SAKATA LA ESCROW; JAJI WARIOBA ALIKOSOA BUNGE!!

Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
WAZIRI Mkuu Mstaafu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amekosoa kitendo kilichofanywa na bunge wakati wa kutoa mapendekezo ya waliohusika na mgawo wa fedha za Tegeta Escrow, akisema walikiuka katiba kwa kuingilia mamlaka ya mhimili mwingine.

Akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kilichorushwa na televisheni ya ITV, juzi alisema Jaji Warioba kilichotokea bungeni wakati wa sakata la escrow ni matokea ya kupingwa kwa mambo muhimu waliyokuwa wameyaweka kwenye rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema maoni ya wananchi yalitaka kuheshimiwa kwa mgawanyo wa madaraka kwa kila mihimili kuheshimu mwingine, hivyo bunge katika sakata hilo halikupaswa kutoa maazimio ya kufukuza watendaji wa serikali kama lilivyofanya.

"Bunge'' kazi yake kwa mujibu wa katiba ni kuisimamia serikali si kufukuza watendaji wa serikali, si sawa na wala si haki kwani Serikali ni mhimili kamili kikatiba unaojitegemea, unaopaswa kuheshimiwa na una mkuu wake ambaye ni Rais...ambaye hapaswi kulazimishwa kufanya jambo,"alisema.
Alisema Katiba iliyokuwa imependekezwa na wananchi ililenga kuondo migongano kama hiyo ambayo imekuwa ikikumba nchi. Alisema kitendo cha wabunge kutoa maazimio ya kufukuza watendaji wa Serikali wakijua kuwa wanaosema wafukuzwe nao ni wabunge wenzao si sawa.

Alisema suala la katiba mpya bado lipo mikononi mwa wananchi na serikali haipaswi kukata tamaa kwa lolote litakalotokea ambapo hatua iliyofikiwa itaheshimiwa na wakati wowote kama itashindikana mwaka huu itafanikiwa wakati mwingine.
 
Amesema sheria ya maadili ya viongozi wa umma haina nguvu ya kukabiliana na mmomonyoko huo na  inakosa meno kwa sababu inasimamiwa na watu walewale wasiotaka ‘kuguswa’.



“Hatuwezi kuendelea kama ilivyo sasa bila kuchukua hatua kali na nzito kushughulikia maadili. Lazima kuna siku suala hili litaingia katika Katiba tu,” alisema.

Jaji Warioba ametoa kauli hiyo ikiwa zimepita siku mbili tangu Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutaja viongozi wa umma itakaowahoji kutokana na kuhusika katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.

Miongoni mwao yupo kigogo wa Ikulu mwenye cheo cha mnikulu, Shaban Gurumo, aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na mwanasheria mkuu wa zamani, Andrew Chenge.

Katika rasimu ya pili ya Katiba, Tume ya Jaji Warioba ilipendekeza miiko na kanuni za uongozi kama tunu za Taifa, lakini Bunge Maalumu la Katiba iliyaondoa na kuyaweka katika msingi wa utawala bora.

Mara kadhaa Jaji Warioba amekuwa akihoji kuwa uzalendo na uadilifu si mpaka mtu awe kiongozi, kwamba mambo hayo mawili si misingi ya utawala bora ni misingi ya kitaifa na inamhusu kila Mtanzania.

Akifafanua zaidi suala la maadili katika kipindi hicho, Jaji Warioba alisema tume yake iliangalia sheria ya maadili ikaona haina nguvu sana na inategemea kiongozi mmoja na ndiyo maana waliingiza suala hilo katika rasimu ya Katiba.

“Tuna sheria ya maadili lakini haina nguvu kwa sababu wanaoisimamia ni walewale. Nchi za Ufilipino (Philippines), Afrika Kusini, Namibia na Kenya walikuwa na sheria lakini haikuwa na nguvu na iliwahusu watu walewale. Waliamua kuweka maadili katika Katiba ili waweze kulitekeleza vizuri,” alisema.

Alisema maadili pia yanawahusu viongozi lakini wakati huo huo viongozi hao ndiyo wanaosimamia sheria ya maadili, hivyo hawawezi kukubali liwemo jambo litakalowadhuru.

Jaji Warioba alieleza jinsi Azimio la Arusha lilivyokuwa na nguvu, akifafanua kuwa suala la maadili lilijipambanua wazi  na waliokuwa wakitenda mambo kinyume walijiondoa wenyewe bila kusubiri kuondolewa.

Akigusia suala la maadili na sakata la mabilioni ya fedha yaliyochotwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow alisema, “Katika suala la escrow niliuliza nani msafi…, we subiri tu si tunakwenda katika uchaguzi mkuu viongozi watakuwa na fedha nyingi sana.”



Akizungumzia daftari wa wapigakura na upigaji wa Kura ya Maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa, alisema, “Nia ya kupitisha Katiba mpya mapema ilikuwa na lengo la kuitumia katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, lakini inahitaji maandalizi. Mfano Katiba Inayopendekezwa ina sehemu ya Tume ya Uchaguzi na kama ukiipitisha, utaunda upya tume hiyo na suala hilo linahitaji muda.”

Alisema ili kufanikisha uundwaji wa tume hiyo ni lazima Bunge likutane, lakini mpaka itakapofika siku ya kuipigia kura Katiba hiyo na kuipitisha, Bunge litakuwa limekwishakaa na hakutakuwa na uwezekano wa kubadili lolote.

“Hakuna haja ya kuharakisha, ni vizuri twende taratibu ili tusije tukafanya makosa ambayo yatatuletea matatizo,” alisema.

Aliongeza, “Itakuwa vizuri kama kura ya maoni ikasitishwa mpaka mwaka 2016. Inaonekana tutalazimika kusubiri na hii inatokana na matatizo tu ya kawaida ya kutokuwa na daftari la Wapigakura.


Jaji Warioba pia aligusia kitendo cha wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuruhusiwa kugombea nafasi za kisiasa baada ya kumalizika kwa Bunge hilo, akisema kuwa hilo lilikuwa kosa kubwa.

“Uganda tume ilipomaliza kazi, wananchi walichagua Bunge la Katiba na sharti moja ni kwamba ukiingia katika Bunge hilo hauruhusiwi kugombea uongozi. Walijua kazi yao ni kupitisha Katiba tu,” alisema.

Alisema kosa lililofanyika nchini ni kuruhusu wabunge waliopitisha Katiba kugombea, hivyo kuwafanya baadhi kuondoa masuala ya msingi waliyoona kuwa ni kikwazo kwao katika uchaguzi.

“Nadhani hiyo ni kasoro tuliyokuwa nayo na tulipeleka watu ambao wana malengo na Katiba kwa manufaa yao binafsi,” alisema.

Kuhusu maridhiano kuelekea upigaji wa Kura ya Maoni alisema, “Suala la maridhiano lilipofika kwenye vyama vya siasa likabadilika na sasa tunazungumzia maridhiano ya vyama vya siasa. Maridhiano ya vyama vya siasa siyo lazima yawe maridhiano ya wananchi.”

 Jaji Warioba pia alizungumzia suala la muungano, kueleza historia ya mfumo wa uteuzi wa viongozi wa Serikali ya Muungano na Zanzibar ili kuondoa dhana ya upande mmoja kuonekana unatoa viongozi wengi kuliko mwingine.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment