KATIKA msimu wa nanasi, huna sababu zakujiuliza
kwa nini usile mananasi kwa wingi.Zipo Faida zinazoweza kupatikana kwenye nanasi ni
nyingi ambazo zinaweza kuwa kama kinga na tiba kwa baadhi ya matatizo ya kiafya
ambayo pengine yangehitaji mtu kwenda hospitali kupatiwa dawa, tena kwa gharama
kubwa.
Miongoni mwa faida hizo ni hizi
zifuatazo:
USAGAJI WA CHAKULA
Nanasi lina virutubisho
vinavyouwezesha mfumo wa usagaji chakula tumboni kufanya kazi yake ipasavyo,
pindi mfumo huu unapowezeshwa kufanyakazi yake vizuri, mtu huweza kupata choo
laini na kwa wakati kama inavyotakiwa. Hivyo wenye kula tunda hili kwa wingi
hawawezi kusumbuliwa na tatizo la ukosefu wa choo. Aidha, kwa mujibu wa tafiti
nyingine, nanasi pia lina virutubisho vyenye uwezo wa kupunguza au kuzuia
uvimbe tumboni.
KINGA YA MWILI
Nanasi linaaminika kuwa miongoni mwa
matunda yenye chanzo kizuri cha vitamin C ambayo kazi yake mwilini ni kuupa
mwili kinga dhidi ya ‘wavamizi’ mbalimbali (freee radicals), ambao wanapoingia
mwilini kazi yao hua ni kuharibu chembechembe hai za mwili. Vile vile
‘wavamizi’ hao wanapoweka makazi mwilini, huziba mishipa ya damu na hivyo
kusababisha magonjwa ya moyo na mengine mengi, ikiwemo kansa ya tumbo.
Kwa kuongezea, vitamini C inaaminika
kuwa na uwezo mkubwa wa kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili, hivyo kuifanya kuwa
kinga ya magonjwa madogo madogo kama vile mafua, kikohozi, homa na maambukizi
mengine. Unapokuwa na kiwango cha kutosha cha vitamin hiyo, bila shaka kinga
yako ya mwili itakuwa imeimarika na hivyo utakuwa umejiepusha na maambukizi
mbalimbali.
CHANZO CHA MADINI
Mbali ya kuwa ni chanzo kizuri cha
vitamin C, nanasi pia ni chanzo kizuri cha madini aina ya ‘manganese’ ambayo
yanaaminika kuwa na uwezo wa kuboresha ufanisi wa vimeng’enyo mbalimbali vya
mwili, vikiwemo vya kuzalisha nishati na kinga ya mwili. Halikadhalika tunda
hili lina kiwango cha kutosha cha vitamin B1 (thiamin).
KUIMARISHA NURU YA MACHO
Inawezekana karoti ikawa ndiyo
inayojulikana na watu wengi kuwa na uwezo wa kuimarisha nuru ya macho, lakini
nanasi nalo lina uwezo mkubwa wa kuimarisha nuru ya macho. Utafiti unaonesha
kuwa ulaji wa tunda hili na matunda mengine, kiasi cha milo mitatu kwa siku,
kunaondoa hatari ya kupungua kwa nuru ya macho kwa asilimia 36 kwa watu wazima.
NANASI LILILO BORA
Nanasi lililo bora ni lile kubwa na
lililoiva vizuri. Wakati ni kweli kwamba nanasi kubwa lina nyama nyingi kuliko
nanasi dogo, lakini hakuna tofauti ya ubora wa virutubisho kati ya nanasi dogo
na kubwa, ilimradi lisiwe limeoza au lenye michubuko mingi. Hivyo chagua nanasi
lilioiva vizuri na lenye kunukia.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi
karibuni na Chuo Kikuu cha Innsbruck, nchini Austria, unasema kuwa tunda
linapokuwa limeiva zaidi ndivyo ambavyo virutubisho vyake vinapokuwa bora. Kwa
kula nanasi ambalo halijaiva vizuri, huenda ukajikosesha faida zinazopatikana
kwenye tunda hilo kama inavyoelezwa.
Mara baada ya nanasi kumenywa na
kukatwa vipande, linatakiwa kuliwa mara moja, iwapo litahifadhiwa kwenye jokofu
kwa ajili ya kuliwa baadaye, njia sahihi ya kuhifadhi ni kuliweka kwenye chombo
chenye mfuniko (container) ili kuhifadhi virutubisho vyake kwa kipindi hadi cha
siku tano bila kupoteza ubora wake, ikiwa pamoja na ladha.
0 comments:
Post a Comment