ni Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba; Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Pia wapo wanaotajwa kwamba huenda wakajitokeza mchakato huo utakapoanza rasmi ambao ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba; Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Wengine ni Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha - Rose Migiro; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.
Katika kikao cha NEC ambacho kitakutana muda wowote wiki ijayo inadaiwa kuwa suala la kura ya Maoni huenda likaibua mjadala mkubwa kutokana na kuibua mijadala mingi hasa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa muda wa utekelezwaji wake hautoshi.
Viongozi wa vyama vya upinzani wameshatangaza kuwa hawatashiriki katika mchakato huo.
Jana, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia aliwasilisha bungeni hoja za kutaka kuahirishwa kwa mchakato huo akisema uko nyuma ya wakati.
Mbatia alitoa hoja hiyo alipokuwa akiomba mwongozo wa Spika, mara baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika: “Mwenyekiti nchi yetu hapa tulipo leo hii hakuna daftari la kudumu la wapiga kura. Julai 9, mwaka jana Tume ya Uchaguzi ya Taifa iliwakutanisha wadau na wakaambiwa daftari la kudumu la wapiga kura lililopo limechafuka, limechafuliwa ni chafu na halifai kutumika tena. Wakatwambia wameanzisha utaratibu wa kuandikisha upya wapigakura wote wa Tanzania na mfumo watakaotumia ni mfumo wa BVR. Walituhakikishia zoezi la kuandikisha wapigakura lingeanza Septemba 9 mwaka jana mwanzoni.”
Hata hivyo, alisema jambo hilo halikufanikiwa na badala yake Serikali ilisema lingefanyika Oktoba na Novemba. Desemba yalifanya majaribio katika majimbo matatu; Kawe, Kilombero na Katavi lakini yalikuwa na changamoto nyingi.
Akijibu mwongozo huo jana jioni, Mwenyekiti wa Bunge Mussa Azzan Zungu alisema Kamati ya Uongozi imeamua kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ifanye mkutano na wadau wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kujadili maandalizi ya Kura ya Maoni.
Alisema Kamati Bunge ya Katiba na Sheria imepewa jukumu la kufuatilia suala hilo ili kuhakikisha kwamba mkutano huo unafanyika na kuwasilisha taarifa kwenye kamati ya uongozi.
Wakati hayo yakitokea bungeni, taasisi za wanaharakati wa Zanzibar zilisema Kura ya Maoni ni batili kutokana na kukiuka sheria.
Mbali na masuala hayo, imelezwa kuwa kikao hicho kitapokea taarifa ya utekelezwaji wa maazimio ya Bunge kuhusu sakata la uchotwaji fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kikao hicho kinafanyika ikiwa ni takriban siku 20 baada ya kufanyika kwa kikao cha Kamati Kuu kilichokutana Zanzibar.
Alipoulizwa kuhusu taarifa hizo za kuwepo kwa kikao cha NEC, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: “Hakuna kitu kama hicho… najua mnataka kuandika, lakini ninachotaka kusema, hakuna mkutano huo.

“Nitashangaa kesho nikiona mmeandika haya… lakini nimewazoea. Hata mkiandika CCM itashinda.”
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment